Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za
rambirambi kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu
Tarcisius Ngalalekumtwa kuomboleza kifo cha Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa
Jimbo la Moshi.
Askofu Msarikie
aliaga dunia jana, Alhamisi, Februari 7,2013 katika hospitali moja ya mjini
Nairobi, Kenya ambako alikuwa anatibiwa akiwa na umri wa miaka 82.
Rais Kikwete katika
salamu zake za rambirambi kwa Rais huyo wa TEC amesema: “Nimehuzunishwa na
kusikitishwa na taarifa za kifo cha Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie ambaye
nimejulishwa kuwa aliaga dunia jana mjini Nairobi, Kenya ambako alikuwa anapata
matibabu hospitalini.”
Amesema Rais Kikwete:
“Askofu Msarikie ambaye alistaafu rasmi mwaka 2007 baada ya kuliongoza Jimbo la
Moshi kwa miaka 22, atakumbukwa kwa mengi. Alikuwa kiongozi hodari wa kiroho.
Alikuwa pia mwalimu mwenye sifa za kutukuka. Askofu alitoa mchango mkubwa
katika elimu na mchango wake katika maendeleo ya sekta hiyo hautasahahulika
kamwe. Alikuwa mkereketwa wa elimu na alichangia sana kuinua kiwango cha elimu
katika Mkoa wa Kilimanjaro.”
“Kwa niaba ya
serikali ninayoiongoza na kwa niaba yangu mwenyewe, nakutumia wewe Baba Askofu
Ngalalekumtwa salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo cha
Baba Askofu Msarikie. Aidha, nakusihi upokee salamu zangu za pole nyingi kwa
viongozi wote na waumini wa Kanisa Katoliki katika Jimbo la Moshi na Tanzania
nzima kwa kuondokewa na kiongozi wao, askofu wao na mwalimu wao,” amesema Rais
Kikwete na kumalizia:
“Baba Askofu
Ngalalekumtwa, naungana nawe, viongozi wenzake na waumini wote wa Kanisa
Katoliki Tanzania kuomboleza msiba huu mkubwa. Msiba huu ni wetu sote na
machungu ni yetu sote. Aidha, naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu,
Mwingi wa Rehema, aiweke pema poponi roho ya Marehemu Askofu Amedeus Msarikie.
Amen.”
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment