Timu ya Taifa ya Burkina Faso
Timu ya Taifa ya Nigeria
 Timu ya Taifa ya  Mali
Timu ya Taifa ya Ghana

Timu ya taifa ya Nigeria (Super Eagles) imetinga hatua ya Nusu Fainali mara baada ya kuikwanyua Ivory Coast kwa magoli 2 - 1 katika michuano ya fainali za mataifa AFCON-2013 inayoendelea huko nchini Afrika Kusini.

Nigeria walikuwa wa kwanza kufunga goli kupitia kwa Emmanuel Emenike katika dakika ya 43 ya kipindi cha kwanza ambapo mpaka mapumziko timu Tembo wa Afrika Magharibi Ivory Coast walikuwa nyuma kwa bao hilo. Kipindi cha kwanza kilitawaliwa zaidi na Nigeria Super Eagles.

Hata hivyo kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Ivory Coast walionekana kuja na mfumo mpya ulioonekana kuwazidi Nigeria na kuwafanya  Ivory Coast kujipatia goli la kusawazisha kupitia kwa Cheikh Tiote katika dakika ya 50 lakini zikiwa zimebakia dakika 13 kabla ya mchezo kuisha, Sunday Mba akaukwamisha mpira  kimiani  na kuandika goli la pili baada ya kuizidi maarifa ngome ya Ivory Coast.

Ivory Coast mwaka jana walitinga fainali na kufungwa na bingwa wa fainali hizo Zambia maarufu kama Chipolopolo kwa mikwaju ya penati.Huenda hizi zikawa Fainali za mwisho kwa gwiji na mkongwe wa timu hiyo Didier Drogba kuitumikia timu hiyo.

Katika mchezo wa pili Burkina Faso wamefanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kuifunga kwa tabu timu ya Togo katika dakika ya 105 bao lililofungwa  na mchezaji Jonathan Pitroipa aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa kona.. 

Awali timu hizi zilitoka suluhu jambo lililowafanye waongezewe dakika 30 za nyongeza.

Mchezo huu ulikuwa mkali na wa kasi kwa timu zote ingawa Togo walionekana kuchoka katika kipindi cha dakika za nyongeza. Hadi mwamuzi anamaliza mchezo, Burkina Faso 1 Togo 0.

Kwa matokeo haya timu za Burkina Faso na Nigeria zinaungana na timu za Mali na Ghana katika Finali za AFCON 2013. 

Ratiba inaonesha kuwa nusu fainali itafanyia tarehe 6 siku ya Jumatano mwezi huu aambapo Ghana itacheza na Burkina Faso wakati Nigeria ikimenyana na Mali.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top