KUSITISHWA
MATUMIZI KATIBA MPYA:TFF KUJADILI TAMKO LA WAZIRI MKANGARA.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella
Mukangara
Sekretarieti
ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepokea barua ya Serikali
ikielezea uamuzi wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella
Mukangara kutengua uamuzi wa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini
kuidhinisha marekebisho ya Katiba ya TFF toleo la 2012.
Baada
ya kupokea barua hiyo jana alasiri (Februari 25 mwaka huu), Sekretarieti
iliwasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye ameagiza kuitishwa kikao cha
dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tamko hilo.
Kikao
hicho cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitafanyika Jumamosi (Machi 2 mwaka huu)
jijini Dar es Salaam.
Waziri
Mkangara ameagiza kusitishwa kwa matumizi ya katiba mpya ya TFF iliyofanyiwa
marekebisho mwaka 2012 na kupitishwa rasmi kwa matumizi mwaka 2013.
Moja
ya sababu alizotaja waziri Mkangara ni kutofuata taratibu za kurekebisha katiba
ambapo mkutano mkuu wa TFF lazima uridhie mabadiliko hayo kwa kupigia
kura.Lakini TFF ilitumia njia ya waraka kwa wajumbe kwa madai kukosa fedha za kuitisha mkutano
mkuu na kuwahudumia wajumbe husika.
Dakta
Fennela Mkangara ameagiza kusitishwa mara moja kwa matumizi ya katiba ya mwaka
2012 na itumike ya mwaka 2006 ambayo
inatambuliwa na baraza la michezo BMT na Wizara yenye dhamana ya michezo.
Katika
hatua nyinigine waziri Mkangara amesema atamuondoa kwenye nafasi yake msajili
wa vyama vya michezo kutokana na kuvurunda katika suala hilo ambalo
limesababisha mgongano usio wa lazima katika mchakato wa uchaguzi ambao
umesitishwa na shirikisho la kandanda duniani FIFA.
Waziri
huyo alisema lazima hata maafisa wa FIFA waambiwe ukweli mtupu kuhusiana na
maagizo hayo na mahala ambapo TFF iliboronga kwa manufaa ya mpira wa miguu hapa
nchini.
KOCHA
AZAM AFUNGIWA KWA KUCHOJOA BUKTA
Kocha
Mkuu wa Azam, Stewart John Hall
Kocha
Mkuu wa Azam, Stewart John Hall amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh.
500,000 kwa kushusha bukta yake na kumlalamikia mwamuzi msaidizi wakati wa
mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu yake na Kagera Sugar
iliyochezwa Januari 26 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es
Salaam.
Adhabu
hiyo imetolewa na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
iliyokutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za michuano ya VPL na Ligi Daraja
la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 inayoendelea hivi sasa na kufanya uamuzi
mbalimbali.
Naye
Kocha Msaidizi wa timu ya Mgambo Shooting, Denis Mwingira ametozwa faini ya sh.
500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar
iliyochezwa Oktoba mwaka jana katika Uwanja wa Manungu.
Ally
Jangalu ambaye ni Kocha Msaidizi wa Polisi Morogoro naye ameangukiwa na rungu
la Kamati ya Ligi kwa kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kutolewa kwenye
benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu. Alitenda kosa hilo kwenye
mechi kati yao na Kagera Sugar iliyochezwa Novemba 10 mwaka jana Uwanja wa
Kaitaba mjini Bukoba.
Matukio
ya aina hiyo kwa kocha Jangalu yamekuwa ya kujirudiarudia ambapo Oktoba 13
mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam iliyochezwa mjini Morogoro aliondolewa na
mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu yake wacheze rafu.
Naye
Kocha wa timu ya Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho amepigwa faini ya
sh. 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya mechi dhidi ya Transit Camp
iliyofanyika Novemba 4 mwaka jana Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.
Pia
Kocha wa Burkina Faso, Hasheem Mkingie amepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya
kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya FDL dhidi ya
Mkamba Rangers.
Kiongozi
wa Majimaji, Joseph Nswila ambaye aliingia uwanjani baada ya mechi dhidi ya
Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi amefungiwa miezi sita.
Vilevile
timu ya Azam imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye
mechi kati yao na JKT Oljoro iliyochezwa Novemba 7 mwaka jana katika Uwanja wao
wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Pia
Coastal Union imetozwa faini ya sh. 500,000 kutokana na washabiki wake
kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao dhidi
ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Nayo
klabu ya African Lyon imepigwa faini ya sh. 500,000 kwa timu yake kugoma
kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi
dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Oktoba 24
mwaka jana.
Timu
ya Burkina Faso ya Morogoro imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na kuonesha
vitendo vya ushirikina kabla ya mechi yao dhidi ya Mbeya City iliyochezwa
Oktoba 24 mwaka jana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Faini
ya ushirikina ya sh. 200,000 pia imepigwa timu ya Pamba baada ya kuonesha
vitendo hivyo kwenye mechi yao dhidi ya Mwadui iliyochezwa Novemba 4 mwaka jana
Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Nayo
Mkamba Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 baada ya washabiki wake kumtolea
lugha chafu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA), Hamis
Semka na kumrushia chupa za maji mwamuzi wa mezani katika mechi dhidi ya Mbeya
City iliyochezwa mjini Morogoro.
Polisi
Dodoma imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kuvamia
uwanjani na kutaka kuwapiga waamuzi katika mechi yao dhidi ya JKT Kanembwa na
kusababisha mipira miwili ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA)
kupotea.
Pia
klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa timu zao kuchelewa kufika uwanjani
au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting). Klabu
hizo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans, Simba, Green Warriors, Majimaji,
Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa, Moro United.
Mchezaji
Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal Union alikwenda
jukwaani na kuanza kupigana na washabiki. Pia kipa wa timu ya Transit Camp,
Baltazar Makene baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka uzio na kwenda kupigana
na washabiki.
Kwa
vile masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu yamepelekwa kwenye Kamati ya
Nidhamu inayoongozwa na Kamishna wa Polisi (CP) mstaafu Alfred Tibaigana kwa
ajili ya kuchukuliwa hatua.
MWAMUZI
FIFA, MAHAGI WAONDOLEWA VPL
Mwamuzi
Msaidizi wa FIFA, Ferdinand Chacha ameondolewa kuchezesha mechi za VPL baada ya
kupata alama za chini kwenye mechi kati ya African Lyon na Simba iliyochezwa
mwezi uliopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Waamuzi wanaopata alama 6.5 au
chini ya hapo kati ya 10 zinazohitajika pia wanaondolewa kwenye mechi za VPL na
FDL.
Waamuzi
wengine walioondolewa kwa kutomudu mechi walizochezesha za VPL ni Mathew Akrama
(Yanga vs Simba), Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba), Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa
Sugar).
Walioondolewa
kwa kupata alama za chini ni Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu), Methusela
Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto Africans vs
Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe
(Toto Africans vs Mtibwa Sugar).
Masoud
Mkelemi aliyekuwa mwamuzi wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro United na
Villa Squad ameondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi
(Pre-match meeting) na alichelewa kwa dakika tano kufika uwanjani.
MAKAMISHNA
VPL/FDL WASIMAMISHWA, WAONYWA
Baadhi
ya makamishna wa VPL na FDL wameondolewa na wengine kusimamishwa kusimamia
mechi za ligi hizo kutokana na upungufu kwenye ripoti zao au kutowasilisha
kabisa ripoti hizo TFF baada ya mechi.
Kamishna
Mohamed Jumbe aliyesimamia mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba ameondolewa
kwenye orodha ya makamishna kutokana na ripoti yake kuwa na upungufu.
Makamishna
wa mechi kati ya JKT Oljoro vs Yanga (Hakim Byemba), JKT Oljoro vs Kagera Sugar
(Salum Kikwamba), Toto Africans vs African Lyon (Charles Komba), Coastal Union
vs JKT Oljoro (Mohamed Nyange) wamesimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao
TFF.
Kwa
upande wa FDL makamishna waliosimamishwa hadi watakapowasilisha ripoti zao TFF
ni wa mechi kati ya Kurugenzi vs Polisi Iringa, Morani vs Mwadui, Polisi Mara
vs Pamba, Polisi Mara vs Mwadui, Morani vs JKT Kanembwa na Pamba vs Polisi
Dodoma.
Wengine
ni Mwadui vs JKT Kanembwa, Polisi Tabora vs Morani, Polisi Dodoma vs Polisi Mara,
Polisi Tabora vs Mwadui, Polisi Mara vs Morani, JKT Kanembwa vs Polisi Mara,
Morani vs Rhino Rangers na Small Kids vs Mkamba Rangers.
Kamati
ya Ligi imewakumbusha makamishna wote kuwa ni jukumu lao kuhakikisha ripoti zao
zimefika TFF na kurekebisha upungufu wa jinsi ya kuripoti matukio yanayotokea
uwanjani. Licha ya kutuma nakala kwa njia ya email, wanatakiwa pia kuwasilisha
ripoti halisi (original) TFF.
MECHI
YA SIMBA, MTIBWA YAINGIZA MIL 62/-
Mechi
namba 121 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa juzi (Februari 24 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Mtibwa Sugar kuibuka
ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba imeingiza sh. 239,686,000.
Watazamaji
10,669 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000,
sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh.
14,577,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh.
9,467,694.92.
Kiingilio
cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo
walikuwa 9,491 na kuingiza sh. 47,455,000 wakati idadi ndogo ya washabiki
ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 105 na kuingiza sh.
2,100,000.
Mgawo
mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,412,162.26, tiketi sh.
3,183,890, gharama za mechi sh. 4,447,297.36, Kamati ya Ligi sh. 4,447,297.36,
Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,223,648.68 na Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,729,504.53.
VUMBI
LA VPL KUENDELEA JUMATANO
Michuano
ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho
(Februari 27 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika viwanja
tofauti.
Vinara
wa ligi hiyo Yanga wataikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000 (viti vya bluu na kijani), sh. 8,000 (viti
vya rangi ya chungwa), sh. 15,000 (VIP C na B) na sh. 20,000 (VIP A).
0 comments:
Post a Comment