WAKATI mjadala wa nani anafaa kuwa rais wa awamu ya tano wa Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania unashika kasi kila kona ndani na nje ya nchi, jina la Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa linazidi kung’ara, Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Tafiti za hivi karibuni zilizofanywa na taasisi mbili tofauti, zimeonesha kuwa Dk. Slaa hashikiki miongoni mwa watu wa vyama tofauti wanaotajwa kutaka kuwania urais mwaka 2015.
Katika utafiti uliofanywa hivi karibuni na mtandao maarufu duniani wa Jamii Forum kwa kuuliza “nani ungependa agombee urais mwaka 2015 kwa tiketi ya CHADEMA na CCM”, majina manne yalipambanishwa, mawili kutoka CCM na mawili CHADEMA.

Waliopambanishwa kutoka CCM ni pamoja na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, ambao wamekuwa wakitajwa kuibua makundi yanayosigana kutaka urais mwaka 2015.
Kwa upande wa CHADEMA, kura hizo za maoni zilizoanza Julai, mwaka jana ziliwakutanisha Dk. Slaa na Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.

Kwa mujibu wa utafiti huo, jumla ya watu 1,188 walishiriki kuwapigia kura wagombea wa CHADEMA, Dk. Slaa na Zitto, wakati 375 waliwapigia Lowassa na Membe.

Matokeo ya utafiti huo, yalionesha kuwa Dk. Slaa alikuwa juu kwa kupigiwa kura 1,007, sawa na asilimia 84, wakati Zitto aliibuka na kura 181, sawa na asilimia 15.

Kwa upande wa CCM, Lowassa aliibuka na kura 164 kati ya wapiga kura 375 wakati Membe aliibuka na kura 67, sawa na asilimia 17.87.

Aidha, kwa mujibu wa matokeo hayo, wapiga kura 144 walipiga kura ya kutomuunga mkono mgombea yeyote kati ya Membe na Lowassa.

Matokeo ya jumla yalionesha kuwa, Dk. Slaa anaongoza kwa kura 1,007 na kufuatiwa na Zitto (181), Lowassa (164) na Membe kura 67.

Katika ufatiti mwingine uliofanywa na Shirika la Utafiti la Synovate na matokeo yake kutangazwa jana, mchuano mkali upo kati ya vigogo tisa.

Kwa mujibu wa utafiti huo, endapo uchaguzi mkuu ungefanyika sasa, Dk. Slaa anaongoza kwa kupata asilimia 17.

Hata hivyo, licha ya kuongoza, Dk. Slaa ameporomoka kwa asilimia 25 ikilinganishwa na matokeo ya utafiti kama huo uliofanywa na taasisi hiyo mwaka 2011 ambapo alipata asilimia 42.

Dk. Slaa anafuatiwa kwa mbali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amefungana na Zitto, kila mmoja akipata asilimia tisa.

Kadhalika, umaarufu wa Pinda ambaye anaongoza miongoni mwa wagombea wa CCM, umeshuka kwa asilimia tatu kutoka 12 za mwaka juzi, wakati Zitto ameendelea na kiwango kilekile cha asilimia tisa alizopata katika utafiti uliotangulia.

Wengine wanaofuata na asilimia walizopata kwenye mabano ni Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli (8), Lowassa (7) na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba (5).

Pia wamo Membe (4) ambaye amefungana na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe (4) na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (2).

Ikilinganishwa na utafiti wa 2011, Lipumba ameporomoka kwa asilimia tisa, Lowassa amepanda kwa asilimia sita, Dk, Magufuli asilimia nne, Mbowe na Membe wamepanda kwa asilimia mbili kila mmoja, wakati Sitta amebaki katika kiwango kilekile cha asilimia mbili.

Hata hivyo, utafiti huo umeonesha kuwa wananchi ambao hawana uamuzi wa kuchagua mtu yeyote kati ya hao kwa sasa, ni asilimia 18, likiwa ni ongezeko la asilimia 12 ikilinganishwa na utafiti uliotangulia.

Hata hivyo matokeo ya kura hizo za maoni sio rasmi kwani kati ya majina yote yaliyoshirikishwa, hakuna hadi sasa aliyekwishatangaza nia ya kuwania urais 2015.

Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Anne Makinda, anaelezewa kumharibia mbio za urais mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Dk. Asha Rose Migiro.

Duru za siasa kutoka ndani ya chama hicho tawala, zinasema kuwa mwenendo na utendaji duni wa Makinda katika kuliongoza Bunge, kumesababisha baadhi ya vigogo wa CCM kuacha kufikiria kumpa nafasi ya kuwania urais Dk. Migiro ili kuua makundi.

Vyanzo vyetu vya habari vililidokeza gazeti hili kuwa, awali baadhi ya vigogo wa CCM wenye ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho, walifikiria kumpeleka Dk. Migiro kuwania urais ili kuua makundi yanayosigana hivi sasa kutaka kiti hicho.

Stahili hiyo ndiyo iliyotumika wakati wa kinyang’anyiro cha uspika ambapo baada ya kubaini kuwapo mpasuko mkubwa wa wana CCM katika nafasi hiyo, Kamati Kuu ya CCM iliamua kwamba ni zamu ya wanawake kuongoza kiti hicho, hivyo wanaume waliogombea walikosa sifa.

Habari zinasema kuwa utendaji kazi wa Spika Makinda, hasa katika kipindi hiki, umemponza Dk. Migiro kwani baadhi ya wana CCM hawana imani na mwanamke kushika nafasi hiyo kubwa kabisa ya uongozi nchini.

“Mama Makinda katuangusha. uendeshaji wake wa Bunge unazidi kumfanya Spika wa zamani Samuel Sitta kuonekana bora. Lakini pia amesababisha mawazo tuliyokuwa nayo kuhusu wanawake kuongoza dola, yafifie kabisa,” alisema mmoja wa makada wa CCM.

Ingawa hajatangaza hadharani, lakini Dk. Migiro amekuwa akitajwa chini kwa chini kuwania kiti hicho, hasa kutokana na hatua ya Mwenyekiti wa CCM, taifa, Rais Jakaya Kikwete kumteua kuwa mjumbe wa NEC, na CC ya CCM.

Mwingine aliyeteuliwa na Rais kushika nafasi ya ujumbe wa NEC na CC ni Dk. Salim Ahmed Salim ambaye naye anatajwa kuwania tena urais 2015.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top