Na Christopher Nyenyembe , Mbeya
JESHI la Polisi katika mikoa ya Iringa na Mbeya, limewakamata watu 29 wakiwemo askari wawili wanaotuhumiwa kuwa majambazi hatari waliohusika na matukio ya mauaji na uporaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athuman, aliwaambia waandishi wa habari kuwa miongoni mwa waliokamatwa ni askari Samuel Balumwina (31) mwenye namba MT 85393 kutoka kikosi cha JKT Itende (844KJ) na PC Samuel Kigunye (27) namba G.9101.

Askari hao wanatuhumiwa kuazimisha sare za majeshi hayo kwa majambazi. Na kuongeza kuwa polisi atashtakiwa kijeshi na kuunganishwa na wengine kwa makosa ya mauaji na uporaji wa mali.

Watuhumiwa hao wa ujambazi wanadaiwa kuhusika katika matukio makubwa likiwemo la mauaji ya askari polisi G 68 PC Japhary aliyepigwa risasi ubavuni akiendesha gari la namba PT 0665 lilipokuwa doria Mkwajuni, wilayani Chunya.

Athuman alisema wananchi wa eneo la Mkwajuni wilaya ya Chunya wakiwa na silaha za jadi kwa hasira ya kuuawa kwa askari Japhary, walimshambulia dereva wa gari la majambazi Shaban John (33) ambaye kabla hajafa aliwataja wenzake alioshirikiana nao.
Alisema uporaji huo waliufanya katika kituo cha mafuta cha Matundasi ambapo walipora kiasi cha sh milioni 2.2.

Kamanda Athuman aliwataja watuhumiwa waliomuua PC Japhary kuwa ni Master, Emmanuel Mdendemi, Mashaka Hongole, Manase Kibona, Mashaka George, John Mahenge (39) na Norasco Mabiki(32) ambao licha ya kutuhumiwa kwa mauaji pia wameshiriki katika uporaji kwa kutumia silaha kwa masista eneo la Wanging’ombe, mkoa wa Njombe.

“Mtandao wa watuhumiwa hawa ni wa hatari sana na unaungana na wale kutoka mikoa ya Iringa na Dar es Salaam,” alisema na kuongeza kuwa watu hao pia wanatuhumiwa kuteka na kuwaua Festo Afwilile Kyando (45) mmiliki wa gari lenye namba T586 AGX aina ya Mitsubishi Fuso na utingo wake, Jamali Msangu (26) na miili yao kutupwa porini Februari 2, mwaka huu.

Alitaja watuhumiwa waliowateka, kuwaua na kisha kupora mali kuwa ni Rajabu Mbilinyi (25) mkazi wa jijini Dar es Salaam, Gregory Charles (25), mkazi wa Sabasaba Mbeya na Ghati Mbilinyi (32) mkazi wa Mwanjelwa ambaye inadaiwa gari lake lenye namba za usajili T464 BLX aina ya Noah ndilo lililotumika kufanya mauaji na alikuwa akitumia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na zile za polisi.

Wengine ni Japhet Ng’ang’ana (24) mkazi wa Makambako anayedaiwa kutunza silaha zilizokamatwa na mfanyabiashara wa Makambako na ndugu wawili Hilary Ng’ang’ana (30) na Claud Ng’ang’ana (36) wakazi wa Nyololo, Mafinga wakishirikiana na Francis Sanga (30) mkazi wa Tunduma anayetuhumiwa kupokea mali za wizi baada ya mauaji ya Mafinga.

Silaha zilizokamatwa zikidaiwa kutumika katika matukio ya ujambazi ni bunduki aina ya shortgun iliyofutwa namba, gobore moja lililokamatwa kwenye gari la Gathi Mbilinyi T464 BLX Noah na bastola tatu zilizotengenezwa kienyeji zinazotumia risasi za shortgun zilikamatwa Makambako na Mbeya kwa Hilary.

Polisi pia imekamata risasi 155 zikiwemo 31 za SMG/SAR na 99 za short gun na 25 za bastola, magari matano na sare za majeshi zinazotumiwa kwenye vitendo vya ujambazi.
Kamanda Athuman alisema majambazi tisa waliohusika na mauaji ya Mafinga watasafirishwa chini ya ulinzi mkali kwenda mkoani humo ili kufikishwa mahakamani. 
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top