Wakazi wa Butiama mkoani Mara na vitongoji vyake, wakitazama mabasi mawili yaliyogongana katika eneo la Sabasaba na kusababisha vifo vya watu 36 na wengine zaidi ya 79 kujeruhiwa.
 
Watu 39 wamefariki dunia huku 79 wakijeruhiwa kwenye ajali iliyohusisha magari matatu eneo la Sabasaba, Wilaya ya Butiama, mkoani Mara.

Miongoni mwa waliofariki dunia yumo Mratibu wa ugonjwa wa Ukimwi wa Mkoa wa Mara, Dk Anatoria Ntangeki.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Philip Kallangi alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jana na kwamba marehemu ni 36 na majeruhi 79.
Wakati Kamanda Kallangi akitaja idadi hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Samson Winani alisema amepokea maiti 34 na majeruhi 79.
Dk Winani alisema Dk Ntangeki na mumewe aliyemtaja kwa jina moja la Sayi walikuwa wakisafiri katika moja ya mabasi hayo. Alisema hata hivyo haikufahamika alikuwa akielekea wapi.
Alisema baadhi ya majeruhi wana hali mbaya, lakini hakutoa idadi yao kwani walikuwa bado wanaendelea kuwahudumia.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Angelina Mabula alisema waliofariki dunia ni 39.
Wanajeshi wasimamia
Zoezi la kutambua maiti lilibidi kusimamiwa na askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kutokana na umati wa watu waliokuwa wamefurika nje ya eneo la hospitali.
Wanajeshi walilazimika kwanza kupanga maiti halafu saa 12:00 jioni waliruhusu watu kuingia kwa ajili ya kutambua ndugu zao.
Miongoni mwa majeruhi wa ajali hiyo wamo Mwandishi wa gazeti hili Mkoa wa Mara, Florence Focus ambaye amejeruhiwa paji la uso na miguu, mwingine ni Mwandishi wa Raia Tanzania, Pendo Mwakyembe ambaye amejeruhiwa kichwani na miguuni.
Mashuhuda wa ajali hiyo walisema ilitokea jana saa tano asubuhi, Barabara ya Musoma-Tarime-Mwanza na kuhusisha mabasi mawili na gari ndogo aina ya Toyota Land Cruiser.

Mkazi wa Kijiji cha Sabasaba, Magori Daniel alisema ajali hiyo ilihusisha basi la Mwanza Coach linalofanya safari zake kati ya Musoma na Mwanza na basi lingine maarufu J4 linalofanya safari zake kati ya Sirari-Tarime na Mwanza.
Daniel alisema wakati basi la Mwanza Coach lililokuwa likitokea Musoma kwenda Mwanza lilipofika eneo hilo lilitaka kulipita gari dogo lakini mbele yake kulikuwa na basi la J4, hivyo Mwanza Coach lilipoteza mwelekeo.
Alisema dereva wa Land Cruiser alijitahidi kubaki upande wake, lakini gari lake liligongwa na basi la Mwanza Coach hivyo dereva alipoteza mwelekeo na kuanguka kwenye daraja.
Daniel alisema wakati hali hiyo inatokea ghafla mabasi hayo yaligongana uso kwa uso hali iliyosababisha watu wengi kufariki dunia papohapo, huku wengine wakijeruhiwa vibaya.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Jerome Mugingi alisema Land Cruiser lilikuwa na watu watatu akiwamo dereva, wawili walifariki dunia palepale huku dereva akiokolewa na wasamaria wema na kumpeleka hospitali kwa matibabu zaidi.
Mugingi alisema baada ya ajali waliwasiliana na polisi na muda mfupi baadaye kikosi cha uokoaji wakiongozwa na Kamanda Kallangi, madaktari na watu wengine waliwasili eneo la tukio na kuanza kuokoa majeruhi ambao walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Mara.
Mwandishi wa habari hizi aliwasili hospitalini hapo na kushuhudia umati wa watu, hali iliyolazimisha wasimamizi wa usalama kuzuia watu kuingia ndani ya eneo hilo. Ofisa usalama ambaye hakutaka kutajwa, alisema hawawezi kuruhusu umati wa watu wote kuingia ndani ya eneo la hospitali, lengo ni kutoa nafasi kwa madaktari kuhudumia majeruhi.
“Kama unavyoona umati ni mkubwa, unafikiri tukiwaruhusu kuingia ndani kuna kitakachofanyika kwa hawa majeruhi, tumewazuia kwa lengo la kuwapa nafasi madakati na wauguzi kufanya kazi zao,” alisema.
Pia, mwandishi wa habari hizi alishuhudia miili ya watu 34 iliyofikishwa chumba cha maiti Hospitali ya Mkoa na magari ya watu binafsi, polisi na basi moja linalomilikiwa na Kampuni ya Mwanza Coach.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top