Mapambano kati ya Polisi na wafanyabiashara ndogondogo, maarufu
Machinga, katika eneo la Manzese, yamesababisha kizaazaa na kusababisha
uharibifu wa mali na kufungwa barabara, kusimamisha shughuli zote kwa
zaidi ya saa tatu.
Hali hiyo ilitokea baada ya ‘Wamachinga’ ambao
waliondolewa kwenye maeneo yasiyoruhusiwa kwa biashara wakati wa ziara
ya Rais Barack Obama wa Marekani nchini, kuamua kurejea kwa nguvu katika
maeneo hayo.
Shughuli za kijamii na kibiashara katika eneo la
Manzese, zilisimama kwa takriban saa tatu kutokana na eneo hilo kugeuka
uwanja wa vita na usalama wa wananchi wasiokuwa na hatia kuwa shakani.
Awali polisi walitoa tangazo la kuwataka Machinga
hao kuondoka katika eneo hilo agizo ambalo halikuwe za kukubaliwa, jambo
lililosababisha kutumika kwa mabomu ya kutoa machozi.
Tukio hilo la Polisi kutumia mabomu hayo lilianza
saa 7 mchana hadi saa 9.45, waliposimamisha kutumia mabomu ambayo
yalikuwa yakifyatuliwa kuwatawanya Machinga hao.
Wakati Polisi wakizunguka kuwatawanya, machinga
nao walikuwa wakiweka mawe na magurudumu ya magari barabarani
kuhakikisha magari ya askari hao hayapati nafasi ya kupita.
Mitaa ya kuzunguka eneo hilo ambalo mara nyingi
huwa na mkusanyiko wa watu, lilionekana kuwa wazi huku Polisi
wakilitawala kwa kuzunguka huku na kule kuhakikisha zoezi hilo
linafanikiwa.
Mwananchi Jumapili lilishuhudia gari la polisi
aina ya Land Rover likiwa limejaa wafanyabiashara hao waliokamatwa
wakati wa kuwaondoa eneo hilo, ambalo ni kandokando ya barabara
inayojengwa ya mabasi yaendayo kasi ya Strabag.
Baadhi ya wafanyabiashara wenye maduka, walijifungia ndani ya maduka yao kuepuka wizi ambao ungeweza kutokea.
Taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya mali ambazo
zimeharibiwa katika vurugu hizo ni pamoja na kuchomwa moto kwa jengo la
tawi la Klabu ya Yanga eneo la Manzese.
Baada ya barabara kufungwa kwa mawe na wamachinga
hao, hali hiyo ilisababisha foleni na usumbufu kwa wenye magari,
waliokuwa wakitoka Ubungo kwenda Karikaoo na wale waliokuwa wakitoka
Karikoo kwenda Ubungo iliwabidi kutumia njia za vichochoro kuepuka
vurugu hizo.
Wakati polisi wakifyatua mabomu hayo, baadhi ya
watu walikuwa wakikimbia ovyo huku watoto wakilia bila ya kupata msaada
wa kuwaondoa katika eneo hilo.
Baadhi ya watu walilazimika kupanda juu ya Daraja la Manzese ili
kukimbia mabomu ya Polisi yaliyokuwa yakilipuliwa mfululizo kuwatawanya
wafanyabiashara hao.
Askari hao walifyatua mabomu hayo katika
mikusanyiko yoyote, bila ya kujali hata wale waliokuwa katika sehemu za
baa na migahawa wakipata vinywaji na chakula.
Mfanyabiashara Steven Frank akizungumzia tukio
hilo alisema, Polisi wametumia nguvu za ziada kuwatawanya kitendo
ambacho kama wangetumia njia ya kistaarabu wangeweza kutekeleza agizo
hilo.
“Palikuwa hakuna sababu ya kufyatua mabomu yao
ovyo, kwani sisi hatukuwa tunawapiga wala nini lakini wao wanafyatua tu
bila mpango,” alisema Frank.
Mwananchi Jumapili alimsikia mmoja wa Polisi hao
akiwasilia na mwenzake kuwa kama wamemaliza mabomu kuna mengine yapo
ndani ya gari.
“Kuna katoni kama tatu hivi katika gari, hivyo
kama mtamaliza tutawasiliana ili tuweze kuwaongezea, lakini inatubidi
tufyatue tu kuwatawanya huku tukiimarisha ulinzi na usalama wa
wananchi,” alisikika Polisi aliyekuwa amevaa kiraia.
Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema hana taarifa
zozote.
Alimtaja Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,
Camilius Wambura kwamba ndiye anayeweza kuzungumzia suala hilo. Hata
hivyo Wambura alipotafutwa hakuweza kupatikana.
Mmoja wa wafanyabiashara wa eneo hilo, Bashir
Zacharia alisema tukio hilo limewasikitisha kwani hawana sehemu ya
kwenda ambayo watafanya biashara kwa wingi.
Via Mwananchi
0 comments:
Post a Comment