JWTZ yaonya 
KUTOKANA na kuzidi kushamiri kwa matukio ya uhalifu nchini, huku wahusika wakionekana kutumia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jeshi hilo limeonya na kupiga marufuku wanaovaa sare za majeshi na kutumia vifaa vyao.

Taarifa iliyosambazwa na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya JWTZ kwa vyombo vya habari jana, inaeleza kuwa hivi karibuni kumekithiri kwa vitendo vya uovu huku wahusika wakiwa wameonekana wamevaa sare na kutumia vifaa vya jeshi hilo.

“Hivi karibuni vichwa vya habari vimetawala sana kwenye vyombo mbalimbali vya habari sehemu mbalimbali hapa nchini, mara utasikia ‘Mwanajeshi feki mbaroni Tanga’ au ‘Aliyejifanya Afisa wa JWTZ akamatwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam’ na mengine mengi…

“Pia kumejitokeza kama fasheni kwa baadhi ya wasanii, hasa wanamuziki mbalimbali hususan wa muziki wa kufoka foka maarufu kwa jina la Bongo fleva, kurekodi video zao wakiwa wamevaa sare za jeshi kama vile suruali, viatu, fulana, kaptula, mabegi au kofia,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza.

“Ukirudi mitaani nako hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la wananchi, hasa vijana wanaovaa sare za jeshi, ukiwauliza wanakozitoa wanakwambia kuwa wamenunua mitumbani ama kwenye maduka ya nguo, ingawaje ukipita kwa wauza mitumba, nao utakuta wanauza nguo za jeshi ingawa hufanya biashara hiyo kwa kificho, kwani huziweka sare hizo kwa nyuma ama ndani kwenye maghala yao, kwa kuwa wanafahamu fika kuwa ni kinyume cha  sheria ya nchi, ingawa wapo baadhi yao ambao huziuza hadharani wakidai kuwa ni mitumba.”

Taarifa hiyo iliongeza kuwa inawezekana kwa namna moja ama nyingine, baadhi ya watumiaji wa sare hizo hawafahamu kuwa ni kinyume cha sheria ya nchi kukutwa nazo, ingawa kutokujua sheria bado sio utetezi mbele ya mahakama.

Katika kukabiliana na tatizo hili, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka wazi juu ya uhalali wa matumizi ya sare hizi.
“Mtu yeyote yule asiye na ruhusa ya kushona, kuuza au kuingiza nchini sare za jeshi,  atakuwa ametenda kosa, kwa hiyo atafikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“Katika uvaaji au uingizaji nguo, kama itatokea kwamba nguo hizo zinafanana kwa aina yoyote ile na zile za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, ikadhaniwa kuwa ni hizo, mtu huyo ana hatia na anastahili kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu sare za majeshi zilizopo,” ilifafanua taarifa hiyo na kuongeza:

“Msisitizo uliowekwa hapa katika vifungu vya sheria ni kwamba, sio lazima ukutwe na sare ambazo zinatumiwa na JWTZ hasha, hapa sheria inasema hata kama tu nguo hiyo itaelekea kufanana kwa namna yoyote ile na sare ya JWTZ ni kosa la kisheria kuitumia.

“Na iwapo atapatikana na moja ya makosa yaliyotajwa kuhusu sare, nguo, viatu, vitambaa, vifungo, beji, au vitu vingine vyovyote alivyokutwa navyo vinavyohusika na JWTZ, basi kwa kutumia sheria zilizopo vitu hivyo vitachukuliwa na serikali,” ilifafanua taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa mtu yeyote ambaye atampa au kusababisha mtu mwingine asiyehusika avae sare za JWTZ, atakuwa ametenda kosa na atafikishwa mahakamani na kuhumiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Pia msisitizo wa JWTZ ni kuhakikisha kuwa, sare hizo zinatumika kwa watu husika tu na hivyo wananchi wanatakiwa kushirikiana katika hilo.
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top