Wanasiasa wakuu waliokuwa wamezuiliwa
Wanasiasa wanne wakuu walioachiliwa na serikali ya
Sudan Kusini, wamepokonywa hati zao za usafiri walipokuwa wanajiandaa
kuondoka nchini humo kusafiri hadi mjini Nairobi Kenya.
Mke wa marehemu John Garanga, Rebecca Garang,
ambaye anashikilia cheo cha juu katika chama cha SPLM , ameambia
mwandishi wa BBC Robert Kiptoo kuwa serikali haikutoa sababu ya
kuwapokonya hati za usafiri wanasiasa hao.
Serikali ya Sudan Kusini
iliwaachilia wanasiasa hao waliokamatwa kwa madai ya kuhusika na njama
ya mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Salva Kiir Disemba mwaka jana.
Waziri wa sheria alisema kuwa serikali
ilifutilia mbali kesi dhidi ya wanasiasa hao wanne wakuu waliotuhumiwa
kupanga njama ya mapinduzi ambayo yamesababisha vurugu za wenyewe kwa
wenyewe nchini humo.
Wanne hao akiwemo aliyekuwa kiongozi wa chama
cha SPLM, walikanusha madai ya kuhusika na njama ya mapinduzi, na pia
wamekanusha uhusiano wowote na mapigano yanayoendelea nchini Sudan
Kusini.
Kuachiliwa kwao imekuwa moja ya matakwa makubwa
ya waasi wanaopambana na serikali na ambao wanadaiwa kuwaua mamia ya
watu katika mji wa Bentiu kwa misingi ya ukabila.
Takriban watu milioni moja wamelazimika kutoroka makwao tangu vita kuzuka Disemba mwaka jana.
Waziri wa sheria Paulino Wanawilla alisema kesi
hiyo imetupiliwa mbali kwa sababu ya kusaidia juhudi za amani na
mapatano katika nchi hiyo ambayo imetumbukia katika vita vya wenyewe kwa
wenyewe.
Wanne hao ni pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa
chama cha (SPLM) Pagan Amum, aliyekuwa waziri wa usalama Oyai Deng Ajak,
aliyekuwa waziri wa ulinzi Majak D'Agoot na aliyekuwa balozi wa nchi
hiyo nchini Marekani Ezekiel Lol Gatkuoth.
BBC
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment