Katibu Mkuu wa Bavicha, Deogratias Munishi, alitoa kauli hiyo katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, kwamba Rais Kikwete alinukuliwa
kuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na ule wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) vinavyotumika kupitishia dawa hizo.
Alisema Bavicha imefedheheshwa na kauli hiyo ya mkuu wa nchi, kwa
kuwa haina mashiko wala haisaidii katika kupambana na biashara hiyo
haramu.
“Bavicha inaona kauli hii ya Rais Kikwete ni dhihaka kwa vijana wa
taifa hili ambao ndio waathirika wakubwa wa dawa za kulevya kwani haina
dhamira pana ya kudhibiti uingizwaji wa dawa hizo.
“Ikumbukwe kuwa tangu rais atamke kuwa anayo orodha ya
wafanyabiashara wa dawa za kulevya hakuna hatua zozote alizochukua dhidi
ya watu hao, zaidi taifa limeendelea kuathirika na biashara hiyo
haramu.
“Bavicha inajiuliza kulikoni mkuu wa nchi anaayakumbatia majina ya
wanaoliangamiza taifa bila kuchukua hatua zozote? Je, anawaogopa? Ama ni
maswahiba zake kiasi cha kuona aibu kuwachukulia hatua?
Kutokana na hali hiyo, Bavicha inamkumbusha Rais Kikwete kwamba,
inachafua taswira yake kama kiongozi wa nchi pia kushusha hadhi ya Ikulu
kwa kuwa inaonekana ni kituo cha kuhifadhi wahalifu.
Alisisitiza kuwa Bavicha inamtaka Rais Kikwete kutambua kuwa maneno
bila matendo katika kupambana na dawa za kulevya nchini hakusaidii bali
kunaendelea kupalilia uharamia huu, hivyo imefika wakati wa kuwataja
hadharani wale wote anaowafahamu wanaojihusisha na biashara hii kisha
awachukulie hatua.
Juzi Rais Kikwete alinukuliwa akisema kwamba haridhishwi na kasi ya
kupambana na dawa za kulevya katika viwanja vya ndege hapa nchini.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment