Paroko wa Kanisa la Orthodox, Parokia za Nyamihuu Kalenga, Iringa,
Costantino Mbilinyi akizungunza na waandishi wa habari nyumbani kwake
katika Kijiji cha Nyamihuu jana kuhusu kushambuliwa kwake.
Padri wa Makanisa ya Orthodox katika Kijiji cha Nyamihuu, Kata
ya Nzihi, jimboni Kalenga Constantino Mbilinyi (36) amepigwa na
kujeruhiwa na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.
Baada ya kukutwa na mkasa huo, Padri Mbilinyi
alishikiliwa kwa muda katika Ofisi ya Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho,
Kumbusho Chengula, na baadaye alichukuliwa na askari ambao walimpeleka
Kituo cha Polisi Kati, mjini Iringa kwa mahojiano.
Kasisi huyo akizungumza na waandishi wa habari
jana alisema alipatwa na mkasa huo alipoambatana na viongozi wa Chadema
waliopiga kambi kwenye Kata ya Nzihi, ambao walikuwa wakielekea kwenye
mikutano ya kampeni za kumnadi mgombea ubunge kupitia chama hicho, Grace
Tendega.
Alisema viongozi hao walimwomba awasindikize
kwenda Kijiji cha Igangimali kwa ajili ya kumwona mtu aitwaye, Samti
Ngonjela ili wamkabidhi mabango Tendega.
“Waliniomba na mimi nikakubali kwa kuwa nilikuwa
na ratiba ya kwenda katika kijiji kile kumwona Bento Ngaila ambaye
tulitaka kuzungumza kuhusiana na mchakato wa shamba langu lililoko
katika kijiji kile,” alisema Mbilinyi na kuongeza:
“Tulipofika nilimtafuta Ngonjela kwa ajili ya
kuwaonyesha viongozi wa Chadema, lakini wakati huo vijana wengine wa
Chadema walianza kubandika mabango ya mgombea katika klabu ya pombe ya
Lazaro Nzigi, na ghafla lilitokea kundi la wanachama wa CCM na kuanza
kuwafukuza.”
Alisema vijana hao walimgeukia wakimshutumu kwamba
aliwapeleka watu wa Chadema katika eneo lile ambalo wao walikuwa na
mkutano wa ndani.
Mbilinyi alisema licha ya kujitetea, wafuasi hao
wa CCM walimkamata na kumwangusha na kumfunga mikono nyuma kwa kamba ya
katani. Wakati huo wafuasi wa Chadema walikuwa wameshaondoka.
“Walianza kunipiga na kunisukuma hali iliyonifanya
nianguke chini na kuumia mkononi na mgongoni. Nikiwa nimeanguka chini
na mikono yangu imefungwa kamba kwa nyuma mmoja wa vijana hao alichukua
pilipili na kuingiza kwenye mfuko wa shati langu kisha wakanichukua na
kunipeleka ofisi ya ofisa mtendaji iliyoko Nyamihuu,” alisema Mbilinyi.
Mbilinyi alisema makada hao wa CCM walimweleza
ofisa huyo kwamba alikwenda na wenzake kuwafanyia fujo na kwamba
aliwatukana na kuwatishia maisha. Alisema watu waliomfanyia unyama huo
anawafahamu.
Ofisa Mtendaji
Kaimu Ofisa Mtendaji, Chengula alithibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa alilazimika kumweka ndani kwa
kuhofia hali ya usalama.
“Ni kweli....nilipigiwa simu na kada wa CCM ninayemfahamu
akaniambia Padri huyo amepeleka wanachama wa Chadema kwenye eneo ambalo
wao walikwenda kuwatembelea wanachama wao na kwamba waliwatukana,”
alisema Chengula na kuongeza: “Ilipofika saa 12 jioni niliona kundi la
watu wakija ofisini huku wakiwa wamemtanguliza Mbilinyi ambaye alikuwa
amefungwa kamba mikononi.”
Alisema baada ya kupokea maelezo ya makada wa CCM
aliamuru Padri Mbilinyi afanyiwe upekuzi kisha alimweka ndani lakini
baadaye saa 5 usiku polisi wakiongozana na viongozi wa Chadema na CCM
walifika kisha kuondoka naye.
Chadema, CCM
Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo ya Ufundi, Benson Kigaila alisema alikwenda polisi kumwekea dhamana.
Aliwapongeza polisi kwa kufika haraka Kata ya Nyamihuu ambako ndiko alikokamatwa padri huyo na kupigwa.
Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Iringa, Delfina
Mtavilalo alisema: “Huyo padri ninamfahamu lakini taarifa kwamba
alipigwa na wafuasi wa CCM hazina ukweli wowote.”
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhan
Mungi hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo na simu yake ilikuwa
ikiita bila kupokelewa.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment