TAMKO LA WAJUMBE WA BUNGE LA KATIBA WA KUNDI LA “TANZANIA KWANZA”

23 Machi 2014

Sisi Wajumbe Wa Bunge Maalum la Katiba tunaotoka makundi mbalimbali na pia tunaoamini katika kauli mbiu isemayo “TANZANIA KWANZA”, tunapenda kutoa tamko rasmi la kuunga mkono hotuba aliyoitoa Mheshimiwa Rais alipokuwa akihutubia Bunge Maalum la Katiba Tarehe 20/03/2014 kama ifuatavyo:   

Kwanza, tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, kwa hotuba yake aliyoitoa wakati akizundua Bunge Maalum la Katiba tarehe 20 Machi 2014. Tunaamini Rais, kama Mkuu wa Nchi, alikuwa na haki na wajibu wa kutoa mwelekeo na maono yake kuhusu Rasimu ya Katiba na hatua hii tuliyonayo sasa ya kuipitia Rasimu kwenye Bunge la Katiba. Tunafarijika kwamba hotuba hiyo imepokelewa vizuri na Watanzania wengi kwenye kila kona ya nchi yetu na wengi wao wamekuwa wakitutumia ujumbe wakituhimiza kuizingatia hotuba hiyo katika kutimiza wajibu wetu.

Pili, tunamshukuru Rais kwa uchambuzi wake wa kina wa Rasimu na ushauri wake kwetu kuhusu haja ya kuweka taifa mbele, kushawishiana kwa hoja kuliko kulazimisha hoja na haja ya kutunga Katiba itakayoliimarisha taifa letu na kuendeleza umoja na ustawi wa Watanzania. Sisi wana TANZANIA KWANZA tutaendelea kushawishi kwa hoja na wala hatutalazimisha.

Tatu, tumeshangazwa na hamaki iliyoonyeshwa  na baadhi ya wajumbe wenzetu kuhusu hotuba ya Rais. Tunasikitishwa na kauli zao zenye mwelekeo wa kuhujumu mchakato wa kupata Katiba mpya.  Viongozi hawahawa wanaotoa kauli hizi walionekana wakishangilia hotuba ya Rais pale aliposema yale waliyokuwa wanakubaliana nayo. Iweje watishie vurugu na kususia kisa tu Rais kasema baadhi ya mambo wasiyokubaliana nayo. Ustahamilivu wa kidemokrasia, ustaarabu na hekima ya uongozi na utu uzima hautaki hivyo.Hotuba ya Rais imeweka wazi faida na hasara za mifumo yote ya Muungano wa Nchi yetu kwa hoja ili Watanzania wawe na fursa pana zaidi ya kutafakari na mwisho kuamua. Mheshimiwa Rais ametimiza kauli yake ya kushawishi kwa hoja na si kwa kulazimisha.

Nne, Hotuba ya Mheshimiwa Rais haikuvuruga wala kuingilia mchakato uliopo mbele yetu. Rais hakuingilia kanuni za Bunge maalum tulizozipitisha, Rais hakubadilisha Sheria ya mabadiliko ya Katiba, Rais hakupiga kura kwenye vifungu vya Katiba, Rais ameanza kwa kuipongeza Tume ya Mh. Jaji Warioba na kuipongeza kw uwasilishaji wake. Alichokifanya Mheshimiwa Rais kama kiongozi mkuu wa Nchi mwenye hekima na busara na uchungu wa Nchi yake na kutambua dhamana aliyopewa na Watanzania wote bila kujali makundi ameelezea faida na hasara za mifumo ya Serikali iliyowasilishwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa Tume. Rais katupa moyo na kutuhimiza tumalize kazi haraka na tuifanye kwa weledi huku tukiweka maslahi ya Taifa mbele. Hata pale alipotoa maoni na ushauri kuhusu baadhi ya vifungu bado Mh.Rais alisisitiza kwamba uamuzi wa mwisho ni wetu sisi Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Tano, dhana ya kuichambua na kuikosoa rasimu maana yake si kumdhalilisha Mwenyekiti wa Tume na Wajumbe wake. Msingi mzima wa kutolewa Rasimu hii ni kwamba Wananchi tuichambue, tuikosoe, tuirekebishe, tuiboreshe na hata ikibidi tuibadilishe na mwisho tutaipigia kura sote kwa pamoja. Rasimu haikuletwa kama Msahafu wala Biblia na ndiyo maana zimewekwa hatua mbili baada ya kazi ya tume kukamilika: BUNGE MAALUM LA KATIBA na KURA YA MAONI YA WANANCHI. Rais akiwa mkuu wa Nchi, naye ana nafasi yake katika mchakato wa Katiba. Sisi wana TANZANIA KWANZA, tunashukuru kwamba Mh. Rais alitutanabahisha kuhusu maeneo muhimu ya kuzingatia ambayo Tume haikuyaainisha kwa upana wake ikiwemo mipaka ya Nchi yetu. Tunawapongeza Wajumbe wa tume kwa kazi waliyoifanya na kuikamilisha. Kazi inayofuatia sasa ni uchambuzi wa Rasimu waliyoiwasilisha. Katika hatua hii ya sasa ya Bunge la Katiba, Rasimu hii inaweza ikakosolewa na hata inaweza kubadilishwa sana. Tunawasihi Wajumbe wa Tume waondokane na dhana kwamba kazi yao inapojadiliwa tofauti na mapendekezo yao siyo udhalilishaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Sita, Sisi Wajumbe wa Bunge Maalum, wana TANZANIA KWANZA ambao idadi yetu ni zaidi ya Wajumbe 400 na ambao orodha yetu tutaitoa hivi karibuni kwa wingi wetu na umoja wetu tunayo dhamira ya kutimiza wajibu wetu kwa mujibu wa Sheria na kwa kuzingatia matarajio ya Watanzania. Tunawasihi wale wenzetu ambao hawakuipenda hotuba ya Mheshimiwa Rais watulie, waondoe hamaki na sote tushirikiane kuifanya kazi hii, kama wapo ambao kitendo cha Rais kuja kuhutubia na kutoa uchambuzi wake kuhusu Rasimu, kinawafanya wasitake tena kushiriki katika mchakato huu, basi uamuzi wao huo waufanye kwa namna ambayo haitatukwaza  au kutuzuia sisi wengine tunaotaka kuendelea na shughuli hii ya mchakato wa Katiba. Tunawasihi viongozi wa Bunge Maalum wasivumilie wala kuendekeza vitendo vya vurugu za makusudi vitakavyozuia uendeshaji wa Bunge. Tunawasihi msiruhusu watu wachache wakaliweka rehani Bunge Maalum ili kutengeneza mtaji wa kisiasa. Tunawasihi Watanzania wawaone na kuwahukumu wale watakaotaka kuvuruga au kukwamisha mchakato adhimu wa kupata Katiba mpya kisa tu Mh. Rais kaja kuhutubia Bungeni.

Mwisho, tunapenda kusisitiza kuhusu umuhimu mkubwa wa vyombo vya habari katika mchakato huu. Hiki ni kipindi muhimu sana katika uhai wa Taifa letu. Wananchi wengi wanafuatilia mchakato huu kupitia vyombo vya habari.  Tunawasihi wamiliki, wahariri na waandishi wa habari wazingatie weledi wa hali ya juu sana katika kuripoti mchakato huu. Wananchi wanapenda kusikia, kuona na kusoma yanayojiri wala sio propaganda za wanasiasa au makundi mbalimbali. Tunapenda kuvisihi vyombo vya habari viwaunganishe Watanzania wote katika kipindi hiki muhimu na cha kihistoria. Hata hivyo tunatoa shukrani zetu za dhati kwa vyombo vya habari na wanahabari wote kwa ushiriki wao katika mchakato huu wa Katiba. Tunazidi kuwasihi waendelee kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa, kutokufanya kazi kwa kufuata propaganda za kisiasa au kufuata makundi, kutoa mizania sawa kwa maoni tofauti bila kuegemea maoni ya kundi moja au matakwa ya makundi fulani kwa kuwa mwisho wa siku sisi sote tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunakuwa na Tanzania moja.
Mungu Ibariki Tanzania

Mungu Libariki Bunge Maalum la Katiba

“TANZANIA KWANZA”

Tunawashukuru kwa kutusikiliza.

Kwa niaba ya Wabunge wa Bunge la Katiba “WANATANZANIA KWANZA”


.......................................................
Said Nkumba, (Mb  Waride Jabu, (Mb)
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top