Mjumbe wa Bunge maalumu la Katiba, Chritopher Ole Sendeka akichangia hoja
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, juzi na jana wamekuwa katika
mtihani mgumu wa kufikia uamuzi wa pamoja kuhusu utaratibu wa upigaji
kura, kati ya kura ya wazi na kura ya siri.
Habari kutoka katika kikao cha ndani cha Chama Cha
Mapinduzi (CCM), zilisema kutokana na mvutano huo, mjumbe mmoja,
Chritopher Ole Sendeka, alijikuta akilia hadharani akitetea upigaji kura
ya wazi.
Kikao hicho kilichofanyika juzi kati ya saa 2:00
na saa 5:30 usiku chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda,
kilishuhudia mabishano makali kati ya wanaotaka kura ya siri dhidi ya
wale wanaotaka kura ya wazi.
Habari hizo zilisema baada ya Pinda kufungua kikao
hicho, alimkaribisha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM, Shamsi
Vuai Nahodha, ili atoe mrejesho wa kikao cha mashauriano.
Inaelezwa kuwa katika kikao hicho, Nahodha
aliwaambia wajumbe kuwa kutokana na mazingira yaliyopo ndani na nje ya
Bunge kwa upande mmoja na wananchi kwa upande mwingine, kura ya siri
haiepukiki.
“Kilio cha Ole Sendeka kwenye party cocas kikao
cha chama (party cocus) juzi usiku kilitokana na kauli ya Nahodha kwamba
kura ya siri haiepukiki,” alidokeza mbunge mmoja wa CCM aliyehudhuria
kikao hicho cha faragha.
Mbunge huyo alilidokeza gazeti hili kuwa ndani ya
kikao kulikuwa na mabishano makali baada ya kauli ya Nahodha, huku
baadhi ya wabunge wakisema wananchi wamechoshwa na msimamo wa CCM.
Ni kutokana na mabishano hayo ndipo Ole Sendeka
aliposimama akipinga mapendekezo yaliyotaka CCM kulegeza msimamo na
kuridhia kura ya siri na wakati alipokuwa akizungumza alipobubujikwa na
machozi.
Huku akilia katika kikao hicho, inadaiwa Ole
Sendeka akisema kwamba kukubali kura ya siri ni kuitosa CCM na msimamo
wake wa kutaka muundo wa Serikali mbili.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa
Ole Sendeka alienda mbali zaidi na kusema endapo Pinda ataridhia kura
hiyo ya siri, basi yeye (Pinda) na viongozi waandamizi wa CCM
waliohudhuria watawajibishwa na CCM.
Kutokana na mtafaruku huo, kikao hicho kilishindwa
kufikia mwafaka na kuahirishwa hadi jana saa 5:00 asubuhi ambapo hoja
ya ama kura ya siri au ya wazi, iliendelea kuwagawa wabunge katika
makundi mawili.
Wakati akifungua kikao cha jana, Pinda alisema
kutokana na yaliyotokea katika kikao chao cha juzi usiku na baada ya
kutafakari kwa mapana yake, chama kimeamua kibakie na msimamo wake wa
kura ya wazi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Kutokana na yaliyojitokeza jana (juzi) na hasa ukiona mtu mzima
analia, tumetafakari tumeona tubaki na msimamo wa kura ya wazi,”
alisema mmoja wa wabunge akimkariri Waziri Mkuu Pinda.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, katika kikao hicho
ilielezwa kuwa kukubali upigaji kura wa siri ni kuiua CCM kwa sababu
wajumbe wengi wa Bunge Maalumu la Katiba, watapitisha muundo wa Serikali
tatu badala ya mbili.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba, wamehoji kitendo cha Mwenyekiti wa Muda wa Bunge
hilo, Pandu Ameir Kificho kuhudhuria kikao cha ndani cha wabunge wa CCM.
“Kificho ni mwenyekiti wa Bunge lenye makundi
tofauti, sasa anapoingia kwenye kikao cha wabunge wa CCM kinachoweka
mikakati ya kupingana na makundi mengine anatoa picha gani?” alihoji
mbunge mmoja.
Taarifa za Kificho kuhudhuria kikao hicho cha jana
cha CCM zilionekana kuwakera wajumbe wengine wa Bunge hilo, wanaotokana
na vyama vya upinzani na wale wanaotoka katika kundi la wajumbe 201.
“Bado tunatafakari tuchukue uamuzi gani, lakini
tukiona vipi, tutasusia kikao cha leo (jana) jioni, nyie njooni ndani
lolote linaweza kutokea,” alidokeza mjumbe huyo anayetoka katika kundi
la vyama vya hiari.
Kura ya siri, wazi yawekwa kiporo
Hata hivyo, jana mara baada ya Kificho kuanza
kikao cha semina saa 10:40 alasiri badala ya saa 9:00 alasiri alisema
semina hiyo imechelewa kuanza kwa sababu ya masuala muhimu.
Kificho aliwaambia wajumbe kuwa kamati ya
mashauriano ilikuwa imemshauri kanuni ya 37 na 38 zinazohusu kura ya
siri viwekwe kiporo kutokana na kutopatikana kwa mwafaka.
“Kamati imenishauri bado tuache kanuni ya 37 na 38
ili kamati ya mashauriano iendelee kunishauri vizuri zaidi ili baadaye
tuje tuwaambie kamati ya kanuni iziandike vipi,” alisema.
Kutokana na ombi hilo, wajumbe waliafiki waendelee kupitia kanuni ya 32 hadi 36 na 39 hadi 43 ambavyo havina mvutano.
UKAWA waweka msimamo
Katika hatua nyingine, wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambao
ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wameweka msimamo wa
pamoja wa kutaka kura ya siri.
Umoja huo unaojumuisha vyama vyote vya upinzani
ndani ya Bunge hilo, walikutana jana kuanzia saa 5:00 asubuhi hadi saa
8:30 mchana katika ukumbi wa Pius Msekwa.
Mkutano huo uliwajumuisha pia Mwenyekiti wa Taifa
wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman
Mbowe na wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba.
Mbowe alipoulizwa jana alisema msimamo wa umoja
huo bado umebakia kura ya siri, akisema utaratibu huo ndiyo mwafaka
utakaowawezesha wajumbe kupiga kura bila kuingiliwa.
Walioteuliwa na Rais wakwama
Kwa upande wa kundi la wajumbe 201 walioteuliwa na
Rais, juzi walikubaliana kila kundi liteue watu watatu wataokwenda
kukutana na kamati ya mashauriano ndipo waweke msimamo.
Taarifa zilizopatikana baadaye jana zilieleza kuwa
kundi hilo lilimchagua Dk Francis Michael kuwa mwenyekiti, halafu
makundi madogo madogo yatateua viongozi kuunda kamati ya utendaji.
Kamati hiyo ya viongozi ndiyo itakayokutana na
Kamati ya Mashauriano ili kuweza kukubaliana kuhusu kanuni za 37 na 38
zisomekeje.
Imeelezwa kuwa hadi semina ya wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba inaanza saa 10:40 alasiri walikuwa hawajakutana na
kamati ya mashauriano.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment