Hashim Rungwe akichangia jambo wakati wa moja ya vikao vya Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.
Mjadala wa namna ya kuamua Rasimu ya Katiba umezua hofu ya Bunge Maalumu la Katiba kuvunjika.
Bunge hilo limeangia siku ya 21 kati ya 70 likiwa
katika mjadala wa kupitisha kanuni, huku kukiwa na mabishano kuhusu
namna ya kupitisha ibara. Hadi sasa Bunge hilo limeshapitisha kanuni 85
za uendeshaji wa chombo hicho, isipokuwa mbili tu, ikiwamo ya upigaji wa
kura katika kupitisha vipengele mbalimbali katika rasimu, ambayo
inaonekana kusababisha mgawanyiko mkubwa.
Hali ya kutokubaliana katika masuala kadhaa
ilisababisha baadhi ya wajumbe kumtaka Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir
Kificho aeleze iwapo Bunge hilo lingeendelea au la kutokana na utata wa
kisheria na kikanuni kuhusu ibara na sura zitakazokataliwa na wajumbe
kwa kura.
Akichangia mjadala wa kanuni mjumbe, Dk. Francis
Michael aliitaka Kamati ya Mashauriano kuhusu vipengele vyenye ushindani
ikae chini na kutoa ufumbuzi kuhusu utata huo.
“Inabidi tuwe na uamuzi, hapa tunataka Katiba Mpya
au hapana. Hapa tunatumia fedha za walipa kodi. Kuna hoja ambazo
zinaonyesha kabisa kuwa zikifika hapa zitagonga ukuta,” alisisitiza.
Dk. Michael alipendekeza wanasheria na wakuu wa Serikali wa pande zote za Muungano kutafuta suluhisho mapema.
“Ni afadhali tuamue kabla hatujaendelea mbele kwa
sababu hakuna mantiki ya kuendelea kukaa hapa wakati tunajua kuna hoja
ambazo zinaweza zisifikie ufumbuzi,” alisisitiza Dk. Michael.
“Kwa hiyo mheshimiwa mwenyekiti kama kichwa
hakikupata solution (suluhisho) huko mbeleni sijui tunakwenda kujadili
vipi hii rasimu… hapa ni mahali pa kuangalia sana,” alisisitiza Hassan.
Naye Christopher Ole Sendeka alisema suala hilo la
kupitisha ibara kwa kuzingatia wingi wa theluthi mbili za kura
halihitaji ushabiki wowote ndani ya Bunge. Kanuni inataka iwapo ibara
haikupitishwa kwa theluthi mbili ya wajumbe, ipelekwe katika Kamati ya
Mashauriano ili kukarabatiwa na kurudishwa na baadaye kupigiwa kura kwa
mara ya pili.
Iwapo wajumbe watapiga kura kwa mara ya pili na
bado ikashindwa kupita, ibara hiyo itaondolewa kabisa. “Mnajadiliana
iwapo Tanzania ni Shirikisho ama Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
inapigwa kura mnakosa theluthi mbili Zanzibar na Tanzania Bara,
mtatakoje hapo?” Alihoji.
Kutokana na mkanganyiko huo, Sendeka alipendekeza
wanasheria waliobobea wakae na Serikali na kukubaliana ikitokea hali
hiyo, njia ipi itatumika kulinusuru Bunge lisivunjike. Pauline Gekul
alisema kanuni inayozungumzia wingi wa kura katika upitishaji wa ibara
imewaacha hewani kuhusu nini kitatokea kama ibara zitashindikana
kupitishwa.
Gekul alipendekeza kuwa badala ya ibara au sura ambayo haikupitishwa kuondolewa, alishauri suala hilo lipelekwe kwa wananchi kuamuliwa kwa wingi wa kura badala ya kuziondoa.
Gekul alipendekeza kuwa badala ya ibara au sura ambayo haikupitishwa kuondolewa, alishauri suala hilo lipelekwe kwa wananchi kuamuliwa kwa wingi wa kura badala ya kuziondoa.
Naye Ummy Mwalimu alipendekeza wakati wa kupitisha
ibara katika hatua ya kamati, suala hilo lipitishwe kwa kuzingatia
uwiano wa zaidi ya asilimia 50 kutoka pande zote za Muungano badala ya
theluthi mbili.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Bunge kubadili vifungu?
Mtaalamu aliyebobea katika masuala ya sheria, Dk.
Akson Tulia alisema Bunge hilo linayo mamlaka ya kisheria kubadili
muundo mzima wa Ibara na Sura za Rasimu ya Katiba.
Akijibu hoja mbalimbali za wajumbe katika Semina
ya Bunge hilo juzi, Dk. Tulia alisema Kamati ya Uongozi ndiyo yenye
mamlaka ya namna sura za Rasimu ya Katiba zitakavyogawanywa.
“Naomba niwakumbushe wajumbe kwamba tumepitisha
kanuni ya 32(1) inayotoa mamlaka ya namna sura zitakavyogawanywa na
katika hilo Kamati ya Uongozi ndiyo itakayoamua,” alisema.
Dk. Tulia alisema: “Kamati ya Uongozi itajua miguu ni ipi, kichwa ni kipi na waanzie wapi.”
Alisema kwa zile sura na ibara zitakazokataliwa
kwa kukosa wingi wa theluthi mbili ya kura kutoka Tanzania Bara na
Zanzibar, zitaondolewa kabisa kwenye rasimu.
Kauli ya Dk. Tulia, ambayo aliitoa wakati akijibu
hoja mbalimbali za wajumbe kwa niaba ya Kamati ya Kanuni, ilionekana
kuwakanganya zaidi wajumbe kuliko kuwapa mwanga.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment