
Mama Maria Nyerere akitoa heshima za mwisho mbele ya jeneza lenye mwili
wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa, wakati wa
shughuli za kuaga mwili huo zilizofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee
jijini Dar es Salaam jana. Mwili huo umesafirishwa kwenda mkoani Iringa
kwa maziko.
Wakati mwili wa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa ukitarajiwa
kuzikwa leo, Serikali imesema kilichosababisha kifo chake ni ugonjwa wa
figo.
Dk Mgimwa alifariki Januari Mosi, mwaka huu katika
Hospitali ya Kloof Medi Clinic, Pretoria nchini Afrika Kusini alikokuwa
amelazwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius
Likwelile uliutaja ugonjwa huo mbele ya waombolezaji waliofika kuuaga
mwili wake kwenye Viwanja vya Karimjee.
Likwelile alisema: “Marehemu Mgimwa alikwenda
Hospitali ya Kloof Medi Clinic, Afrika Kusini Novemba 3, mwaka 2013 kwa
ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake...baada ya uchunguzi,
madaktari walimshauri alazwe kwa uangalizi zaidi na matibabu na kwamba
aliendelea na matibabu ya figo hadi kifo chake.”
Aaagwa Dar
Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza mamia ya
waombolezaji waliofika kwenye viwanja vya Karimjee kutoa heshima za
mwisho kwa mwili wa marehemu Dk Mgimwa, pamoja na viongozi wengine
wakiwemo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Spika wa Bunge, Anne
Makinda, mawaziri, Mama Maria Nyerere na viongozi wengine wa vyama vya
siasa.
Kikwete ambaye alikuwa wa mwisho kutoa heshima
zake baada ya kuchelewa kufika kwenye viwanja hivyo akitokea Zanzibar,
mara baada ya kufika alitia saini kitabu cha maombolezo na kutoa heshima
za mwili kwa marehemu Mgimwa.
Kwa mujibu wa ratiba, leo Rais Kikwete pia
anatarajiwa kuongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Iringa kwenye mazishi ya
waziri huyo yanayotarajiwa kufanyika katika Kijiji cha Magunga.
Salamu za Mbowe
Akizungumza kwa niaba ya vyama vya upinzani,
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema Dk Mgimwa
alikuwa mwelewa, mnyenyekevu na mstarabu.
“Kwa muda niliomfahamu Dk Mgimwa akiwa kwenye
siasa, sikuwahi kumwona akikwaruzana wala kugombana, muda wote alikuwa
mstaarabu na msikivu kwa kila mtu,” alisema.
Mbowe alisema viongozi wa kisiasa wanatakiwa kuiga mfano wake kwa kuacha chuki na malumbano yasiyokuwa na tija.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Kauli ya Spika
Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema wamepoteza
mtu muhimu waliyekuwa wakimtegemea hasa katika mabadiliko ya muda wa
bajeti yaliyoanza mwaka 2013.
“Kama tungekuwa na uwezo wa kumrudisha duniani na
kumpeleka mtu mwingine tungefanya hivyo kwa sababu ya umuhimu wake,
lakini hatuna uwezo huo, tulimpenda, tulimuhitaji lakini Mungu amempenda
zaidi,” alisema Makinda.
Naye Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema Dk
Mgimwa alikuwa kiongozi asiye na mzaha kazini lakini hakuwa na makuu
wala hakujikweza.
Alisema Mgimwa alizingatia sheria, taratibu na
kanuni katika kushughulikia kero za Watanzania katika kujenga msingi
imara ya Bajeti ya Serikali.
“Katika kipindi cha takribani miaka miwili ambacho
tumekuwa chini ya uongozi wa Dk Mgimwa, tumejifunza mambo mengi ya
kifedha, kibajeti na kiuongozi ambayo tutaendelea kuyatumia,” alisema.
Naye Waziri wa Fedha wa Uganda, Jackson Kajala
alisema Sekta ya Uchumi na Fedha imepata pigo kubwa kutokana na kifo
hicho kutokana na mchango wake katika masuala ya forodha na sarafu moja
kwa nchi wanachama wa jumuiya.
“Tutamkosa, nilipata kukutana naye katika mikutano
mingi ya Jumuiya na nipo hapa kuwawakilisha Mawaziri wa Fedha wa Afrika
Mashariki na wote kwa ujumla wetu tumesikitishwa sana na kifo cha
Waziri Mgimwa,” alisema Kajela.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja
wa Mataifa (UNDP), Alberic Kacou alisema kuwa marehemu alitumia muda
wake mwingi na sehemu kubwa ya maisha yake katika fani yake ya uchumi na
fedha.
Alisema kuanzia NBC alikokuwa ameajiriwa wakati
fulani utumishi wake chuo cha benki hadi katika nafasi yake ya uwaziri
alikuwa kiungo muhimu baina ya wahisani, serikali na wafanyabiashara
wadogo.
“Alikuwa na mchango mkubwa sana katika masuala ya
uchumi kwani hata hoja za wahisani zilipata majibu ya msingi kuhusiana
na bajeti ya nchi, ninaamini kuwa waliobaki wataendeleza kile ambacho
marehemu alikuwa anaifanya,” alisema Kacou.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ambaye
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, alisema tofauti na
mawaziri wengine, Mgimwa alifanya kazi kwa zaidi ya saa 16 kwa siku
wakati wanapitia Sheria ya Fedha ambako walikaa katika kikao hadi saa
saba usiku.
“Nilikutana naye tena baadaye usiku huo na nilipomuuliza,
alinieleza kuwa alikuwa anamtaarifu Waziri Mkuu Mizengo Pinda
walipofikia katika kikao hicho,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema Mgimwa atakumbukwa kwa mengi kwani licha ya uchapakazi, alikuwa anasikiliza, anatafakari kisha anajibu.
Mwili wawasili Iringa
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana jioni aliupokea
mwili wa Dk Mgimwa baada ya kuwasili mkoani Iringa uliowasili saa 11:15
jioni tayari kupelekwa katika kijiji cha Magunga, Kata ya Maboga, Wilaya
ya Iringa Vijijini tayari kwa mazishi leo.
Mara baada ya kuwasili, mwili wa Dk Mgimwa
uliosindikizwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, Naibu Spika, Job Ndugai,
wabunge na viongozi wa dini ulipelekwa kwenye Ukumbi wa Siasa ni Kilimo
ambako Waziri Mkuu aliongoza maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Iringa na
vitongoji vyake kuuaga.
Huzuni, vilio na simanzi vilitanda ndani na nje ya
ukumbi huo, huku baadhi ya wapiga kura wake wakiwemo madiwani wakiangua
vilio na wengine wakiwa katika makundi wakitafakari.
Baadaye, Waziri Mkuu aliyetokea kijijini kwake
Kibaoni, wilayani Mpanda, Katavi alikokwenda kwa mapumziko ya mwisho ya
mwaka, alikwenda kijijini Magunga kukagua ujenzi wa kaburi atakalozikwa
Dk Mgimwa, uwekaji wa mahema pamoja na eneo la kufanyia ibada ya
mazishi.
Vilevile alikagua mahali ambapo mwili wa marehemu utalazwa ukisubiri taratibu za mazishi hapo leo.
Akiwa Kijiji cha Magunga kilichopo kilometa 66
kutoka Iringa mjini, Waziri Mkuu alifika nyumbani kwa Mama Mzazi wa Dk
Mgimwa, Consolata Semgovano na kumpa pole pamoja na ndugu, jamaa na
marafiki wa marehemu.
Hali ya Mji wa Iringa pia ilionekana kubadilika
huku kukiwa na misafara ya magari yaliyokuwa inakwenda kwenye kijiji
hicho ambacho mazishi hayo yatafanyika leo.
0 comments:
Post a Comment