Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman
Mahakama imeanza kutekeleza mpango kabambe wa kuondoa mrundikano
wa kesi na kwa mara ya kwanza katika historia ya mhimili huo nchini,
majaji na mahakimu wamewekewa malengo ya kesi wanazopaswa kusikiliza na
kuzitolea uamuzi.
Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema chini ya
mkakati huo, majaji wa kanda za Mahakama Kuu zenye mrundikano wa kesi
kwa muda mrefu, wametakiwa angalau kumaliza kesi 220 kwa mwaka.
Kadhalika kwa kesi mpya zinazofunguliwa, majaji
wametakiwa kujitahidi kumaliza kesi hizo ndani ya miezi 24, wakati
Mahakimu Wakazi na wale wa Wilaya wametakiwa kumaliza mashauri
yanayopangiwa kuyasikiliza ndani ya miezi 18.
Vyanzo huru ndani ya mhimili huo, vimeliambia
gazeti hili kuwa chini ya mkakati huo kabambe, mahakimu wa mahakama za
mwanzo kote nchini wametakiwa kumaliza kesi mpya ndani ya miezi 12.
Ili kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa, wadau
muhimu akiwamo Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, Jaji Kiongozi, Fakhi
Jundu na Majaji wa Mahakama ya Rufani walikutana Desemba 2013, Bagamoyo
Mkoa wa Pwani katika mkutano ulioweka mkakati wa utekelezaji wa uamuzi
huo.
Mkutano huo uliofanyika chini ya uenyekiti wa Jaji
Mkuu, Mohamed Chande Othman, pia uliwashirikisha wawakilishi kutoka
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkurugenzi wa Mashtaka
nchini (DPP), watendaji wakuu wa Mahakama hizo na viongozi wa Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS).
Katika kuanza utekelezaji wa mkakati huo, Msajili
wa Mahakama Kuu, Ignas Kitusi na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Pantrine
Kente walitembelea kanda mbalimbali kuhakiki wingi wa kesi zilizopo.
“Mheshimiwa Kitusi yeye alikwenda Kanda ya Moshi
na Kente alikwenda Kanda ya Arusha na hivi tunavyoongea (jana) Kente
anaelekea Kanda ya Moshi kuhakikisha mashauri ya rufaa,” ilidokezwa.
Gazeti hili lilipomtafuta Kitusi na kumuuliza
kuhusu mkakati huo unaohusisha majaji na mahakimu kuwekewa malengo kwa
ajili ya kupunguza mrundikano wa kesi alijibu kwa kifupi: “Ni kweli
hicho kitu kipo.”
Kwa upande wake, Kente alisema hawajapata maagizo
ya kesi ngapi zinatakiwa kumalizika ndani ya mwaka mmoja isipokuwa
mchakato wa kukabiliana na mrundikano wa kesi unaendelea na utapatiwa
ufumbuzi hivi karibuni.
Alisema kwa kuwa kesi za Mahakama ya Rufani lazima
zisikilizwe na majaji watatu wanaangalia uwezekano wa kuwawezesha ili
kukabiliana na tatizo hilo.
“Ndio tunajipanga namna Mahakama ya Rufani
itakavyoweza kumaliza kesi nyingi kwa haraka, hili lipo kiufundi zaidi
lakini tutalipatia ufumbuzi mapema iwezekanavyo,” alisema Kente.
Wakili apongeza
Mkakati huo umekuja wakati kukiwa na malalamiko ya
kuwapo mrundikano na ucheleweshaji wa kesi katika mahakama nyingi
nchini, huku nyingine zikiwa zimekaa zaidi ya miaka 10.
Wakili mashuhuri wa siku nyingi, Peter Shayo
alitaka mhimili huo uende mbali zaidi ili Jaji apimwe kwa idadi ya
mashauri anayoyasikiliza na kuyatolea uamuzi katika kipindi cha mwaka
mzima.
“Tunapaswa tuwe na kitu kinaitwa Performance
Contract by Judges (mkataba wa ufanisi kwa majaji) ili kigezo cha
kuongezewa muda wa mkataba iwe ni idadi ya kesi alizosikiliza na
kuziamua kwa mwaka,”alisema.
Wakili Shayo alisema utaratibu huo ndio unaotumika
nchini Kenya kupima ufanisi wa majaji na Uganda nayo iko njiani kuanza
kuutumia sambamba na nchi ya Zambia.
“Ingawa yako mazingira tofauti ambayo kesi inakuwa
haijacheleweshwa na Hakimu au Jaji, lakini wakijua kwamba ufanisi wao
utapimwa kwa njia hiyo itasaidia kuongeza ufanisi,”aliongeza Shayo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment