KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amekana na kusisitiza kuwa hajawahi kuwasiliana na Mwenyekiti wa chama hicho, Wilaya ya Temeke, Joseph Patrick ili kumshinikiza ajiuzulu uongozi.
Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alisema taarifa zinazotolewa na Patrick kuwa viongozi wakuu wa chama hicho walimlazimisha ajiuzulu nafasi yake, baada ya kubainika kumuunga mkono Zitto, ni za uongo zenye lengo la kupotosha ukweli wa mambo.

Alisema siku zote chama chake hakina utaratibu wa kufanya kazi moja kwa moja na wilaya kwa namna yoyote ile.

“Nimeshangazwa na uzushi na uongo unaosambazwa na Patrick, kwamba sisi viongozi wa juu tulimshinikiza ajiuzulu… napenda kuhakikisha kwamba katibu mkuu huwa hafanyi kazi na wilaya… hizi ni hila zilizopandikizwa tu,” alisema Dk. Slaa.

Alisema yeye kama mtendaji mkuu wa chama, hajawahi kufanya mawasiliano yoyote na kiongozi wa wilaya kuhusiana na jambo lolote.

Alisema kwa taratibu zilizopo, katibu mkuu huwasiliana na viongozi wa kanda au mkoa ambao ndio wenye mamlaka kikatiba kufanya mawasiliano ya kikazi na wilaya za chama.

Alisema hata kama kuna maagizo ambayo yanatakiwa kufika wilayani, anachoweza kufanya yeye ni kuagiza kanda au mkoa ambao wanaweza kushughulikia masuala ya ngazi za wilaya.

“Si kweli uongozi wa chama taifa uliwahi hata mara moja kumwelekeza kiongozi yeyote wa ngazi ya wilaya kufanya jambo au uamuzi wowote, mimi ni muumini wa Katiba nazijua taratibu.

“Taarifa zilizoandikwa katika vyombo vya habari zilipotosha ukweli, uongozi wa chama taifa hauna wajibu kikatiba kufanya mawasiliano ya kikazi moja kwa moja na wilaya, tunachoweza kukifanya ni kuwasiliana na kanda au mkoa ikibidi.

“Ni bahati mbaya huyo anayesema mimi katibu mkuu na mwenyekiti (Freeman Mbowe), tulimlazimisha aitishe vikao vya kujiuzulu, hasemi ilikuwa lini na wapi, anaishia kutoa shutuma tu zisizo na ushahidi, mwambieni awaonyeshe hizo barua na nyaraka zinazomtaka kujiuzulu, nadhani hizo ni hila zinatengenezwa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top