Clement Mabina enzi za uhai wake
MWENYEKITI wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina ameuawa na wananchi wenye hasira katika ugomvi wa mashamba. Mabina ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kisesa wilayani Magu mkoani hapa, aliuawa jana asubuhi katika eneo la Kijiji cha Kanyama wilayani Magu.

Mabina alishindwa katika uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza mwaka jana na waziri wa zamani ambaye pia alikuwa mbunge wa Ilemela, Dk. Antony Diallo.

Habari hizo zilipatikana mapema jana asubuhi na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Magu, Charles Mkapa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Desdery Kiswaga naye alipotafutwa alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.

Akizungumza na RAI Jumatatu jana, OCD Mkapa alikiri kutokea kwa tukio la kupigwa na kuuawa kwa Mabina, baada ya kutokea kutokuelewana baina yake na wananchi wa eneo la kijiji hicho.

Kwa mujibu wa Mkapa, Mabina alikwenda kupanda miti katika shamba lake lililopo katika kijiji hicho, ndipo mtafaruku ulipotokea baina yake na wanakijiji.

“Ni kweli mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Mwanza na diwani wa Kisesa amefariki dunia kwa kupigwa na wananchi.

“Awali ilisikika milio ya bunduki katika eneo hilo la Kanyama, nimemtuma mkuu wa upelelezi wa wilaya (OC-CID) kwenda katika eneo la tukio,” alisema OCD Mkapa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Desdery Kiswaga alisema kuwa amepokea taarifa za kuuawa kwa mabina aliyepigwa na wananchi wenye hasira kutokana na ugomvi wa mashamba na kueleza kuwa amesikitishwa na kuuawa kwa kiongozi huyo.

“Naelekea katika eneo la tukio hivi sasa, hakika inasikitisha ni kweli Mabina amefariki dunia baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira, baada ya kutokea kutokuelewana,” alisema Kiswaga.

Taarifa zaidi kutoka eneo la tukio zimeeleza kuwa, Mabina alifika katika eneo hilo asubuhi kwa ajili ya kupanda miti katika eneo la milima ya Kanyama linalodaiwa kuwa na mgogoro.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa wananchi nao walifika katika eneo hilo na kuhoji sababu za diwani huyo kupanda miti katika eneo hilo ambalo bado lina mgogoro wa umiliki na hivyo kutokea mabishano baina yake na wananchi.

Baada ya majibishano ya muda mrefu na kuona wananchi wameanza kumzingira Mabina, aliamua kufyatua risasi hewani kuwatawanya wananchi hao ambapo kwa bahati mbaya risasi moja ilimpiga mtoto aliyekuwa katika eneo hilo na kupoteza maisha.

Taarifa hizo toka katika eneo hilo la tukio zimeeleza kuwa kutokana na tukio hilo wananchi walimzingira Mabina na kuanza kumpiga kwa silaha mbalimbali za jadi kama vile mapanga, fimbo, mawe, mikuki na kusababisha kifo chake papo hapo.

Mabina aliwahi kuwa mwanachama wa NCCR-Mageuzi kabla ya kujiunga na CCM, ambapo mwaka 1995 aligombea ubunge katika jimbo la Magu, lakini alishindwa na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Malaki Lupondije.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top