NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, ametaja mawaziri watano wanaotaka kukwamisha mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya.

Zitto alisema mawaziri hao hawataki mabadiliko ndiyo maana wamekuwa wakikwamisha juhudi za Rais Jakaya Kikwete za uundwaji wa katiba mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Aliwataja mawaziri hao aliowaita ni wahafidhina, wasiopenda mabadiliko ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, William Lukuvi, Stephen Wassira, Mathias Chikawe na George Mkuchika.

Zitto alisema kama Rais Kikwete anataka kufanikiwa kwenye mchakato wa uundwaji wa katiba mpya ni vema akawafukuza kazi mawaziri hao kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo jana mkoani Tabora alipokuwa akihutubia mikutano ya hadhara na kufungua matawi ya CHADEMA wilayani Nzega.

Alisema viongozi hao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakimshauri Rais Kikwete vibaya, hususan katika suala la katiba, hali ambayo imewaweka njia panda wananchi.

Zitto alisema mawaziri hao hivi karibuni wakati wabunge wa vyama vya upinzani walipotoka bungeni kupinga baadhi ya vipengele katika mchakato wa muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013, walitoa kauli tofauti zenye madhara kwa jamii.

Alisema Pinda alishindwa kutumia nafasi yake kuishauri serikali hatua za kuchukua ili kuepusha mtafaruku.

Aliongeza kuwa wakati Lukuvi na Wassira walipotoa lugha ya maudhi kwa viongozi wa upinzani juu mustakabali wa Tanzania katika mchakato wa katiba mpya, rais aliwapuuza na kuamua kukutana na wenyeviti wa vyama vitatu vya upinzani.

“Kama mnakumbuka Lukuvi alilidanganya Bunge kuwa Wazanzibari walishirikishwa katika mchakato mzima, Wassira aliamua kutembea kifua mbele na kusema hakuna nafasi ya wapinzani kwenda Ikulu kujadiliana na rais.

“Chikawe aliamua kumtisha rais kwa kumweleza kuwa ataingia katika mgongano na Bunge. Hivi ni vitisho, na kwa bahati mbaya kwao, Kikwete amewashitukia sasa sijui kwanini hawatimui kazi.” alisema.

Alisema uamuzi wa Rais Kikwete kukubali kukutana na viongozi wa vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi huku akikubali kuwa kuna mambo yanayoweza kujadiliwa kwa utaratibu mzuri, ni uthibitisho kuwa washauri hao wa rais hawapaswi kuendelea kushikilia nafasi walizonazo.

Zitto alisema viongozi hao bado wanaamini suala la katiba ni mambo ya CCM, na kwamba Watanzania hawana nafasi ya kujadili au kuamua kupitia kwa wawakilishi wao.

Kuhusu waziri mkuu, Zitto alisema ameshindwa kuwaunganisha wabunge na shughuli za Bunge, hali aliyoeleza kuwa inaifanya serikali isemewe na wabunge.

Alisema wakati kesho ikiwa ni kumbukumbu ya miaka 14 tangu kufariki dunia kwa Mwalimu Nyerere, serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeamua kwa makusudi kuwasahau wakulima.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top