WAKATI watumishi wa umma wakitaabika na mishahara midogo, huku
wakipendekeza marupurupu ya wabunge yapunguzwe, wabunge wa CCM juzi
waliwaweka kitimoto viongozi wa Bunge wakitaka mishahara yao
ipandishwe.
Madai hayo yanakuja zikiwa ni siku chache tangu Spika wa Bunge, Anne
Makinda, naye kunukuliwa na vyombo vya habari akidai marupurupu ya
wabunge ni madogo hatua inayowafanya wengi wao kuishi maisha magumu
baada ya kupoteza ubunge.
Hata hivyo, kikao hicho kilikuwa na upinzani mkali baada ya wabunge wa
CHADEMA, John Mnyika na Tundu Lissu kupinga hoja za wabunge wa CCM
wakiwataka wawe na uchungu na wananchi.
Sakata hilo lilitokea juzi kwenye kikao cha wabunge na uongozi wa
Bunge cha kupeana utaratibu wa ratiba za shughuli za Bunge (briefing).
Baada ya wabunge kupata taarifa fupi ya ratiba walipata nafasi ya
kujadili mambo yanayowahusu, hususani huduma kwa wabunge.
Sintofahamu ilikuja pale wabunge wa CCM walipotoa hoja ya kuwataka
viongozi wa Bunge kuwaambia ni maslahi gani wanayapata kwa kuwachagua
wao hadi sasa.
Chanzo chetu kilidokeza kuwa mbunge mmoja kutoka mkoani Tabora (jina
tunalihifadhi) alihoji hilo na kuwataka viongozi wao kama wameshindwa
kazi basi wajiuzulu kwa hiari huku akisema wabunge wana maslahi madogo,
hivyo kuhitaji kuongezewa mishahara.
“Alitoa hoja ya kuahirisha kujadili hoja nyingine ili wajadili
mishahara yao ambayo alidai ni midogo na kutaka iongezwe mara moja kwa
kuwa wabunge wana hali ngumu sana,” kilisema chanzo hicho.
Baadaye alifuatia mbunge mwingine kutoka mkoani Dodoma ambaye alihoji
juu ya posho wanazopata na kusema mshahara ni mdogo, hivyo akapendekeza
malipo ya sh milioni 12 ili waweze kufikia viwango vya nchi nyingine
kama Kenya.
“Lakini mbunge mwenzake kutoka mkoani Mara (anamtaja) alitoa hoja ya
viongozi wa Bunge kukaa viti vya mbele ili wahojiwe na kama hawataki
wafukuzwe kazi mara moja na kuchagua makamishina wengine pamoja na
Spika na Naibu Spika,” kiliongeza.
Chanzo hicho kilisema kuwa wabunge hao walikuwa na umoja na kushikana
kupigania posho na mishahara mikubwa zaidi wakisema hawatosheki.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA),
nusra atibue mjadala huo baada ya kuwapinga watoa hoja na kupendekeza
posho za vikao zifutwe kama kweli wabunge wanaipenda nchi yao na
wananchi wao.
Inaelezwa kuwa wabunge walipinga hoja yake kwa kuguna na kunong’ona
wakiashiria kutounga mkono, hatua iliyomfanya mbunge mwenzake wa Singida
Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) kuingilia kati.
Lissu aliwaambia wabunge waache umbumbumbu wa kutosoma sheria ya
utumishi wa Bunge kwa kuanza kutaka kumtoa spika na naibu wake
madarakani, akisema wao sio sehemu ya uamuzi wa malipo kwa wabunge na
kwamba malipo yao yapo mikononi mwa rais.
Kikao hicho kiliahirishwa kwa mahitaji kufanyika kwa kikao kingine
rasmi kwa ajili ya kujadili maslahi ya wabunge, huku wabunge wakitaka
spika awepo na Waziri Mkuu ili waweze kuwahoji juu ya malipo yao.
Wadadisi wa masuala ya siasa wanaiona hali hiyo kama hatua ya wabunge
wengi kutokuwa na matumaini ya kurudi bungeni kwa kipindi kingine.
Kwamba wanashinikiza malipo makubwa ili fedha hizo ziwasaidie kwa
ajili ya maandalizi ya kuhakikisha wanakuwa na hazina pindi
wanapomaliza muda wao mwaka 2015.
0 comments:
Post a Comment