Sakata la vigogo kuficha mabilioni ya shilingi katika benki za Uswisi, limechukua sura mpya baada ya Serikali ya nchi hiyo kutunga sheria inayowabana walioweka fedha kwenye benki zake kuzithibitisha, la sivyo zitarejeshwa katika nchi husika. 

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alifanya mazungumzo na Serikali ya nchi hiyo ambayo imemweleza kuwa imebadili sheria zake ili kuwadhibiti wageni wanaoficha fedha nchini humo.
Akizungumza na gazeti hili, Zitto alisema amepata taarifa hizo juzi baada ya kukutana na Waziri wa Fedha wa nchi hiyo ambaye alimwandalia mazungumzo na watalaamu wake.
Alibainisha kuwa tangu kuibuka kwa sakata hilo mwaka 2012 na Bunge kuiagiza Serikali kufuatilia, Serikali haijaomba taarifa yeyote kutoka Uswisi kuhusu Watanzania waliohifadhi fedha nchini humo.
“Jana nilikutana na Waziri wa Fedha na akatuacha na mazungumzo na wataalamu wake. Wamesema hadi sasa, Tanzania haijasaini mkataba wa kubadilishana taarifa za kikodi (Multilateral convention on administrative assistance in tax matters),” alisema Zitto na kuongeza;
“Kwa kutosaini, Tanzania inajinyima haki ya kupata taarifa hizi na kutoza kodi kwa watu walioficha fedha huku (Uswisi), maana Sheria ya Kodi ya Tanzania inataka kila Mtanzania popote anapopata kipato halali lazima alipe kodi.”
Zitto alieleza kuwa kitendo cha Serikali ya Uswisi kubadili sheria zake, kinaiwezesha nchi hiyo kutoa taarifa za benki za watu walioweka fedha nchini humo wakiwamo Watanzania, ambao sasa watatakiwa kuthibitisha kama fedha hizo ni safi au la.
“Kiufupi, Tanzania haijaomba taarifa yeyote kutoka Uswisi. Ila Uswisi wamebadili sheria yao na sasa mmiliki wa fedha ndiyo anapaswa kuthibitisha kwamba ni safi, na ikithibitika kuwa hazina mwenyewe wala maelezo, zitarudishwa nchi husika,” alisema.
Zitto alisema mbali na kukutana na watendaji hao wa Serikali amezungumza na Umoja wa Mabenki wa nchi hiyo uliobainisha kuwa Uswisi ina Watanzania wachache wenye fedha.
“Wamesema Watanzania wengi wana fedha Uingereza, Jersey, Cayman Islands na Mauritius. Dubai pia imetajwa sana,” alisema Zitto. 

Zitto alielezea kuwa umoja huo wa benki za Uswisi umeanzisha mkakati wa kusafisha fedha uitwao ‘clean money strategy’, na wamegundua watu wengi ambao ni wanasiasa, wamezuia akaunti zao na kupeleka majina kwenye Serikali zao.
“Tanzania haijafanya maombi rasmi hapa Uswisi na hivyo wao kama benki hawawezi tu kutoa taarifa bila kuombwa. Sheria yao imerekebishwa ambapo sasa ni wajibu wa mwenye akaunti kusema kama fedha zake ni halali au hapana,” alisema Zitto na kuongeza.
Hivi sasa hawapokei pesa kutoka nchi za Afrika au wanapokea kwa tahadhari sana, maana kuna reputational risk (kupoteza heshima),” alisema.

Wito wa timu ya uchunguzi
Zitto alipendekeza timu iliyoundwa kuchunguza fedha hizo itoe taarifa yake kwenye Mkutano wa Bunge unaoanza Oktoba 29, mwaka huu, akieleza kuwa, “Kuendelea kukaa na taarifa, kutaongeza tetesi za kweli au za uwongo.”
Alisema mpango huo wa kusaka fedha zilizofichwa nchini Uswisi, umelenga zile zilizofichwa na watu binafsi kutokana na rushwa au kuuza dawa za kulevya na kampuni kubwa za kimataifa.
Alibainisha kuwa wengi waliotambulika ni wanasiasa, vigogo wa jeshi na wakuu wa mashirika ya umma na watendaji wa Serikali.
“Katika mabenki ya Uswisi, kuna kiasi cha Dola za Marekani 197 milioni. Fedha nyingi zipo katika benki za Uingereza na visiwa vyake, Dubai na Mauritius,” alisema na kuongeza;
“Wapo watu waliopata fedha kihalali, lakini wanaficha fedha hizo na mali zao nje ili kukwepa kodi. Wengi wa hao ni wafanyabiashara wakubwa nchini. Tanzania inapoteza Dola za Marekani 1.25 bilioni kati ya mwaka 2001 na 2012 kwa njia hizi.”
Alibainisha kuwa Tanzania lazima itunge sheria ya kufilisi mali ambazo mtu anashindwa kuthibitisha amezipataje.
“Tayari ninafanyia kazi muswada binafsi wa sheria wa kubadilisha sheria ya makosa ya jinai ya mwaka 1991. Wasaidizi wangu wanafanyia kazi muswada huo ili usomwe kwa mara ya kwanza kwenye mkutano wa Bunge unaonza Oktoba 29 na kueleza kuwa sheria ya sasa ina upungufu,” alisema.
Madai hayo ya Zitto yamekuja ikiwa umepita mwaka mmoja tangu Bunge kuipa Serikali muda wa kuchunguza sakata la vigogo walioficha mabilioni katika benki za Uswisi.
Zitto ndiye aliibua sakata hilo mwishoni mwa mwaka 2012. Kufuatia hoja hiyo, Serikali iliunda timu kutokana na Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka jana.
Werema ahoji Mwananchi ni Bunge?
Timu hiyo inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye jana baada ya kutafutwa na gazeti hili alisema, “Uchunguzi kuhusu walioficha fedha Uswisi bado haujakamilika.”
Viongozi wengine wanaounda tume hiyo ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu.
Alipoulizwa kama kuna uwezekano wa ripoti hiyo kuwekwa wazi katika Mkutano ujao wa Bunge, Werema alisema, “Kwa nini, kwani wewe ndiyo Bunge. Uchunguzi bado unaendelea”.
Hata hivyo, kwa mujibu wa agizo la Bunge, tume hiyo inatakiwa kuwa imekamilisha uchunguzi wake mwezi huu na kuwasilisha ripoti yake katika mkutano huo wa Bunge.
Alipoulizwa kuhusu ripoti hiyo, Naibu Spika, Job Ndugai alisema, “Wiki ijayo katika kikao cha Kamati ya Uongozi, Serikali itatakiwa kutoa taarifa za uchunguzi huo na kama haujakamilika kikao hicho kitaamua jambo la kufanya na endapo uchunguzi utakuwa umekamilika zitapangwa taratibu za kuiwasilisha ripoti bungeni.”
Waziri wa Fedha anena
Naye Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema jana kuwa sheria za kimataifa zipo wazi kwamba fedha chafu zinazogundulika kufichwa nchi fulani, hurejeshwa katika Serikali ya nchi husika.
“Lengo la sheria hizi za kimataifa ni kuhakikisha kuwa fedha za wizi zinazoibwa nchi fulani, haziwezi kuhifadhiwa katika nchi nyingine,” alisema.
Alipoulizwa kama wizara yake ina taarifa zozote kuhusu Watanzania walioficha fedha Uswisi alisema, “Kuna Tume iliundwa na Bunge kufuatilia suala hilo nadhani ndiyo itakuwa na majibu sahihi.”
Uchunguzi wa walioficha mabilioni ya Uswisi uliibuka baada ya Benki ya Taifa ya Uswiss (SNB) kutoa taarifa mapema Juni 2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki nchini humo.
Orodha hiyo inadaiwa kuwa na majina ya baadhi ya Watanzania wenye akaunti zinazofikia Dola 196 za Marekani milioni ambazo ni sawa na Sh323.4 bilioni.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top