KUFUNGIWA kwa magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa madai ya
“uchochezi” ni mwendelezo wa matumizi ya sheria mbovu ya magazeti
ambayo imekuwa ikitumika mara kwa mara kuzima au kuzuia mawazo na maoni
ambayo serikali inayaona kuwa hayafai.
Kwa vile sheria hii imeweka madaraka makubwa kwa waziri mwenye
dhamana ya vyombo vya habari, basi neno lake ni la mwisho na haihitaji
hata kufafanua uamuzi wake. Na baya zaidi ni kuwa uamuzi wake hauwezi
kuhojiwa na mahakama yoyote.
Wakati umefika kwa vyombo vya habari, wananchi na wadau wengine
kuanzisha vuguvugu litakalosababisha sheria hii ibadilishwe na hata
kufutwa ili yeyote mwenye dhamana ya vyombo vya habari asichukue uamuzi
bila kuangaliwa na chombo kingine (kama mahakama).
Katika demokrasia ni muhimu kuhakikisha uwepo wa mfumo wa kusimamiana
(checks and balances) ili kwamba mtu au chombo kimoja kisiwe na nguvu
za kiimla (dictatorial powers). Kama Waziri angetakiwa kwenda
mahakamani kufungua kesi dhidi ya magazeti haya – kesi ya uchochezi -
ni wazi kuwa mahakama ingetakiwa kuangalia ushahidi uliopo na uzito wa
ushahidi huo ukilinganishwa na haki za kikatiba zinazolinda vyombo vya
habari na watoa maoni.
Kwa msingi huo, japo ninatambua uwezo na mamlaka ya waziri kuchukua
uamuzi aliochukua, nasimama kupinga na kuulaani kwani unadumaza uhuru
wa maoni, unatisha vyombo vya habari na una lengo la kuwalazimisha
Watanzania kusoma na kusikiliza maoni yenye baraka za watawala tu na
hivyo kuwapa nguvu juu ya fikra na akili za wananchi.
Lakini zaidi napinga uamuzi huu kwa sababu unaifanya serikali iwe
mlezi wa akili za wananchi kana kwamba hawajui kupima habari.
Ikumbukwe hadi leo hii hakuna kesi hata moja au mtu hata mmoja ambaye
amewahi kushitakiwa na kukutwa na hatia ya kufanya jambo dhidi ya
serikali au viongozi ati kwa vile amesoma habari ikamchochea kufanya
jambo hili – maana ndio msingi wa hoja ya uchochezi! Napinga, nakataa
na ninakebehi madaraka haya ya waziri. Kimsingi huu uchochezi unaodaiwa
na serikali kufanywa na vyombo vya habari uko kwenye mawazo ya
serikali peke yake; hauko kwa raia!
Hakuna habari yoyote iliyowahi kuandikwa ambayo imeenda na
kusababisha watu kufanya vurugu na hata habari ambazo zingeweza kweli
kusababisha au zimesababisha matukio utaona kuwa vyombo vyake vya
habari havijawahi kufungwa; na wakati mwingine habari kama hizo
ziliandikwa kwenye magazeti ya serikali yenyewe!
Habari haiwi ya kichochezi kwa sababu tu imeandikwa kwa ukali au
kejeli; haiwi ya uchochezi kwa sababu watu fulani serikalini hawapendi
vichwa vya habari! Maana tukikubali hili itabidi wahariri waanze
kupeleka vichwa vya habari vya magazeti kwa msomaji wa vichwa vya
habari wa serikali ili avipitie na kuvikubali! Na itabidi wamtengee
fedha nyingi tu ya kutosha ili asitumie muda wake kufanya mambo yake
binafsi yasije magazeti kuandika habari za uchochezi bure!
Lakini zaidi ya hili hatari kubwa ambayo iko wazi ni kuwa kuelekea
2015 tutashuhudia mengi ambayo yatakuwa na lengo la kulinda mawazo ya
wananchi yasiwe hasi dhidi ya serikali yao na hasa dhidi ya chama
tawala. Hii ni kwa sababu kama magazeti yataandika habari ambazo
zitaonekana kuwafanya watu waichukie serikali – basi habari hizo
zitaitwa za kichochezi; yaani zinawachochea watu kuiangalia serikali
kwa mwanga mbaya! Na hili tumeliona maana hivi tunavyozungumza tayari
kuna kesi dhidi ya wahariri kadhaa kwa madai yale yale ya habari za
kichochezi. Na matokeo yake wahariri itabidi waanze kuimba nyimbo za
serikali.
Hapa inabidi kujiuliza hivi kama tukio lililotokea Nairobi lingetokea
Tanzania kweli vyombo vyetu vingeweza kuandika na kuripoti kwa uhuru?
Tumeshuhudia vyombo vya habari vya Kenya vikihoji na kuuliza maswali
mazito sana kuhusu operesheni ile, maswali ambayo yanaweza kuifanya
Serikali ya Kenyatta kuonekana isiyowajibika na kwa kweli upande
mwingine kuonekana haijajipanga vizuri kiulinzi na usalama.
Je, hoja hizi zikitolewa Tanzania juu ya vyombo vyetu vya usalama na
tukaonyesha udhaifu wake na tukafafanua matokeo ya udhaifu huu wa
vyombo hivi – ongezeko la dawa za kulevya, kuibuka kwa ujambazi,
utekaji n.k kweli kuna gazeti litabakia mitaani?
Baada ya kusema hayo ni muhimu kusema pia kuwa uhuru wa habari na
uhuru wa maoni unataka vyombo vya habari kuwajibika na kujiangalia
vyenyewe (self-censorship) ili kuhakikisha kuwa habari wanazoandika
zinaendana na ukweli na uhalisia, na hili ni muhimu hasa kwa magazeti
ambayo yanadai kuwa ni objective. Habari za kuvuta hisia (sensational
news) zinatakiwa zibakie kwenye vyombo vya habari vya namna hiyo
(tabloids). Kwa kadiri sheria hii bado ipo, wahariri na waandishi
wajipime wasiwape sababu watawala kuingilia vyombo vyao vya habari.
Lakini siyo kujipima tu, nimewahi kuandika huko nyuma kuwa vyombo vya
habari vyenyewe vimejiweka kwenye hali ya kuingiliwa na serikali
(compromised position). Baadhi ya vyombo vyetu vingi ambavyo vinaitwa
‘huru’ vinategemea mno fedha za serikali – kupitia matangazo mbalimbali
– kiasi kwamba inabidi kujikomba kwa watawala.
Tumeshuhudia vyombo hivi vingi havina sera na uwezo wa kujiendesha
vyenyewe bila kupokea kitu kidogo (bahasha) ili vitoe ripoti fulani.
Matokeo yake tumeona waandishi wanaenda kwenye mikutano ya habari
wanakuwa pale kama wao ndio kaseti; wanarekodi tu na kushindwa kuuliza
maswali ya akili, ya kubana na yenye kuonyesha uelewa.
Matokeo yake
kama tulivyoona habari ya Rais Kikwete kuagiza JWTZ kuingia kupambana
na ujangili, vyombo vya habari vilipewa habari iliyoandikwa na
mwandishi wa Ikulu na vyenyewe ama kuiweka jinsi ilivyo au kuibadili
maneno kidogo. Habari hiyo hiyo utaona imeandikwa kwenye magazeti yote
ikiwa imeandikwa na “Mwandishi Maalumu”.
Vyombo huru vya habari vinapofanya hivi vinakuwa vimejiuza; kwani
kabla ya kuandika habari vilitakiwa kuhakikisha maswali mbalimbali
yanajibiwa badala ya wao kuwa wasemaji wa serikali. Kama serikali ina
habari inataka iwafikie wananchi ni jukumu lake kuwapa waandishi uhuru
wa kuandika habari hiyo jinsi ilivyo na kutoa nafasi kwa vyombo vya
habari kuuliza maswali yanayoendana na tamko au habari iliyotumwa na
serikali.
Wahariri na waandishi kuendelea kukubali ‘posho’ za mikutano ya
serikali wakati tayari wanalipwa mishahara na vyombo vyao vya habari
wanajiweka katika mazingira mabaya zaidi ya kuingiliwa na vinapoteza
uhuru wake. Na hili linawapa watawala nguvu dhidi ya waandishi na hata
vyombo vya habari vyenyewe na mwisho watu wanaposoma habari fulani
utakuta haizami kwa undani wake au inaacha kwa makusudi maswali muhimu.
Yote haya yanaturudisha kwenye jambo moja kubwa; Tanzania inahitaji
sheria mpya vyombo vya habari (Media law) ambayo itafutilia mbali
sheria ya wakati wa Vita Baridi ya 1976. Kwa uongozi ambao unaonekana
kuchukia na kukebehi mambo yaliyofanywa na Mwalimu Julius Nyerere, basi
wangeonyesha kwa kufutilia mbali mojawapo ya sheria zake kali ya
magazeti na ile ya usalama wa taifa ya 1970.
Utasikia watu wanasema Mwalimu Nyerere alikuwa dikteta sijui aliminya
uhuru wa vyombo vya habari. Ukweli ni kuwa sheria zile zile alizotumia
Nyerere na wao wanazitumia! Angalau kwa upande wa Nyerere wengine
tunaelewa mazingira ya dunia na nchi yetu wakati ule, lakini hawa sasa
hivi hawana hata udhuru; wanahitaji sheria zinazoendana na mabadiliko
ya dunia na hali ya ulimwengu mamboleo. Kinyume chake wataendelea
kutumia hizi sheria za zamani ambazo hazitambui mabadiliko ya kisasa na
uelewa wa kisasa wa masuala ya haki za kiraia na za kibinadamu.
Kama tulivyowakatalia walipoingia madarakani tu 2006 pale aliyekuwa
Katibu Mkuu wa CCM alipowajia juu waandishi wa habari na kutishia
kuchukua hatua kali inabidi tuendelee kuwakatalia, lakini zaidi kwa
vile sera yao hii iko wazi kuwa wako kinyume na uhuru wa habari, basi
ni jukumu letu kuendelea kuunga mkono chama kingine cha siasa ambacho
kiko tayari kutuahidi kuwa kitafutilia mbali sheria hizi kandamizi ili
tuweze kukiingiza madarakani.
Wale ambao waliwarudisha hawa madarakani na kuwapigia debe; wasianze
kulalamika sasa kwani wanavuna walichopanda. Lakini kama sasa wameokoka
kisiasa basi wakati umefika waungane na wapigania mabadiliko nchini
kutaka watawala wetu waachane na sera hii ya kufungia magazeti; kama
wana hoja basi wajibu hoja kwa hoja na habari ya uongo kwa kuweka
ukweli.
Serikali isiogope kusahihisha habari au hata kuweka sawa habari
fulani. Hili ni jambo rahisi na inaonyesha serikali iko karibu na
wananchi badala ya mtu mmoja huko aliko kuamua kufungia gazeti kwa
sababu habari aliyosoma haikumpendeza au inakera na kuudhi.
Kuudhika si
sababu ya kufungia magazeti vinginevyo kila mtu ambaye anamuudhi
mwingine angekuwa anafungiwa kuzungumza kwa muda. Hii ni sehemu ya
maisha na serikali ianze kuonyesha kuwa inaweza kumudu maneno makali.
Ukitokea uhalifu kufanyika kwa sababu yoyote ile basi wahalifu
washughulikiwe badala ya kuhangaika na vyombo vya habari; na kama
chombo cha habari kinaunga mkono na kuhamasisha kufanyika uhalifu basi
hilo nalo lichukuliwe kwa uzito wake unaostahili.
0 comments:
Post a Comment