Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza kuwa majeshi
ya Kenya yataendelea kukaa Somalia hadi usalama utakapoimarishwa katika
nchi hiyo iliyokumbwa na vita vya miaka mingi.
Rais Kenyatta amesema kuwa nchi yake haitashurutishwa na magaidi walioteka jengo la maduka la Westgate kwa siku 4.
Rais
Kenyatta alihutubia umati uliokusanyika kwa maombi ya pamoja ya dini
mbali mbali, kwa ajili ya watu 67 waliouawa katika shambulio la
Westgate.
Shambulio hilo ndio baya zaidi kuwahi kutokea nchini Kenya tangu majeshi yake yaingie nchini Somalia mwaka wa 2011.
''Hawa wauaji waliokuja kutenda ukatili wao ulio
na woga hapa nchini kwetu, walikuwa wanadai kuwa wanafanya hivyo
kwasababu majeshi ya Kenya yapo nchini Somalia. Nataka niwaeleze bayana
kuwa, majeshi yetu yatakaa huko hadi kuwepo amani katika nchi hiyo.''
Mmoja wa makasisi walioongoza maombi hayo,
alisema,'' Baba tunakuomba utawale nchi hii. Na uwaoneshe maadui wote wa
taifa hili kuwa wewe unaipenda nchi hii na jina lako litatukuzwa.''
Wapiganaji hao wa Al Shabaab wamesema kuwa
walifanya shambulio hilo kulipiza kisasi kwa namna majeshi ya Kenya
yaliingia na kuwapiga nchini Simalia.
Rais Kenyatta pia ametangaza kuwa serikali
itaunda tume maalum kuchunguza upungufu mkubwa uliojitokeza kwa vyombo
vya usalama kufuatia shambulio la Westgate.
''Tutaunda pia tume maalum kuangalia ni wapi
tulikosea, ili tujirekebishe kuendelea mbele. Tuone ni wapi kumetokea
upungufu na ni vipi tutarekebisha.''
Ushirikiano
Aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga,
alikuwa miongoni mwa waliohudhuria maombi hayo. Bwana Odinga ametoa
wito kwa jamii ya kimataifa kuisaidia Kenya kukabili ugaidi.
Aliongeza kuwa ni makosa kwa mataifa ya
magharibi kutoa tahadhari kwa raia wao kutotembelea Kenya huku kwa
upande mwingine zikishinikiza Kenya kufayia mabadiliko idara zake za
usalama.
Bwana Odinga amesisitiza kuchukuliwa hatua za kuimarisha usalama nchini Kenya.
''Shambulio hili ni ishara kuwa tunaingia katika
makabiliano makali zaidi. Ni lazima tubadilishe mbinu zetu za kukusanya
intelijensia na uharaka wa kuchukua hatua. Ni lazima pia tuweke adhabu
kali kwa maafisa wanaolinda mipaka yetu ambao wanakubali mlungula na
kuruhusu maadui kuingia nchini na kutuumiza.''
Mwandishi wa BBC anasema kuwa wakenya
walivyojitokeza kwa wingi, walitaka kuonesha ishara ya utangamano wa
dini mbali mbali licha ya tofauti za imani.
Wiki moja baada ya shambulio la Westgate kumalizika, watu 39 wameripotiwa kutoweka.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment