Mahakama ya kimataifa ya ICC, imetoa kibali cha
kukamatwa kwa raia Mkenya ambaye anatuhumiwa kwa kujaribu kuwahonga
mashahidi ili wajiondoe kwenye kesi dhidi ya Naibu Rais wa Kenya William
Ruto.
Viongozi wa mashtaka walisema kuwa mshukiwa huyo
Walter Osapiri Barasa ameshtakiwa kwa makosa matatu ikiwemo kutumia
njia za ufisadi kumshawishi shahidi mmoja na mkewe kwa kumlipa shilingi
milioni 1.4 au dola 16,200, ili wajiondoe kama mashahidi katika kesi
hiyo.
Aidha mahakama inasema kuwa ni juu ya Kenya sasa kumkamata Barasa.
Kiongozi wa mashtaka Fatou Bensouda amesema kuwa
ana ushahidi wa kutosha kuonyesha njama ya Barasa kutaka kuwahonga
mashahidi ili wajiondoe katika kesi dhidi ya Ruto.
Bensouda amesema kuwa kuna mtandao wa watu wanaofanya kila wawezalo ili kuporomosha kesi dhidi ya Ruto.
Lakini Barasa ameambia BBC kuwa yuko tayari kujitetea mbele ya mahakama hiyo na kuonyesha kuwa hana hatia.
Naibu Rais Ruto na Rais Kenyatta wameshtakiwa
kwa kupanga na kuongoza ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo
watu 1,200 walifariki.
Muda kuongezwa
Mahakama ya kimataifa ya ICC italazimika kuwa na
vikao virefu zaidi vya kusikiliza kesi dhidi ya Naibu rais wa Kenya
William Ruto, kwa sababu ya muda uliopotea kutokana na Ruto kurejea
Kenya kwa dharura.
Jaji anayeongoza kesi hiyo Chile Eboe-Osuji pia
alisema kuwa mahakama itadurusu uwezekano wa kusikiliza kesi hiyo
Jumatano siku ambayo wangepumzika ili kuruhusu kesi nyengine kusikilizwa
ndani ya chumba hicho.
"kama tunavyojua sote tumepoteza muda katika
kesi hii kwa sababu ya matukio ambayo hayangeweza kuepukika. Lazima
tuweze kupata muda huo'', alisema jaji huyo.
Kesi dhidi ya Ruto iliahirishwa Septemba 23 kutokana na shambulizi la kigaidi nchini Kenya ambalo liliwau watu zaidi ya sitini.
Hata hivyo jaji huyo alisisitiza kuwa kesi hiyo
itaahirishwa kwa muda ili kutoa nafasi kwa kuanza kusikilizwa kwa kesi
dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta Novemba tarehe 12 ambaye ni mshitakiwa
mwenza wa William Ruto.
Kesi dhidi ya Ruto na mwenzake Joshua Sang,
iliahirishwa tarehe 23 Septemba, wakati mahakama ilipomruhusu Ruto
kurejea Nairobi kushughulikia shambulizi la kigaidi la Westgate na
athari zake.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment