Na Frank Geofray-Jeshi la Polisi.
Jeshi la Polisi Nchini limewataka
Wananchi kufunga kamera maalumu za kuwatambua wahalifu (CCTV) katika
maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu kama vile kwenye maduka makubwa,
benki na kwenye nyumba za ibada ili kuweza kuwatambua wahalifu kwa
urahisi pindi uhalifu unapojitokeza katika maeneo hayo.
Hayo yamesemwa na Msemaji wa Jeshi la
Polisi Nchini, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso wakati
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mikakati mbalimbali
iliyowekwa na Jeshi hilo katika kupambana na wahalifu na uhalifu
unaojitokeza hapa nchini.
Alisema hivi sasa Jeshi la Polisi
Nchini linaendelea na utaratibu wa kutoa elimu kwa wamiliki wa Maduka
makubwa, Benki na nyumba za ibada kufunga kamera hizo maalumu ambazo
hurahisisha kumtambua mhalifu na hatimaye kukamatwa na kufikishwa katika
vyombo vya sheria.
"Tunawashauri kufunga hizo kamera na
kufanya ukaguzi wa watu na magari yanayoingia katika maeneo yao ili
kuhakikisha hakuna mhalifu anayepata mwanya wa kutekeleza uhalifu katika
maeneo hayo muhimu ambayo kwa kiasi kikubwa yanakuwa na mkusanyiko
mkubwa wa watu na sisi kama Jeshi la Polisi tutatoa ushirikiano mara
moja pindi tutakapopata taarifa"Alisema Advera.
Aidha alisema hivi sasa wanaendelea na
mpango wa kuimarisha usalama kuanzia ngazi ya familia ambapo kila
Tarafa itakuwa na Askari 15 kulingana na hali halisi katika kata hizo
ambapo kwa ujumla kwa nchi nzima ni Askari takribani elfu nane.
Alisema majukumu ya Askari hao katika
Tarafa ni kuhakikisha kuwa uhalifu unapungua hasa kwa kushirikiana na
kamati za ulinzi na usalama katika maeneo husika pamoja na kutoa elimu
ya Ulinzi shirikishi ambapo kupitia mpango huo taarifa zz wahalifu
zitafika mapema na kufanyiwa kazi kabla uhalifu haujatokea.
Alibainisha kuwa mpango huo tayari
umeshaanza kutekelezwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini ambapo katika
jiji la Dar es Salaam tayari umeshazinduliwa katika mikoa mitatu ya
kipolisi ambayo ni Ilala, Temeke na Kinondoni.
0 comments:
Post a Comment