Muungano wa Afrika na Kenya zimelitaka baraza la
usalama la Umoja wa Mataifa kuakhirisha kesi dhidi ya Rais Kenyatta na
naibu wake William Ruto katika mahakama ya ICC, kwa mwaka mmoja ili
waweze kukabiliana na tisho la ugaidi linalokumba taifa hilo.
Hii ni baada ya Kenya kushambuliwa na magaidi
zaidi ya wiki tatu ziliopita na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 65 na
mamia ya wengine kujeruhiwa.
Kundi la kigaidi la Al Shabaab
lilikiri kushambulia jengo la maduka la Westgate kama hatua ya kulipiza
kisasi hatua ya majeshi ya Kenya kuwa nchini Somalia kupambana na kundi
la Al Shabaab.
Katika ujumbe wake kwa baraza la usalama la UN
na ambayo shirika la habari la Reuters liliuona, viongozi wa Muungano
huo wamesema kuwa kesi inayoendelea dhidi ya viongozi wa Kenya
itawatatiza na kuwazuia kutekeleza majukumu yao ya kikatiba.
Viongozi wa Kenya wanakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 na 2008.
ICC inadai kuwa waliongoza vita vya kikabila vilivyosababisha vifo vya watu 1,200 na kuwaacha maelfu bila makao.
Wote wamekanusha madai hayo na hata kuitaka mahakama kusitisha kesi hizo au kuziakhirisha.
Muungano wa Afrika hata hivyo uliwahi kuomba
mahakama ya ICC kuhamisha kesi hizo ili kuwapa muda wa kuimiarisha vita
dhidi tishio la ugaidi na usalama katika kanda nzima.
Wajumbe wa baraza la usalama la UN hata
hivyo,wamesema kuwa wanaweza wakatafakari ombi lolote la AU ingawa
walikataa ombi la Kenya la kuakhirishwa kesi hizo mwaka 2011 na kukataa
ombi lengine mwezi Mei la kutaka kesi hizo kusitishwa likisema kuwa
halina mamlaka ya kufanya hivyo.
Baraza la usalama hata hivyo linaweza
kuidhinisha kuakhirishwa kwa kesi hizo chini ya kifungu namba 16 cha mkataba
wa Roma uliounda mahakama hiyo miaka 10 iliyopita. Hata hivyo baraza
hilo litahitajika kupitisha azimio la kulipa mamlaka ya kuahirisha kesi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment