Naibu Rais wa Kenya, William Ruto
Naibu rais wa Kenya William Ruto, ameondoka kuelekea
Hague Uholanzi ambako anakabiliwa na kesi ya uhalifu dhidi ya binadamau
katika mahakama ya ICC ambapo kesi yake inatarajiwa kuanza siku ya Jumanne.
Maafisa wakuu wa serikali walimuaga Ruto katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi.
Bwana Ruto na rais Uhuru Kenyatta,
wameshtakiwa kwa kesi ya uhalifu dhidi ya binadamu, ingawa wanakana
kuhusika na mauaji yaliyotokea kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi wa
mwaka 2007-2008.
Mnamo siku ya Jumapili, Rais Kenyatta alisema
kuwa ICC lazima isikize kesi hizo kwa ratiba nzuri ambayo itawapa
viongozi hao muda wa kurejea nyumbani kwani wote hawawezi kuwa nje ya
nchi kwa wakati mmoja.
Kesi dhidi ya Kenyatta inatarajiwa kuanza kusikilizwa mwezi Novemba.
Mkuu wa kituo cha redio kilichodaiwa kuchochea
mapigano katika mojawapo ya maeneo yaliyokumbwa na mapigano, Joshua Arap
Sang , ameshtakiwa kwa kosa la kuchochea mapigano na kusaidia watu
kuyaandaa mapigano hayo ambapo naye amekanusha madai hayo.
Tuhuma dhidi ya wanaume hao watatu, yanatokana
na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007, ambapo zaidi ya watu 1,000
waliuawa na wengine laki sita kuachwa bila makao.
Kenyatta na Ruto walikuwa mahasimu wa kisiasa
wakati wa uchaguzi wa mwaka 2007 na wanatuhumiwa kwa kupanga na kusaidia
kutekeleza mapigano kati ya makabila hasimu.
Wadadisi wanasema kuwa kesi zao katika mahakama
ya ICC ziliwasaidia katika kampeini zao kwani walizitumia kukosoa
mataifa ya magharibi kwa kuingilia mambo ya ndani ya nchi hizo.
Mnamo siku ya Jumamosi, Kenyatta aliwakabidhi
hundi ya zaidi ya dola elfu nne familia za watu ambao walilazimika
kutoroka makwao kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu na ambao bado
walikuwa wanaishi katika kambi za wakimbizi.
Wiki jana bunge la Kenya lilipitisha hoja ya mjadala wa Kenya kujiondoa katika mahakama ya ICC.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment