SERIKALI imetangaza kuwapatia mafunzo ya miezi mitatu wanafunzi waliomaliza kidato cha sita waliokuwa wanasoma masomo ya sayansi kabla ya kujiunga na vyuo vya ualimu.

Akijibu swali bungeni jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, alisema wanafunzi hao ni wale ambao ufaulu wao hakukukidhi viwango vya kujiunga na vyuo vya ualimu.
Alisema serikali kupitia Wizara ya Elimu imeamua kufanya hivyo, ili kuhakikisha kunakuwepo na walimu wa Sayansi wa kutosha ili kuziba pengo lililopo.

“Natoa wito kwa wanafunzi wote waliomaliza kidato cha sita waliokuwa wanasoma michepuo ya sayansi hata kama walipata ‘S’ katika masomo yote, walete maombi yao Wizara ya Elimu mwezi huu,” alisema.

Alisema wizara itawapatia mafunzo ya miezi mitatu wanafunzi hao na baada ya hapo watakwenda kujiunga na wenzao ambao tayari wameanza mafunzo ya stashahada.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda (CCM), Mulugo alisema kipindi cha ukoloni elimu ilitolewa kwa ubaguzi.

Alisema katika kipindi hicho Wazungu walipendelewa kwa kupewa elimu bora zaidi wakifuatiwa na Waasia na wa mwisho walikuwa Waafrika.

Alisema maeneo ya nchi pia yalibaguliwa na kwamba Ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania ambao ulikuwa na vivutio vingi wakoloni walijenga shule nyingi kuliko Ukanda wa Kusini Magharibi ambao ulifanywa kuwa vyanzo vya vibarua.

“Baada ya uhuru serikali imechukua hatua mbalimbali za kuondoa tofauti za utoaji wa elimu kwa nchi nzima ukiwamo Mkoa wa Lindi.
Alisema baada ya serikali kutaifisha shule za watu binafsi na kuanza kuwachagua wanafunzi wanaojiunga na shule za sekondari, kila mkoa ulipewa mgawo wa nafasi za sekondari.

Mulugo alisema pia kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMES) na Mpango wa Maendelelo wa Elimu ya Sekondari (MMES II) inatoa upendeleo maalumu katika maeneo yaliyo nyuma kielimu ikiwamo mikoa ya Lindi, Mtwara, Shinyanga, Katavi, Kigoma, Rukwa, Tabora na Rukwa.

Katika swali lake, Mtanda alitaka kujua sababu za Mkoa wa Lindi kuwa nyuma kielimu na kuitaka serikali kuja na mpango wa dharura kuhusu mkoa huo
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top