HOJA ya kutengwa kwa Zanzibar katika rasimu ya Katiba, jana iliwalazimu wabunge wa vyama vitatu vya upinzani vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kususia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013.

Dalili za kambi hiyo kuupinga muswada huo zilianza kunukia tangu asubuhi baada ya kuwapo kwa fununu kuwa serikali kwa kushirikiana na wabunge wa CCM ilikuwa ikilazimisha muswada huo usomwe mara ya pili na kujadiliwa licha ya kasoro zilizomo.

Akibainisha kutengwa huko kwa Zanzibar katika mchakato huo, msemaji mkuu wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekwisha kutoa rasimu ya Katiba kwa mujibu wa kifungu cha 19(1)(d) cha Sheria.

Alisema rasimu hiyo imependekeza mabadiliko makubwa katika muundo wa Jamhuri ya Muungano kwa kupendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali tatu.

“Baada ya kukamilika kwa mchakato wa kutoa maoni juu ya rasimu hii kwa mujibu wa kifungu cha 18, Tume itawasilisha ripoti kwa Rais na kwa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 20(1).

“Baada ya hapo, Rais, “atachapisha rasimu ya Katiba katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine pamoja na maelezo kwamba rasimu ya Katiba itawasilishwa kwenye Bunge Maalumu kwa ajili ya kupitishwa Katiba inayopendekezwa,” alisema.

Lissu alisema ili kutimiza matakwa haya ya Sheria na kwa kuzingatia mapendekezo ya rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume, Bunge tukufu linahitaji kuangalia upya suala la uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalumu.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 22(2) cha Sheria, idadi ya wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalumu watakaotokana na makundi yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1)(c) “...haitapungua theluthi moja ya wajumbe hao.

“Hii ina maana kwamba, kwa uchache kabisa, wajumbe hao wa Zanzibar hawatapungua 55. Rasimu ya Katiba itakayojadiliwa na Bunge Maalumu inahusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano peke yake,” alisema.

Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, aliongeza kuwa rasimu hiyo imependekeza kwamba masuala yote yasiyo ya Muungano ya Washirika wa Muungano, yaani Tanzania Bara na Zanzibar, yashughulikiwe na Katiba za Washirika hao.

Kwa sasa wabunge wanaotoka Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ni 83, wakati Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina wajumbe 76. Kwa ujumla, kwa hiyo, ili kutekeleza matakwa ya kifungu cha 22(1) na (2) cha Sheria, Zanzibar itakuwa na wajumbe 219 katika Bunge Maalumu lenye wajumbe 604, sawa na takriban asilimia 36 ya wajumbe wote.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua: kama ilikuwa busara na sahihi kwa nusu ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Zanzibar, kwa nini isiwe busara na sahihi vile vile kwa nusu ya wajumbe wa Bunge Maalumu litakaloijadili na kuipitisha Katiba Mpya hiyo kutoka Zanzibar?” alihoji.

Baada ya Lissu kumaliza hotuba yake, wabunge kadhaa wa upinzani walisimama kuomba mwongozo wa Spika, ambapo wa kwanza kuzungumza alikuwa Habib Mnyaa wa Mkanyageni (CUF).

Mnyaa aliomba Naibu Spika, Job Ndugai, asitishe shughuli za Bunge ili muswada huo usijadilikwe akiunga mkono hoja ya Lissu kwamba Zanzibar haijashirikishwa katika mchakato huo pamoja na wadau wengine.

Hoja ya Mnyaa ilipanguliwa na Pindi Chana, wa Viti Maalumu (CCM), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, akisema kuwa Zanzibar ilishirikishwa na miongoni mwao alikuwamo Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

Hata hivyo, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) alipigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza akichambua baadhi ya vipengele kwenye muswada huo kuwa vimechomekwa bila wadau kushirikishwa.
Katika kutoa uamuzi wa kiti, Ndugai alikubaliana na hoja ya Mnyika lakini akasema uamuzi wake atautoa baada ya kushauriana na wasaidizi wake, jambo ambalo Lissu alilikataa na kuomba mwongozo.

“Muswada huu ukiachwa ujadiliwe unaweza kuligawa Bunge kwa vile Zanzibar hawajashirikishwa,” alisema Lissu lakini akakatizwa na Ndugai akitakiwa akae chini.

Baada ya hapo, Naibu Spika alimpa nafasi mchangiaji wa kwanza, Chana, ambaye hata hivyo wakati anaanza kujenga hoja wabunge wote wa CUF walisimama na kuanza kutoka nje wakifuatiwa na CHADEMA na NCCR-Mageuzi huku Augustine Mrema wa TLP akibaki na CCM.

“Wakati wabunge hao wakitoka nje, Ndugai alisema hiyo ni demokrasia lakini akawatisha kuwa: “Nawaona na mambo yangu mnayajua”.

Mapema Lissu katika maoni ya kambi ya upinzani aligusia kuwa wamepigia kelele jitihada za serikali ya CCM kudhibiti mchakato wa Katiba Mpya kwa kuendeleza kile tulichokiita miaka miwili iliyopita, “... kivuli kirefu cha urais wa kifalme katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.”

“Hapo tulikuwa tunazungumzia mamlaka ya Rais ya uteuzi wa wajumbe na watendaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na tulisema kwamba mamlaka hayo yalikuwa na lengo moja tu: “Kuhakikisha kwamba matokeo ya kazi ya tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na serikali yake na Chama chake cha CCM.

“Mapendekezo ya marekebisho yaliyoko kwenye muswada huu yanaonesha wazi kwamba ushauri wetu kwa Rais Kikwete na kwa timu yake ya watalaamu umepuuzwa.

“Badala yake, serikali hii sikivu ya CCM imeamua kuturudisha nyuma kwa zaidi ya miaka miwili kwa kuibua tena pendekezo la kumfanya rais kuwa mteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalumu wasiotokana na wabunge au wawakilishi wa Zanzibar,” alisema.

Lissu alisema kuwa hiii ni kwa sababu aya ya 3 ya muswada inapendekeza kwamba wajumbe hao sasa wateuliwe na rais. Hiyo ni sawa na kusema kwamba kilichokuwa hakifai miaka miwili iliyopita sasa kinafaa; na kilichokataliwa wakati ule sasa kinakubalika.

Ushahidi wa masilahi haya ya CCM ni kile kinachoitwa ‘Ufafanuzi Kuhusu Rasimu ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wanachama na Viongozi wa CCM’ uliotolewa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Juni 10, 2013.

Katika ufafanuzi huo, CCM imekataa mapendekezo yote muhimu yaliyoko kwenye rasimu ya Katiba iliyotolewa na tume. “Needless to say, Rais Kikwete ni Mwenyekiti wa vikao vyote vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.

“Kumpa Rais, na Mwenyekiti wa CCM Taifa mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu litakaloijadili – na kuikubali au kuikataa – Rasimu ya Katiba ambayo chama chake kimekwishaikataa ni sawa na kuipa CCM fursa nyingine ya kujaza Bunge hilo na makada wake kwa lengo la kutekeleza matakwa ya chama hicho,” alisema Lissu.

Hata hivyo, licha ya mjadala huo kuendelea wabunge wote wa CCM waliochangia walitumia muda mwingi kuwazungumzia wenzao waliotoka nje badala ya kujikita kwenye hoja.
Tanzania Daima 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top