Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imefuatilia taarifa
kwenye vyombo vya habari mbalimbali hapa nchini, kuhusu kushiriki kwa
Mheshimiwa Lu Younqing Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini
kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
uliofanyika huko Shinyanga, mwishoni mwa juma lililopita.
Taarifa hizo zimeambatana na picha zinazomuonyesha Mheshimiwa Lu akiwa
amevaa kofia yenye nembo ya CCM. Habari zinaeleza kuwa Balozi alikwenda
Shinyanga kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa viwanda vya kuchambulia pamba
vinavyojengwa na mwekezaji wa Kichina anayeitwa Tahong, na viwanda hivyo
vitakuwa na uwezo wa kuchambua tani 120,000 za pamba kwa mwaka,
vitakapokamilika mwakani.
Wizara inatambua mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Jamhuri ya watu wa
China na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vilevile inatambua kazi
nzuri ambayo Balozi Lu Younqing amekuwa akifanya toka alipowasili nchini
Tanzania. Kutokana na tukio hili, Wizara inapenda kuelekeza kwamba
kitendo cha Balozi yeyote kuhudhuria mikutano ya hadhara ya vyama vya
siasa na kuvaa sare zenye nembo ya vyama vya siasa sio sahihi na
kinakiuka Kifungu cha 41(1) cha Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961,
unaoongoza uhusiano wa kidiplomasia. Mkataba huo wa Vienna unazuia
wawakilishi wa nchi za nje kujihusisha na masuala ya ndani ya nchi
ikiwemo siasa wanapofanya kazi zao kwenye nchi za uwakilishi. Aidha,
Sheria ya Diplomasia ya Tanzania ya Mwaka 1986 ambayo ni zao la Mkataba
wa Vienna pia hairuhusu Balozi au mfanyakazi wa Ubalozi kujihusisha na
masuala ya ndani ya nchi.
Itakumbukwa kwamba, katika kipindi
cha mwaka 2010 hadi 2012 Wizara ilikumbana na vitendo vinavyofanana na
kitendo hiki na ikachukua hatua stahiki. Na kwa tukio hili pia Wizara
imechukua hatua za kidiplomasia zinazostahili ili kuzuia jambo hili
lisitokee tena.
IMETOLEWA NA: WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA 18 Septemba, 2013 Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment