ALIYEKUWA Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hayati Dk.
Daudi Balali ametajwa kuwa ndiye aliyeialika na kuiongezea mkataba wa
ukaguzi wa madini nchini Kampuni ya Alex Stewart.
Ushahidi huo ulitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Dar es Salaam na aliyekuwa Mkurugenzi wa Soko la Fedha wa BoT,
Crecencia Mbatia (61), ambaye anamtetea aliyekuwa Waziri wa Fedha,
Basil Mramba.
Mbatia ambaye alikuwa mwenyekiti wa timu ya watu watano ya
majadiliano ya jinsi ya kupata kampuni hiyo na wenzake, kisha kuandaa
mkataba kati ya BoT na Alex Stewart, alisema kuwa Dk. Balali ndiye
alitoa idhini na sio Mramba wala aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,
Daniel Yona.
Mramba, Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Gragy Mgonja
wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia
serikali hasara ya sh bilioni 11.7 kutokana na Kampuni ya Alex Sterwart
kupewa msamaha wa kodi bila ridhaa ya Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA).
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji John Utamwa, Sam Rumanyika na Hakimu Mkazi Saul Kinemela.
Mbatia alidai kuwa hivi sasa ni mstaafu, lakini mwaka 2002 akiwa na
wadhifa huo aliongoza timu hiyo ya majadiliano vizuri na kwamba
ilifanya kazi ya kumtafuta mkaguzi wa madini kupitia intaneti.
Aliongeza kuwa wakati wanatafuta kampuni hizo, walizipata 21, lakini
kamati yake ilichagua tano na serikali kupitia BoT ikaziandikia barua
zije kwenye majadiliano.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, kampuni mbili tu ndizo zilijibu barua ya
serikali ikiwemo Alex Stewart na baada ya mchakato, ikakubaliwa kuja
nchini kufanya kazi hiyo.
Mbatia ambaye alikuwa akiongozwa na wakili wa kujitegemea, Herbbet
Nyange kutoa ushahidi wake, alidai kuwa katika kipindi chote cha kamati
ya awali aliyokuwa akiiongoza hapakuwepo mwakilishi toka Wizara ya
Fedha.
Aliongeza kuwa alikuwa akiwaona wanasheria toka ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali ambao walikuwa wakishiriki katika vikao vya timu hiyo
ya majadiliano.
“Hata hivyo, timu yangu haikuweza kufanya majadiliano na Kampuni ya
Alex Stewart kwa sababu wakili wake alivyofika katika timu yangu
alisema haoni haja ya kufanya majadiliano kuhusu bei na gharama za
uendeshaji na timu hiyo, kwani tayari Gavana Balali kwa niaba ya BoT na
serikali nzima ilikuwa tayari imeishamtumia barua ya mwaliko
ikionyesha jinsi atakavyofanya kazi na gharama za uendeshaji,”
alieleza.
Mbatia alijibu maswali aliyokuwa akiulizwa na wakili wa Yona, Elisa
Msuya huku akisoma kielezo cha 11 ambacho ni barua ya BoT kwenda kwa
kampuni hiyo, ambayo Gavana Balali aliiandikia kuiarifu kuwa
imeiongezea tena mkataba wa miaka miwili.
Hata hivyo, upande wa jamhuri unaongozwa na wakili wa serikali,
Oswald Tibabyekomya na Shadrack Kimaro uliomba mahakama iahirishe kwa
muda kesi hiyo ili waweze kwenda kujiandaa na maswali ya kumuuliza
shahidi huyo.
Jaji Utamwa aliahirisha kesi hiyo hadi leo shahidi huyo atakapokuja kuhojiwa na upande wa jamhuri.
Novemba 2008 ilidaiwa mahakamani hapo na mawakili wa upande wa
jamhuri kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa ya matumuzi mabaya
ya madaraka na kuisasababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7.
0 comments:
Post a Comment