MATUKIO ya kushambuliwa kwa viongozi wa dini visiwani Zanzibar yameanza kujirudia tena baada ya Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju visiwani humo, Anselm Mwang’amba, kumwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana na kumsababishia majeraha makubwa katika sehemu zake za mwili.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai visiwani humo, Yusuph Ilembo, alisema kuwa kiongozi huyo wa kiroho alikuwa katika duka la huduma ya mitandao ‘Internet Café’ inayojulikana kwa jina la Mlandege Sun shine.

Alieleza kuwa alipigiwa simu na hivyo kumfanya atoke nje kwa ajili ya kupokea lakini ghafla alitokea mtu mmoja asiyemfahamu na kummwagia tindikali iliyomsababishia majeraha.

Ilembo alisema baada ya padri kumwagiwa tindikali alikimbilia ndani ya chumba cha mtandao kuomba msaada na ndipo mhudumu wa hapo alipowasiliana na watu wengine kuomba msaada wa kumpeleka Hospitali ya Mnazi mmoja kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Aliongeza kuwa padri Mwang’amba alipata majeraha katika sehemu zake za mwili ikiwa ni pamoja na mikononi, kifuani, tumboni na usoni.

Hata hivyo, alisema kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo kwa kuwa aliyefanya tukio hilo alikimbia na kwamba uchunguzi bado unaendelea ili kumpata mhusika.

Akizungumza na Tanzania Daima, ndugu wa karibu wa padri huyo, Simon Lisiel, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Parokia ya Mtakatifu Michael Mpendae mjini humo, alisema hali ya mgonjwa si nzuri na kwamba anaendelea na matibabu.

Alisema kuwa padri huyo ni kawaida yake kila siku kwenda katika eneo hilo la mtandao kwa ajili ya kuangalia taarifa zake na ndipo alipomwagiwa tindikali majira ya saa kumi jioni.

Hili ni tukio la tano kutokea visiwani Zanzibar ambapo Septemba 13 mwaka huu, Sheha wa Shehia ya Tomondo, Wilaya ya Magharibi Unguja, Mohammed Omar Said (65), alimwagiwa tindikali na mtu asiyejulikana wakati alipokuwa akichota maji nje ya nyumba yake.

Desemba mwaka jana, padri Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki Zanzibar alipigwa risasi na Februari 17 mwaka huu, padri Evarist Mushi wa kanisa hilo aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akienda kuongoza ibada ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Teresia.

Novemba 5, 2012, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, naye alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazoezi katika kiwanja cha Mwanakwerekwe.

Agosti 7 mwaka huu raia wawili wa Uingereza walimwagiwa tindikali kwenye eneo la Mji Mkongwe visiwani Zanzibar "Stone Town".

Wasichana hao wawili wa miaka 18 walikuwa walimu wa kujitolea katika shule moja ya Kanisa la Anglikana visiwani humo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top