Tundu Lissu
BAADA ya Mahakama ya Rufaa kuafiki ombi la wakili Godfrey Wasonga la
kuondoa kesi ya kupinga ubunge wa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu
Lissu (CHADEMA), mbunge huyo ametangaza kusudio la kuwashtaki Katibu
Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na mtangulizi wake Yusuph Makamba.
Katika kesi hiyo ambayo atamuunganisha pia wakili wa CCM, Wasonga na
bodi ya wadhamini ya chama hicho, Lissu anadai kuwa viongozi hao ndio
walishinikiza afunguliwe kesi ya kupinga ubunge wake.
Katika Mahakama ya Rufani jana, jopo la majaji watatu, Salumu Massati,
Engela Kileo na Natalia Kimaro, liliridhia ombi la wakili Wasonga
kuondoa kesi hiyo mahakamani kwa sababu waliokuwa walalamikaji,
Shaban Selema na Paskali Hallu, walijitoa wote wakisema hawana nia ya
kuendelea na kesi hiyo.
Awali kulikuwa na ubishani mkubwa wa kisheria kuhusu uhalali wa kesi
hiyo kuondolewa mahakamani, ambapo mlalamikiwa namba moja, Tundu Lissu,
alisema kuwa maombi hayo ya kuiondoa yalikuwa yameletwa kwa nia mbaya
ili kuifanya mahakama isitende haki.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wakili wa serikali, Vincent Tango, na
kuongeza kuwa hata ombi hilo lilikuwa limewasilishwa kinyume cha sheria.
Akisoma uamuzi wa mahakama, Jaji Kileo alisema baada ya kuangalia
mazingira ya kesi yenyewe na kwa namna walalamikaji walivyojitoa,
mahakama haikuona sababu ya kumwambia wakili Wasonga alipe gharama kama
Lissu alivyoomba.
Badala yake mahakama iliamuru mlalamikaji wa pili katika kesi hiyo
aliyechelewa kujitoa mpaka kesi ikapangwa kusikilizwa, ndiye alipe
gharama za kesi hiyo, huku gharama za kesi katika mahakama kuu wazilipe
na waliokuwa walalamikaji wote wawili.
Akizungumza na gazeti hili baada ya uamuzi huo, Lissu alisema sasa
anawashtaki viongozi wa CCM kwa kushinikiza afunguliwe kesi bure.
“Ninao ushahidi wa maandishi jinsi Makamba na Kinana walivyokuwa
wanashinikiza na kusaidia kulipa fedha ili mimi nifunguliwe kesi,”
alisema.
Lissu alisema atamshtaki Makamba kwa kuwa aliagiza yeye (Lissu) ashtakiwe wakati
Kinana alikuwa anashinikiza rufaa ikatwe licha ya walalamikaji wote
kujitoa tangu awali.
Hata hivyo Lissu alisema rufaa hiyo haikupaswa kukatwa, kwani Aprili
27, 2012, ndio hukumu ilitolewa Singida na Jaji Moses Mzuna ambapo kwa
taratibu za kisheria walipaswa kutoa taarifa ya kukata rufaa ndani ya
siku 30 na kuwapatia walalamikiwa taarifa hiyo.
“Hadi rufaa inatajwa na hukumu kutolewa sijawahi kupatiwa notisi hizo
za rufaa wala nakala ya hukumu, na mwenendo wa kesi kama waliamua
kutokutoa taarifa walipaswa kukata rufaa ndani ya siku 60, lakini rufaa
tunayosikiliza leo imekatwa Mei 20, 2013.
“Kisheria rufaa hii haikupaswa hata kupokelewa na mahakama na kama
walifungua kwa kuchelewa kisheria barua yao ya maombi ilipaswa kusainiwa
na Msajili wa Mahakama ili kueleza sababu za kuchelewa,” alisema.
Aliongeza kuwa alishangaa kwani licha ya kasoro hizo, hicho
kinachoitwa hati ya msajili alichopewa hakina jina la msajili wala
sahihi na muhuri wa mahakama ingawa rufaa imepangiwa tarehe na
imesikilizwa.
Lissu alisema kuwa kesi yake kukatiwa rufaa mwaka huu ni baada ya
hotuba ya upinzani kumtaja Kinana kuwa kinara wa biashara ya pembe za
ndovu.
“Ndipo Kinana alianza mpango wa kuwasiliana na wakili Wasonga
kumshauri akate rufaa na kuahidi kuwalipa majaji kila mmoja sh milioni
300 ili ubunge wangu utenguliwe,” alisema.
Tanzania Daima lilipata barua ya tarehe 20/05/2013, yenye
kumb.No/KM/CCM/01/2013 kutoka kwa Wasonga kwenda kwa Katibu Mkuu wa CCM.
“Mheshimiwa Katibu Mkuu maandalizi ya rufaa Mahakama Kuu yanahitaji
gharama kubwa sana, hii ni kutokana na umakini unaohitajika na pia
kuwalipa watu wa kufanya kazi husika, hivyo naambatanisha invoice ya
malipo ya awali ya sh 2,000,000 fedha za maandalizi ya awali ya sababu
za rufaa pamoja na vitabu husika.
“Ikumbukwe kuwa katika shauri la mwanzo nilikuwa nalipwa na CCM mkoa
wa Singida na hawakumaliza malipo, CCM Daima kurudi nyuma mwiko,”
ilisomea barua hiyo.
Barua hiyo ya Wasonga kwenda kwa Kinana iliambatanishwa na invoice
namba 076, yenye TIN 109-920-649 ili Kinana alipe malipo hayo ya rufaa.
Kwa mujibu wa Lissu bila Makamba na Kinana, asingefunguliwa kesi hizo za bure.
“Sasa nitawashtaki na wakili wao pamoja na bodi ya wadhamini wa CCM,
na watanilipa ili nipate fedha za maandalizi ya uchaguzi wa serikali za
mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2015,” alitamba.
Baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2010, CCM kupitia kwa Makamba, iliandika
barua yenye kumb. Na. CCM/OND/636/VOL.11/122 ya Novemba 9, 2010 kwenda
kwa makatibu wake wa mikoa na wilaya kuwaamuru wote walioshindwa katika
uchaguzi wapinge matokeo na kwamba chama kingewasaidia gharama za
uendeshaji wa kesi hizo.
Katika barua hiyo, Makamba aliwataka wagombea wa ubunge kufungua kesi
katika Mahakama Kuu ya Tanzania, huku wagombea udiwani walioangushwa
kufungua kesi katika mahakama za hakimu mkazi ndani ya siku 30, tangu
ulipofanyika uchaguzi huo.
Sugu amponza ofisa
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Upelelezi wa Dodoma mjini, Jumanne
Amasi, ameingia matatani na kulazimishwa kuhamia Iramba ili yule wa
Kiomboi aende Dodoma kuisaidia CCM kukabiliana na wapinzani.
Taarifa kutoka chanzo chetu zimethibitisha kuwa mkuu huyo wa upelelezi
amehamishwa kwa dharura kwenda Iramba kutokana na shinikizo la kigogo
mmoja wa CCM.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa ni kutokana na mkuu huyo kukataa maelekezo ya
kigogo huyo yaliyomtaka amweke mahabusu mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi (CHADEMA), baada ya fujo zilizotokea bungeni.
Inadaiwa kuwa awali mkuu huyo pia alikataa kumkatamata Mbilinyi maarufu
kama Sugu alipokuwa Desert Hotel ya mjini Dodoma, akitoa sababu kwa
wakuu wake kwamba kosa la mbunge huyo lilitendekea bungeni na alipaswa
kuwajibishwa kwa kanuni za Bunge.
Alipotafutwa msemaji wa polisi kwa simu kufafanua madai hayo, simu yake iliita bila kupokelewa.
Chanzo chetu kimethibitishiwa na Mkuu wa Upelelezi wa Iramba kuwa
tayari amepokea taarifa za kuhamia Dodoma kikazi lakini akadai ni
masuala ya kawaida.
Naye mkuu wa upelelezi wa Dodoma, hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo
kwani alidai kuwa hana taarifa na kwamba kama atahamishiwa Iramba
atachukulia kama sehemu ya kazi.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment