Siyo kundi la Sungusungu, Polisi Jamii au askari wa makundi ya
kiharakati au kisiasa unaoweza kufahamu. Hakuna ofisi wala vikao
wanavyokaa kusikiliza mashtaka kabla ya uamuzi, mbaya zaidi hakuna
anayejitambulisha kama mfuasi wa baraza hilo, lakini linatoa hukumu na
kutekeleza mauaji ya kutisha.
Taarifa zinaonyesha kuwa kwa mwaka jana pekee,
wastani wa watu watatu walikuwa wakiuawa kila wiki na kikundi hicho cha
watu kinachofahamika kama Baraza la Kimila katika Mkoa wa Simiyu,
wakiwamo wanawake na watoto.
Wanachama wa kikundi hicho maarufu Dagashida,
hufahamiana muda wa kupokezana ‘Mbiu’inaposikika kama ishara ya
kuhudhuria tukio la utoaji wa hukumu.
Unaweza kulinganisha na Kundi la Al-Shabaab, kwani
baraza hilo hufanya maasi na kusambaa msituni kwa muda wa siku
zisizopungua tano wakihofia kutiwa mbaroni na Jeshi la Polisi.
Baraza hilo ni mfano wa kamati ya ulinzi au
mahakama inayojiendesha kwa kufuata miiko na kanuni zake katikati ya
Serikali inayoendeshwa kwa utawala wa sharia, likidaiwa kutoka Kabila la
Wasukuma na jamii ya Kinyantuzu waliopo Mkoa wa Simiyu.
Mmoja wa maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la
Polisi Mkoa wa Simiyu aliyeomba kutotaja jina lake gazetini kwa sababu
za siyo msemaji wa polisi alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo ya
kikatili akishauri atafutwe mhusika ili atoe ufafanuzi kuhusu matukio
hayo.
Hali ilivyo kwa sasa
Mwandishi wa gazeti hili alifanikiwa kufika Vijiji
vya Igangabilili, Nyamiswi, Badugu, Shigala, Budalabujiga na Mikoma
vilivyopo Wilaya za Itilima, Bariadi, Busega na maeneo mengine mkoani
humo.
Hofu iliyopo siyo kwa wanakijiji tu, bali hata
mgeni yeyote, wakiwamo watumishi wa Serikali kama walimu, watakaoonekana
kuwa tofauti na jamii hiyo.
Taarifa zinaonyesha kuwa hata kwa mwandishi wa habari atakayebainika kuingilia utaratibu wao, atakutana na adhabu kali.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyamiswi Kata
ya Gambushi, Leah Muhami anasema kuwa hali ni mbaya na kwamba mbali ya
kuchoshwa na ukatili huo, wanakijiji wamekuwa wakihofia kutoa
ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuogopa kuonekana wasaliti kwa
baraza hilo wakihofu kugharimu maisha yao.
“Yaani wakikusikia unatoa taarifa zao polisi,
lazima maisha yako yatakuwa hatarini. Watakushughulikia na wanapofanya
mauaji hutakiwi kuonekana ukiwa na simu ya mkononi, ”anasema Leah.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Ukatili unavyofanyika
Katibu wa CCM kutoka Wilaya ya Itilima, Jumaa
Iadhi anasema ukatili huo, umekuwa ukifanyika kwa kulipiza kisasi,
ugomvi wa mirathi, mipaka ya ardhi na njama zozote za kupangwa kwa namna
yoyote, hata na watu wenye fedha.
“Kwa mtu ambaye watamhisi au kupelekewa tuhuma za
aina yoyote dhidi yake, watapiga mbiu na kumweka katikati, kisha
watampiga faini ya pesa ambazo anatakiwa kuzitoa papo kwa papo,”anasema
Iadhi.
Anasema kuwa awali, baraza hilo walikuwa
wakikusanya fedha na kuzipeleka kwenye ujenzi wa visima, madarasa au
madawati. “Wakati mwingine imeshakuwa ni kama mradi wao wa kujipatia
pesa za pombe, yaani ni ukatili usiovumilika,”anasema Iadhi.
Mwingine ni Michael Miraji, ambaye ni mkazi wa
wilayani Bariadi anasema kuwa sababu za kukithiri kwa matukio hayo ni
jamii hizo kukosa huduma ya Jeshi la Polisi, kukosekana kwa imani za
kidini na elimu.
“Makanisa na misikiti ni muhimu sana, mbali na
mambo mengine kisaikolojia watu wanajengewa tabia ya ustaarabu, lakini
huku hadi mwenyekiti wa kijiji, unakuta naye hana dini yoyote,” anasema
Miraji.
Anaongeza kuwa umbali uliopo kati ya Kituo cha
Polisi na kijiji ni takriban kilometa 60. “Kwa umbali huo, askari
wamekuwa wakikuta tukio tayari limeshatokea, hivyo ni vigumu sana
kudhibiti, labda Serikali iongeze nguvu kwa mkoa huu wa Simiyu kama
sehemu ya Operesheni Maalumu.
Matukio ya karibuni
Baadhi ya matukio ya hivi karibuni ni pamoja
lililotokea Kata ya Zagayu ambapo wanawake wawili waliteketezwa kwa moto
na baraza hilo kwa tuhuma za ushirikina.
Mbali na tukio hilo, tukio jingine ni la mauaji ya
kuchomwa moto nyumba na familia ya watu watatu katika Kijiji cha
Budalabujiga.
Mmoja kati ya maofisa usalama mkoani humo, ambaye
hakuwa tayari kutajwa jina lake anasema kuwa ingawa ukatili huo
umepungua, lakini bado kuna changamoto kubwa katika vijiji vya Kata ya
N’hobora.
“Juzi kuna wanakijiji watatu waliuawa kwa mapanga
wakihusishwa na ushirikina, pia kuna Kata ya Mkoma imekuwa na mauaji
sana,” anasema na kuongeza:
“Takwimu za matukio hayo zimeanza kupungua kutokana na juhudi za utawala mpya wa Mkoa wa Simiyu ulioanzishwa hivi karibuni.”
Anaongeza: “Mwaka mmoja uliopita tulikuwa
tunapokea taarifa za matukio ya vifo viwili mpaka vitatu vya wanakijiji
kuuawa kikatili kutoka ndani ya kila kijiji, lakini kwa sasa zinaweza
kumalizika siku tatu mpaka wiki hatujasikia.”
Mwalimu wa Sekondari ya Biashara wilayani Bariadi,
Mwangwa Bujiku anasema kuwa ukatili huo umejenga hofu hata kwa walimu
wanaopangiwa kwenda kufundisha maeneo ya vijiji vya mkoa huo.
“Wenyeji wa eneo hili hawapendi mtu anayekuwa
tofauti na wao kiuchumi, hata ukiongea Kiswahili wanaona unajidai. Kuna
mwalimu alipangiwa Kata ya Dutwa, alionekana kuishi tofauti
wakamtengenezea kesi ya kutembea na mwanafunzi,” anasema Bujiku.
Anafafanua kuwa vijana wa baraza hilo waliamua kumpigia mbiu mwalimu huyo na kumpiga faini na kumfilisi kila kitu.
“Yule mwalimu akachukuliwa uhamisho na walikuwa wamepanga kumuua kabisa,”anasema.
Linatumika kwa visasi
Katibu wa Umoja wa Wazazi mkoani humo, Fadhil
Murani anasimulia akisema kuwa mbaya zaidi baraza hilo limekuwa likitoa
hukumu kwa kutumia hisia na tuhuma zisizokuwa na uhakika.
“Halafu mtuhumiwa wakishamweka katikati,
haruhusiwi kujitetea wala kuzungumza chochote, matokeo yake wanamchoma
moto au wanamuua kwa mapanga,”anasema Murani.
Anasimulia kuwa asilimia kubwa ya vijana wa baraza
hilo kwa sasa wanatumiwa na watu wenye fedha katika ugomvi wa mipaka ya
ardhi na mashamba.
“Mfano; kama una adui yako ukapeleka pesa kidogo
kwa wazee wa baraza hilo au ukawanunulia pombe, halafu ukamshtaki mtu,
lazima utasikia yule mtu kavamiwa usiku na kuuawa kwa mapanga au
watampigia Mbiu na kamchoma moto,”anasema Murani.
Mmoja wa wanavijiji kutoka Kata ya Mahuni, Deo
Ngulyati anasema kuwa malengo halisi ya kuwepo kwa baraza hilo yamepotea
kwani limegeuka kuwa adui na hasara katika ustawi wa jamii.
Mwananchi
“Zamani lilikuwa ni baraza linalosaidia ukuaji wa ustawi wa
jamii na kuchochea maendeleo, walidhibiti migogoro, walihamasishana
kwenye misiba na majanga, kujenga huduma za kijamii na walizuia
uhalifu,” alisema Ngulyati.
Changamoto kwa Jeshi la Polisi
Moja kati ya changamoto kubwa na ya muda mrefu kwa
Jeshi la Polisi mkoani Simiyu ni hofu ya kuendelea kusambaa kwa mauaji
na hukumu hizo.
Baadhi ya Askari Polisi mkoani humo wamezungumza
kwa nyakati tofauti juu ya changamoto inayoendelea kujitokeza kupitia
baraza hilo.
Mmoja kati ya askari hao aliyeomba kuhifadhiwa
jina lake, anasema kuwa vijana wa baraza hilo wakishatekeleza hukumu yao
kwa raia hukimbilia msituni na kujificha mfano wa Kundi la Al- Shabaab
wakiwindana na polisi.
Anaongeza kuwa changamoto nyingine iliyopo ni viongozi wa Serikali za Mitaa na viongozi wa kisiasa kutotoa ushirikiano.
“Hakuna mwanasiasa, awe diwani au mwenyekiti wa
kijiji anayeingia bila kushirikisha baraza hilo, kwa hivyo wanapokuwa
madarakani wanakosa ujasiri wa kuwakemea kwa maovu wanayoyafanya,”
anasema askari huyo.
Akichangia hoja hiyo, askari mwingine katika kundi
hilo anasema kuwa kwa sasa kuna baadhi ya wanakijiji wameshaanza kutoa
taarifa za matukio ya mauaji yanapofanyika.
“Tukimkamta mmoja wa vijana wa baraza hilo
changamoto nyingine inajitokeza kwenye ushahidi mahakamani. Hakuna
mwanakijiji atakayekubali kusimama mahakamani kutoa ushahidi, kwa hofu
ya kuuawa. Inabidi mtuhumiwa aachiwe huru kwa kukosa ushahidi,” anasema
askari huyo.
0 comments:
Post a Comment