Mama Maria Nyerere
MJANE wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria amedhulumiwa viwanja vitatu tofauti mjini Dar es Salaam. 

Hali hiyo, imesababisha kuwapo na mgogoro mkubwa kati ya familia ya Nyerere na watu ambao wanadai wameuziwa viwanja hivyo miaka kadhaa iliyopita vilivyo katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, kimoja kikiwa Mikocheni ‘B’ Plot 402 Block C na kingine kipo Msasani Beach Namba 778, ambacho kinadaiwa kugawanywa kwa watu wawili.
Viwanja hivyo, vinadaiwa kuvamiwa na mfanyabiashara maarufu Dar es Salaam, Paul Mushi na mkwe wa Hayati Rashid Kawawa aitwaye Issa Majura Mshangama.

Habari za uhakika kutoka ndani ya familia hiyo, zilizothibitishwa kwa MTANZANIA Jumatano na nyaraka mbalimbali, zinasema kutokana na hali hiyo, Mama Maria amelazimika kuiandikia Serikali barua akitaka msaada wa kurudishiwa viwanja vyake.

Katika nyaraka hizo, zinaonyesha viwanja hivyo ni mali halali ya mtoto wa tatu wa Mwalimu, John Nyerere.

Katika barua yake ya malalamiko kwa Kamishina wa Ardhi ambayo Mama Maria aliiandika Mei 28, mwaka huu inasema; “kijana wangu, John Nyerere ni mmiliki halali na kwamba ana vielelezo kamili vya kisheria.

“Ofisi yako ilimpa Letter of Offer ambayo anayo mpaka sasa. Lakini ameshindwa kujenga katika eneo hilo kwa sababu ya uvamizi wa nguvu wa mtu aitwaye Paul Mushi, ambaye ameweza kuhodhi kiwanja hicho kwa miaka mingi, bila kujali au kuogopa sheria za nchi.

“Kwa vile mwanangu, John anaumwa na hawezi kutetea haki yake dhidi ya mvamizi huyo, nathibitisha kuwa John amemuomba na kumteua George Francis Mlawa ambaye ni mwanasheria, amsaidie kupigania haki hiyo iliyo wazi, lakini anazuiwa kuipata.”

Nyaraka nyingine zinaonyesha kuwa Machi 12, mwaka huu, John alimuandikia barua Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, akikana kufanya mauziano ya kiwanja Na.778 kwa Issa Majura.

Sehemu ya barua hiyo inasema: “Kwanza kabisa nakana kufanya mauziano na ndugu (Issa Majura), kiwanja changu sijakiuza kwa mtu yeyote yule, kama kuna mtu anadai kuwa nimemuuzia anadanganya, naomba aitwe na mimi nije mbele yako athibitishe jinsi nilivyomuuzia kiwanja hicho.

“Ninachokumbuka, ndugu Majura alivamia kiwanja changu baada ya kumuondoa kwenye kiwanja hicho, hajarudi tena mpaka ninapopata taarifa kutoka kwenye ofisi yako kwamba kauziwa kiwanja changu,” ilieleza barua hiyo.

Kwa mujibu wa barua hiyo, John aliiomba manispaa impatie nyaraka zinazothibitisha mauziano hayo, lakini ilishindwa kufanya hivyo.

Miongoni mwa nyaraka hizo, ni pamoja na nakala ya hati ya makubaliano ya mauzo (Deed of Transfer, Sales Agreement), Stakabadhi za kodi za Serikali zilizolipiwa, barua ya toleo aliyopewa Majura na kodi ya malipo (Capital Gain tax) alilipa nani.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya familia hiyo, zilieleza kuwa manispaa hiyo hadi sasa haijatoa nyaraka hizo.

Pamoja na wavamizi hao kuendelea kuhodhi viwanja hivyo, familia bado inaendelea kulipia gharama za ardhi kila mwaka, huku wanaotumia rasilimali hiyo ni wengine.

Chanzo cha habari kilieleza kuwa: “Kwa muda mrefu familia ya Nyerere inafuatilia jambo hili bila mafanikio, tunaona kuna hali fulani ya ukiukaji wa sheria, hawa watu wana fedha nyingi.

“Mushi ni mfanyabiashara, ndio sehemu ya wamiliki wa baa maarufu ya Corner iliyopo Sinza Africasana, inasemekana anahodhi maeneo mengi sasa hatujui anayapata kwa njia kama hii anayoitumia au vipi.

“Ni kweli Majura alikuwa rafiki wa John, kuna kipindi mke wake ambaye ni mtoto wa Kawawa, aliweka kontena kwenye kiwanja cha John cha Msasani Na. 778, baada ya mvutano kontena liliondolewa akaja Mushi akaweka likaondolewa tena.

“Hicho kiwanja kimegawanywa na kutoka viwanja viwili, kimoja kina Na. 782 wamegawana Mushi na Majura.”

Chanzo hicho kilienda mbali zaidi na kueleza kuwa, Manispaa ya Kinondoni iliwahi kubomoa majengo yaliyokuwamo katika kiwanja namba 402, hali ambayo iliifanya familia kuamini kuwa imeshinda vita hiyo.

“Tuliamini kuwa mvamizi ameshindwa, tukaanza kujipanga ili kupaendeleza, sijui jambo gani limefanywa ukienda utashangaa mwenyewe.

“Eneo limeshazungushiwa uzio wa mabati, na ndani kuna biashara inaendelea ya kuuza matofali na saruji,” kilisema.

Chanzo hicho kilieleza kuwa licha ya ucheleweshwaji wa haki hiyo, familia bado inaendelea kufuatilia jambo hilo kwa kufuata misingi na sheria za nchi kama zinavyoelekeza.

MTANZANIA Jumatano ilipomtafuta waziri mwenye dhamana ya Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka simu yake iliita bila kupokelewa.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top