Dk. Joyce Ndalichako
Watahiniwa 3,000 wa kujitegemea wako hatarini kutofanya Mtihani
wa Kidato cha Nne mwaka huu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni
Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kutokuwa na taarifa zao za kulipia
karo za mtihani huo pamoja na zile za usajili.
Tayari Necta imetuma barua kwa watahiniwa hao kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani mwaka huu.
Licha ya maelezo hayo ya Necta, taarifa
zinaonyesha kuwa watahiniwa hao walishalipa ada za mtihani huo kupitia
njia mbalimbali za kielektroniki zilizoainishwa na baraza hilo, ikiwamo
benki na kampuni za simu za mkononi.
Watahiniwa walipaswa kulipa Sh35,000 ikiwa ni ada za mtihani huo kupitia wakala mbalimbali walioteuliwa na Necta.
Gazeti hili lilifanikiwa kuona barua ya Necta
kwenda kwa mmoja wa wanafunzi waliojisajili kufanya mtihani huo kwa
mwaka 2013 ikimweleza kuwa, hataweza tena kufanya mtihani huo kwa kuwa
hakulipa karo ya mtihani huo.
Barua hiyo ilieleza kuwa, kumbukumbu za Necta
zinaonyesha kuwa wanafunzi hao wamejiandikisha kufanya mtihani, lakini
hawajawasilisha fomu za usajili wala kulipa karo za mtihani huo.
“Hivyo kwa barua hii, unafahamishwa kuwa
umeondolewa kuwa mtahiniwa mwaka 2013,” ilisema sehemu ya barua hiyo
zilizosambazwa kwa watahiniwa hao.
Kutokana na kuwepo hali hiyo, baadhi ya watahiniwa
kutoka maeneo mbalimbali nchini, wameanza kufuatilia Necta kujua hatima
yao wakiwa na vielelezo vya malipo yao.
Ofisa Habari wa Baraza la Mitihani Tanzania
(Necta), John Nchimbi alithibitisha kuwa baraza hilo liliandika barua
kwenda kwa watahiniwa takriban 3,000 waliokuwa wamejiandikisha kama
watahiniwa binafsi na kuwaeleza kuwa hawatafanya mtihani huo kwa mwaka
huu.
Alifafanua kuwa, baadhi yao walifika Necta wakiwa
na stakabadhi zilizothibitisha kuwa wamelipa karo hiyo na hivyo
kurudishwa kwenye kundi la watakaofanya mtihani huo mwaka huu.
“Necta hatupokei fedha moja kwa moja, tuna
mawakala, kilichotokea ni kuwa baadhi ya watu walilipa karo za mitihani,
lakini kwenye mfumo wetu tulikuwa hatuoni kama walilipa,” alisema na
kuongeza:
“Kwa hiyo watu wote walioandikiwa hizo barua ni
wale ambao kwenye mfumo wetu hawaonekani kama wamelipa, lakini wengi wa
hawa walikuja na risiti zikionyesha kuwa walikuwa wamelipa na
wakarudishwa kwenye mfumo,” alisema.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Alipoulizwa ni wanafunzi wangapi ambao tayari walikuwa
wamelalamika na kurejeshwa kwenye orodha ya watakaofanya mtihani huo
mwaka huu, Nchimbi alisema mpaka wiki ijayo watakuwa na idadi ya
waliothibitisha kuwa wamelipa fedha hizo.
“Mfumo wetu sisi uko sawa, hauna tatizo lolote. Na
siwezi kusema ni wapi tatizo lilitokea, lakini ninachojua ni kuwa suala
hilo kwa sasa linashughulikiwa,” alisema.
Alieleza kwamba, wiki ijayo wataweza kujua ni
watahiniwa wangapi bado wana matatizo, kwani utaratibu wa kupanga namba
za watahiniwa utakuwa umekamilika.
Alisema pia kuwa, idadi hiyo inaweza kuonekana
kubwa kutokana na baadhi ya walioomba kurudia mtihani huo kuahirisha
kufanya hivyo, baada ya matokeo ya mtihani wa taifa yaliyotangazwa mara
ya pili kuwawezesha kuendelea na kidato cha tano ama mfumo mwingine wa
elimu ya juu.
Alisema kwamba, kwa wale ambao wamepata barua na
walishalipa karo hiyo, wanatakiwa kupeleka stakabadhi zao za malipo hayo
Necta ili warudishwe kwenye kundi la watahiniwa watakaofanya mtihani
huo mwaka huu.
Kwa mwaka 2012 watahiniwa wa kujitegemea
waliosajiliwa kufanya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne walikuwa 68,804
ambapo wasichana walikuwa 34,605 sawa na asilimia 50.30, huku wavulana
wakiwa 34,199 sawa na asilimia 49.70.
Kati ya watahiniwa hao, waliofanya mtihani
walikuwa 61,001 wakiwamo wasichana 30,918 na wavulana 30,083. Watahiniwa
7,803 sawa na asilimia 11.34 hawakufanya mtihani huo.
Hata hivyo, kutokana na matokeo ya mwaka jana kuwa
mabaya zaidi yakilinganishwa na yale ya mwaka juzi, ilitarajiwa kuona
idadi kubwa zaidi ya watahiniwa wakijiandikisha kufanya mtihani huo
mwaka huu kama watahiniwa wa kujitegemea. Jumla ya watahiniwa wote
waliosajiliwa kufanya mtihani huo mwaka jana walikuwa ni 480,029,
wakiwamo wasichana 217,587 na wavulana 262,442 na waliofanya mtihani huo
walikuwa ni 458,139 sawa na asilimia 95.44.
Mfumo wa udahili kwa kutumia mtandao wa kompyuta
ulikwaza pia baadhi ya wanafunzi walioomba kujiunga na vyuo vikuu
mbalimbali chini ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU).
Hivi karibuni Necta ilikumbwa pia na utata katika
matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne yaliyokuwa kwenye mtandao,
hali iliyolazimisha Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako na
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kulitolea
ufafanuzi.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment