IMANI za kishirikina zimegubika kijiji cha Iyela, Kata ya
Mkwamba, wilayani Nkasi, Rukwa, na kusababisha walimu sita kati ya 10
wa Shule ya Msingi Mkwamba kukimbia shule hiyo na kuomba wapangiwe shule
nyingine, ili kuokoa maisha yao.
Wakizumgumza na Tanzania Daima kwa niaba ya walimu wenzao katika
shule hiyo, Josephat Kapandila na Jelazi Kakusa, walisema walimu hao
wakiwamo wa kike wamekimbia baada ya kudai kuingiliwa kimwili na
wanaume kwa imani za kishirikina
Walisema sakata hilo limedumu kwa muda mrefu sasa na wametoa taarifa
ofisi ya kijiji, ili kupata msaada lakini wamekosa ushirikiano.
Kutokana na hali hiyo, waliiomba Ofisi ya Elimu Wilaya kuwasaidia na
ndipo walimu wawili kati ya wahanga wa tukio hilo walipopewa uhamisho.
Walisema kuwa walifikiri baada ya walimu hao wa kike kuondoka shule
ingerudi katika utulivu, lakini vitendo hivyo vimeendelea na walimu
wengine kulazimika kuondoka.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Michael Kapela, alisema licha ya shule
hiyo kukumbwa na matatizo hayo ameshangazwa na ofisi ya elimu wilaya
kukubali kuwahamisha walimu bila yeye kujua.
Alisema kwa kawaida kama mwalimu anaomba uhamisho ni lazima maombi yaanzie
kwake, mratibu kata na kisha ngazi ya wilaya, lakini ofisi ya wilaya
imekuwa ikitoa barua za uhamisho bila wao kushirikishwa na kutaka kujua
tatizo hasa ni nini katika shule hiyo kwa lengo la kulitafutia ufumbuzi.
Afisa mtendaji wa kata hiyo Ghambi Idon alikiri kuwapo kwa tatizo kati
ya wananchi na walimu wa shule hiyo wakituhumiana walimu wa kike
kuingiliwa kimwili kiushirikina.
0 comments:
Post a Comment