HIVI karibuni Tanzania ilikumbwa na aibu kubwa, katika sekta ya elimu, baada ya kushuhudia matokeo yasiyoridhisha kwenye Mtihani wa Taifa (NECTA) wa kidato cha nne (2012), ambapo 60% ya wanafunzi waliofanya mtihani huo walifeli.
Baada ya matokeo hayo mabovu kuwahi kutokea katika historia ya Tanzania, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kupitia kwa Waziri wake Mkuu, Shukuru Kawambwa, walikuja na mkakati wa kuboresha kiwango cha ufaulu wa ‘Matokeo Makubwa Sasa’, kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Lengo la mkakati huo ni kuona kiwango cha ufaulu kinafikia 80% hadi kufikia mwaka 2015, ambapo wamelenga kuboresha mazingira yote ya ufundishaji nchini kwa wanafunzi, ili kuinua kiwango hicho cha ufaulu.

Jumamosi iliyopita, timu yetu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ilimaliza harakati zake za kutafuta nafasi ya kushiriki Kombe la Dunia, mwakani nchini Brazil, ambapo ilifungwa na Gambia mabao 2-0, mchezo uliochezwa Uwanja wa Independent, jijini Banjul nchini Gambia.

Ulikuwa ni mchezo wa kukamilisha ratiba tu, kwani tayari Ivory Coast walishafuzu katika kundi hilo, kwenda katika hatua ya pili ya mtoano, kwa ajili ya kupatikana timu tano zitakazoliwakilisha bara la Afrika kwenye fainali hizo.

Lakini pia mchezo huo ulikuwa unaamua msimamo wa nafasi kwenye kundi, ambapo Morocco wameshika nafasi ya pili nyuma ya Ivory Coast, Tanzania nafasi ya tatu nafasi ambayo itatufanya tuzidi kuporomoka kwenye viwango vya ubora vya FIFA, huku Gambia ikiwa imeshika mkia.

Matokeo hayo yanamaanisha tumeshindwa kwenda kwenye fainali zozote kubwa tokea aondoke kocha Mbrazil Marcio Maximo, ambaye aliipeleka Stars katika fainali za kwanza za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN), ambapo Stars iliishia kwenye hatua ya makundi, baada ya kuzidiwa kete dakika za mwisho na Zambia, ambayo ilifuzu katika hatua inayofuata.

Kinachosubiriwa mbeleni ni Stars kuanza tena mchakamchaka, katika harakati za kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), yanayotarajiwa kufanyika mwakani nchini Morocco, ambapo makundi ya kuwania kushiriki fainali hizo, yanatarajiwa kupangwa hivi karibuni.

Hivi sasa soka la Tanzania lipo kwenye hekaheka ya kupata viongozi wapya watakaoongoza Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), baada ya uongozi wa sasa kufikia ukomo wa kuongoza, ambapo Oktoba 27 mwaka huu watapatikana viongozi wapya watakaowarithi wanaomaliza muda wao katika Shirikisho hilo.

Viongozi wapya watakaoingia madarakani, watakutana na harakati hizo za AFCON, hapa inabidi waweke mikakati mipya, ikiwemo kufumua uozo wote uliopo Stars, kwani inabidi tuje na mikakati mipya na bora kama ile ya Wizara ya Elimu ya ‘Big Results Now’, lengo ni kuiona timu yetu ikipata ufanisi zaidi katika mashindano yote tunayoshiriki mbeleni.

Inasikitisha kuona nchi kubwa kama Tanzania, inasota miaka 33 sasa kushiriki mashindano makubwa duniani, baada ya mwaka 1980 kushiriki kwa mara ya mwisho fainali za Mataifa ya Afrika, zilizofanyika nchini Nigeria, fainali ambazo ni moja ya mashindano makubwa duniani kwa upande wa timu za Taifa.

Mipango mikubwa ya ‘Big Results Now’ katika soka ni kuhakikisha kunakuwa na uangalizi mzuri kwa timu za vijana, ambapo inabidi wapatikane vijana wengi zaidi wenye vipaji na kuendelezwa, pia kile Kituo cha Kulea Vipaji Tanzania (TSA), kifufuliwe na kuwalea vijana hao, kituo ambacho kilimtoa Thomas Ulimwengu, anayecheza TP Mazembe ya Congo DRC hivi sasa.

Pia mkakati mwingine ni kuboresha ligi zote hapa nchini, ili wapatikane wachezaji walioiva na kuifanya Ligi Kuu iwe bora na ushindani kwa timu zote, kwani hivi sasa mfumo uliopo ni mbovu ambao unaangalia zaidi Ligi Kuu na kusahau madaraja ya chini, ambapo mashindano yao ni mabovu na hayatoi wachezaji walioiva.

Tukifanya hivyo tutashuhudia mabadiliko hata kwenye timu yetu ya Taifa, kwa kuwa vinyozi na kuondokana na kasumba ya kila mwaka ya kufanya vibaya, hali iliyompelekea Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ally Hassan Mwinyi kuiita ‘Kichwa cha Mwendawazimu’.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top