Kwa mara ya kwanza katika historia ya Liberia,
wanafunzi wote wamefeli mtihani wao wa mwisho wa sekondari na hivyo
kumaanisha kuwa hakuna hata mmoja ambaye atafuzu kuingia chuo kikuu.
Waziri wa elimu wa Liberia amesema ameshinda kufahamu ni kwa nini hakuna wanafunzi hao wamefeli kiasi hicho.
Zaidi
ya wanafunzi elfu ishirini na watano walianguka mtihani huo ambao
ungewapa fursa ya kujiunga na chuo kikuu cha Liberia ambacho ni moja ya
vyuo vikuu vinavyoendesha na serikali.
Lakini wasimamizi wa chuo hicho wameiambia BBC
kuwa wanafunzi hao hawakuwa makini na ufahamu mzuri wa lugha ya
Kiingereza ambayo ilitumiwa kuwatahini.
Taifa la Liberia linaendelea kujinasua kutokana
na athari za mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyomalizika zaidi ya
miaka kumi iliyopita.
Rais wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf, ambaye
pia ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, amekiri kuwa mfumo wa elimu
nchini humo bado ungali duni na unahitaji marekebisho ya dharura.
Mwandishi wa BBC mjini Monrovia, anasema shule nyingi nchini humo havina vifaa vya kimsingi na waalimu waliohitimu.
Lakini hii ni mara ya kwanza katika historia ya
taifa hilo kwa wanafunzi wote kufeli mtihani huo licha ya kulipa ada ya
usajili ya dola ishirini na tano.
Chuo hicho kikuu ambacho kina idadi kubwa ya
wanafunzi hakitakuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wakati muhula mpya
utakapoanza mwezi ujao.
Lakini wanafunzi wengi wanasema hawajaamini
matokeo ya mtihani huo na waziri wa Elimu Etmonia David-Tarpeh,
ameiambia BBC kuwa anatarajia kukutana na wasimamizi wa chuo hicho ili
kujadili suala hilo.
BBCSwahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment