Waziri wa mambo ya nje wa Syria , Walid Maullem,
amesema anapinga vikali madai kuwa wanajeshi wa serikali ya Syria
walitumia silaha za kemikali.
Maullem, aliyasema hayo mjini Damascus, baada ya
Marekani kudai kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa silaha
za kemikali zilitumika nchini humo.
Bwana
Maullem, amesema wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, wameshindwa kufika
katika eneo la pili linalodaiwa kushambuliwa kwa silaha hizo, baada ya
kuzuiliwa na wapiganaji wa waasi.
Marekani na washirika wake wanajadili uwezekano
wa kuanzisha mashambulio dhidi ya Syria kufuatia madai ya shambulio hilo
la kemikali lililotokea wiki iliyopita.
Waziri huyo amewaambia waandishi wa habari, kuwa
ikiwa nchi yake itashambuliwa kijeshi, kwa misingi ya kuwepo kwa silaha
za kemikali, itakuwa kwa visingizio vya uongo na jambo ambalo halina
msingo wowote.
Amekariri kuwa serikali ya Syria imetimiza ahadi
zote ilizotoa kwa Umoja wa Mataifa kuhusiana na kuruhusu wachunguzi
wake kufika nchini humo na pia kuwapa ulinzi
Awali serikali za Urussi na Uchina, kwa mara
nyingine tena zimetoa onyo dhidi ya kutumia nguvu za kijeshi kutatua
mzozo wa kisiasa unaokumba taifa la Syria.
Onyo hilo limetolewa huku Marekani na washirika
wake wakijadili uwezekano wa kuanzisha mashambulio dhidi ya Syria,
kujibu shambulio lililotokea wiki iliyopita.
Wachunguzi wa UN washambuliwa
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urussi
amesema, jaribio lolote la kutoshirikisha baraza la usalama la Marekani
na kubuni kila alichokitaja kama visingizio ambavyo havina msingi,
litakuwa na athari kubwa katika mzozo huo.
Utawala wa Moscow vile vile umeshutumu uamuzi wa Marekani wa kuhairisha mazungumzo ya kujaribu kutatua mzozo huo wa Syria.
Wachunguzi hao wa Umoja wa Mataifa wanatarajiwa
kuendelea na uchunguzi wao hii leo kwa siku ya pili mfululizo, viungani
mwa mji mkuu wa Damascus.
Jopo hilo la Umoja wa Mataifa lilishambuliwa kwa risasi hiyo jana na mtu mmoja ambaye aliwavizia Magharibu mwa Damascus.
Shirika la habari la Serikali ya Uchina, Xinhua,
limesema kuwa mataifa ya Magharibi, yamechukua uamuzi wa haraka kuhusu
nani aliyehusika na utumizi wa silaha za kemikali nchini Syria hata
kabla ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa kukamilisha uchunguzi wao.
Hapo jana waziri wa mambo ya nje wa Marekani
John Kerry, alitoa matamshi makali kuhusu madai kuwa silaha za kemikali
zimetumika nchini Syria na kusema kuwa waliohusika ni sharti
wawajibishwe.
BBCSwahili
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment