Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda alisafirishwa jana kwa helikopta kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro na kupandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa kujibu mashtaka yanayomkabili.
Ponda jana alianza kwa kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu asubuhi na kufutiwa mashtaka ya uchochezi yaliyokuwa yakimkabili baada ya kusomewa mara ya kwanza Agosti 14, mwaka huu akiwa kitandani katika Taasisi ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kumshtaki.
Alidaiwa kutenda makosa hayo katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano kati ya Juni 2 na Agosti 11 mwaka huu.
Ponda alifikishwa mahakamani hapo saa 12 asubuhi na baadaye alipandishwa kizimbani na kufutiwa kesi hiyo, baada ya Wakili Kweka kuwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya Kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Hata hivyo, baada ya kufutiwa mashtaka hayo, aliendelea kushikiliwa na kisha akachukuliwa na kupelekwa Morogoro ambako pia alisomewa mashtaka ya uchochezi.
Kuwasili Moro
Sheikh Ponda aliwasili kwa helikopta ya polisi na kutua kwenye Uwanja wa Gofu, Morogoro akiwa chini ya ulinzi wa polisi na alipakiwa kwenye gari maalumu ambalo liliongozana na magari mengine matatu ya polisi huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama ukiwajumuisha askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), askari wa upelelezi, Usalama wa Taifa pamoja na mbwa wa polisi na kusababisha shughuli za kazi katika Mahakama hiyo na ofisi za jirani kusimama kwa muda.
Baada ya kufika mahakamani saa tano asubuhi, magari yalisimama kwa takriban dakika 30 kabla ya kumtoa na kumwongoza kwenye Mahakama ya wazi ambayo tayari ilikuwa umejaa watu.
Baada ya kumalizika kusomwa kwa kesi hiyo, msafara uleule ulimrejesha Uwanja wa Gofu saa sita mchana na kupandishwa kwenye helikopta kurejea Dar es Salaam.
Mahakamani Morogoro
Ponda alisafirishwa kwa helikopta ya polisi hadi Morogoro na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi akiwa chini ya ulinzi mkali.

Mara baada ya kumfikisha katika Mahakama hiyo iliyofurika mamia ya waumini na wafuasi wake, Wakili wa Serikali, Bernard Kongola alimsomea mashtaka matatu yanayomkabili.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate alisema: “Agosti 10, mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro Ponda Issa Ponda, aliwaambia wafuasi wake.
“Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Bakwata ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watakuja kwenu na watajitambulisha kwamba wao ni Kamati za Ulinzi na Usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya msikiti yenu na muwapige sana.”
Kongola alisema kauli hiyo ilikuwa ikiumiza imani za watu wengine na kwamba hatua hiyo ni kinyume cha agizo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu lililotolewa na Hakimu Victoria Nongwa Mei 9, mwaka huu ikimtaka kuhubiri amani ndani ya mwaka mmoja na kwenda kinyume na kifungu cha Sheria namba 124 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Ponda alikana.
Katika shtaka la pili, Ponda anadaiwa Agosti 10 mwaka huu katika eneo la Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro aliwaambia Waislamu kuwa Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu.
Alisema Serikali haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo walipokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo na kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine jambo ambalo ni kinyume cha Kifungu cha Sheria 129 cha mwaka 2002, shtaka ambalo pia alikana.
Shtaka la tatu linafanana na lile la pili lakini na upande wa mashtaka ulieleza kuwa maneno hayo yaliumiza imani za watu wengine na kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha Kifungu 390 cha Sheria na Kanuni ya Adhabu namba 35 cha mwaka 2002, shtaka ambalo Sheikh Ponda alilikana. Baada ya kusomwa kwa mashtaka yote matatu, wakili wa Serikali aliiambia Mahakama kuwa upelelezi wa kesi umekamilika na kupanga kesi kuanza kusikilizwa Septemba 2 mwaka huu. Upande wa utetezi uliomba Mahakama kupanga kuanza kusikilizwa kwa kesi Agosti 26, mwaka huu.
Hakimu Kabate aliwapa mawakili kujadiliana na baadaye kuomba kesi hiyo ianze kusikilizwa Agosti 28 mwaka huu.
“Kitendo cha kumuondoa mteja wangu gerezani na kwenda kumsomea shtaka jingine Morogoro nimelilaani. Sijalipenda. Polisi hawakuwa na nia nzuri na Ponda kwa sababu sheria zinajulikana na kila mtu ana haki ya kutetewa,” alisema Nassoro.
Akizungumzia kufutiwa kesi Mahakama ya Kisutu, Nassoro alisema Serikali imeamua kufuta kesi kabla ya kusikilizwa baada ya kuona imeelemewa kwani alishapeleka maombi ya kuirudisha Mahakama Kuu kutoka Kisutu kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na maombi hayo yalipewa namba 11/2013.
Msemaji wa familia, Isihaka Rashidi alisema: “Hawa jamaa wamempeleka Morogoro kwa siri kwa sababu jana (juzi) tulikwenda Segerea hakukuwa na hizo taarifa. Tumekuja kushtuka asubuhi baada ya mke wake kwenda kumpelekea chai na kuambiwa ameondolewa na kupelekwa Morogoro.”
Alisema baada ya kupata taarifa hizo iliwalazimu kuwasiliana na ndugu zao waliopo Morogoro kwa ajili ya kwenda mahakamani kusikiliza kesi hiyo.
Mwananchi

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top