Waziri wa Fedha Dk. William Mgimwa
KAMATI za Bunge zinazosimamia fedha za umma zimeazimia kuwa
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma haiweki uwazi wa kutangaza umiliki
wa mali za viongozi hali inayosababisha viongozi kutoweka wazi mali wanazozimiliki na ni rahisi mtu kuzushiwa umiliki usio wa kweli.
Katika maazimio yao 22 yaliyofikiwa siku ya mwisho wa mafunzo, juzi,
kamati hizo za Hesabu za Serikali (PAC), Serika za Mitaa (LAAC) na ile
ya Bajeti zimependekeza kuwa ni vema sekretarieti ikafanya utafiti wa
umiliki wa mali kwa viongozi wa umma na kuweka taarifa hizo katika
tovuti yake.
Lengo la kufanya hivyo ni kuwawezesha wananchi kuziona mali
zinazomilikiwa na viongozi wao na pale ambapo kiongozi hatakuwa ametoa
taarifa ya umiliki huo basi taarifa hiyo itolewe kwa tume.
Katika maazimio mengine kamati zimekubaliana kuwa kutokana na
kutokuwepo na taarifa sahihi kuhusu deni la taifa, kuna umuhimu wa
kuwakutanisha wadau wakuu wanaohusika hususan Benki Kuu (BoT), Hazina,
Kamati za Bunge na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG).
Hatua hiyo itawawezesha kujua kwa usahihi zaidi ukubwa wa deni hilo.
Vilevile imeamuliwa kuwa serikali ishauriwe kuunda chombo huru
kitakachosimamia deni la taifa.
“Kamati za Bunge zinazoshughulikia usimamizi wa fedha na rasilimali za
taifa zishughulikie zaidi maafisa masuuli hatarishi (risk based) ili
kuleta thamani ya fedha katika utendaji wao. Kamati zishirikiane na CAG
katika kuamua ni afisa masuuli yupi aitwe kukutana na Kamati,”
walisema.
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge na
Tamisemi imetakiwa kuanzisha utaratibu wa kuratibu mikutano na mafunzo
ya wakurugenzi wa halmashauri kwa pamoja kuliko kila wizara kuwaita
watendaji hao katika sehemu mbalimbali kwa muda tofauti na kuwafanya
kutokuwepo ofisini kwa kipindi kirefu.
“Taarifa za mwaka za Kamati za Bunge ziwe na kipengele cha kiwango cha
utekelezaji wa mapendekezo ya kamati yaliyotolewa awali. Kamati
ziwezeshwe kifedha ili ziweze kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yao.
“Kanuni za Bunge zieleze utaratibu wa ufuatiliaji wa maazimio ya Bunge
na namna utekelezaji wake utavyowasilishwa bungeni. Vilevile Bunge
litenge siku ya kuijadili serikali ilivyoshughulikia hoja za kamati za
Bunge. Spika ashauriwe kuhusu umuhimu wa kuunda kamati ya Bunge ya
kufuatilia ahadi za serikali,” alisema mjumbe mmoja na kuungwa mkono na
wenzake.
Serikali iandae mjadala wa kitaifa wa kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana
na vitendo vya rushwa na mmomonyoko wa maadili vinavyoongezeka kwa kasi
hapa nchini.
Vilevile viongozi wa umma na watendaji waongoze kwa mfano kwa
kutojihusisha na vitendo vya rushwa katika kutekeleza majukumu yao.
“Sheria ya “Anti Money Laundering” ya 2006 irekebishwe ili iweke
viwango vya fedha ambavyo mtu anaweza kuingia au kutoka nazo nchini bila
kuziweka wazi. Kuna umuhimu wa Waziri wa Fedha kutengeneza kanuni za
kutekeleza sheria hiyo.
“Benki Kuu iandae mfumo thabiti wa usimamizi wa maduka ya fedha na
kuhakikisha kutungwa kwa sheria inayozuia matumizi ya fedha za kigeni
katika shughuli za kibiashara hapa nchini,” alisema mjumbe akiungwa
mkono na wenzake.
0 comments:
Post a Comment