MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewahukumu
kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya sh milioni 21 vigogo
wanne wa iliyokuwa Kampuni ya Development Entrepreneurship for
Community Initiative (DECI ).
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Alocye Katemana, pamoja na adhabu hiyo
pia ameiagiza serikali ifanye mchanganuo wa mali za DECI ambazo
inazishikilia, kwa kuwa zipo mali zilishikiliwa zisizo za kampuni hiyo
bali za watu wengine.
Alisema kuwa fedha za wateja wa DECI walizopanda zirejeshwe kwa wateja
wenyewe ambao wataonesha uthibitisho wa kweli kuwa walipanda fedha zao
huko.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi, Stewart Sanga na
kusomwa na Hakimu Katemana, washitakiwa walikuwa watano, ambao
ni Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo ole Loitginye, Samwel
Mtares na Arbogast Kipilimba.
Washitakiwa hao walikuwa wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke.
Hakimu Katemana alisema washtakiwa hao ambao ni wachungaji wa makanisa
ya Pentekoste wametiwa hatiani kuanzia wa kwanza hadi wa nne, isipokuwa
mshtakiwa wa tano ndiye ameachiliwa huru baada ya mahakama kumuona hana
hatia katika makosa hayo mawili.
“Mahakama imeridhika kuwa upande wa Jamhuri uliokuwa unawakilishwa na
Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila na Justus Mulokozi, umeweza
kuthibitisha kesi yao na kwa maana hiyo mahakama inawatia hatiani
washitakiwa hao wannne na kumwachilia huru mshitakiwa mmoja, kwa sababu
mashitaka dhidi yake Jamhuri imeshindwa kuyathibitisha,” alisema.
Alisema katika kosa la kwanza kila mshitakiwa atapaswa alipe faini ya
sh milioni tatu au kwenda jela miaka mitatu, na katika kosa la pili kila
mshitakiwa atatakiwa alipe faini ya sh milioni 18 au kwenda jela miaka
mitatu na kwamba mshitakiwa atakayeweza kulipa faini ataachiliwa huru.
Kabla ya hukumu, Hakimu Katemana, aliwapatia nafasi mawakili wa pande
zote mbili kuzungumza chochote, ambapo Wakili wa Serikali, Mwangamila,
alieleza kuwa washitakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na kwamba makosa
waliyoyatenda yana madhara katika uchumi wa nchi, hivyo akaomba wapewe
adhabu kali.
Wakili wa washitakiwa, Ndusyepo, alidai kuwa wateja wake ni mara yao
ya kwanza kutenda makosa hayo ambayo waliyatenda wakati wakiwa katika
harakati za kuwakwamua waumini wao katika lindi la umaskini.
Aliomba mahakama isiwapatie adhabu kali kwani wateja wake hawana uwezo
wa kulipa fidia, ikizingatiwa kuwa wengine ni wastaafu na hawana huwezo
wa kifedha.
Jana saa 7:00 mchana, Wakili Ndusyepo aliliambia gazeti hili kuwa
tayari ndugu wa Domick na Mtares walikuwa wakielekea benki na ofisa wa
mahakama kwenda kulipa faini ili waweze kukwepa adhabu ya kwenda jela.
Juni 12 mwaka 2009, washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa
mara ya kwanza, baada ya vuta nikuvute kati ya viongozi na wanachama wa
DECI .
Wakili Mwangamila alidai washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka
mawili ambayo ni kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume cha
kifungu 111A (1,3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16.
Alidai kuwa, kati ya mwaka 2007 na Machi 2009, katika makao makuu ya
DECI , yaliyopo Mabibo Mwisho, jijini Dar es Salaam, washitakiwa
waliendesha na kusimamia mradi wa upatu katika sehemu tofauti nchini,
kwa ahadi ya kuwapa wanachama wao fedha zaidi ambazo katika mazingira ya
kibiashara ni kubwa kuliko mradi waliokuwa wakiufanya.
Mwangamila alidai kuwa, shitaka la pili ni kupokea amana za umma bila
kuwa na leseni, kinyume cha kifungu cha 6 (1,2) cha Sheria ya mabenki na
Taasisi za Fedha Na. 5 ya mwaka 2006 na kwamba, washitakiwa wote katika
kipindi hicho wakiwa kwenye ofisi zao za DECI , walipokea amana kutoka
kwa umma bila leseni.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment