WAziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mh. Shukuru Kawambwa.

HOTUBA YA WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI, MHESHIMIWA DKT. SHUKURU JUMANNE KAWAMBWA (MB) KATIKA WARSHA YA MPANGO WA MATOKEO MAKUBWA SASA KATIKA SEKTA YA ELIMU ILIYOTOLEWA KWA WATENDAJI WA ELIMU NGAZI YA KANDA, MKOA NA WILAYA.  UKUMBI WA MIKUTANO WA MAKUMBUSHO YA TAIFA. DAR ES SALAAM, AGOSTI 14, 2013
Mhe. Philip Mulugo, Naibu Waziri, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi;
Bw. Selestine Muhochi Gesimba, Kaimu Katibu Mkuu;
Prof. Eustella Bhalalusesa, Kamishna wa Elimu;
Wakurugenzi;
Maafisa Elimu Mkoa na Maafisa Elimu Wilaya;
Wakaguzi Wakuu wa Shule Kanda;
Wakaguzi Wakuu wa Wilaya;
Waratibu Elimu Kata;
Wakuu wa Vyuo Vya Ualimu;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana.

1.0 UTANGULIZI

Napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha katika Mkutano huu muhimu ambao, pamoja na mambo mengine una lengo la kuwandaa katika uzinduzi wa Mpango wa Serikali wa “Matokeo Makubwa Sasa” katika Sekta yetu ya Elimu. Kushiriki kwenu katika uzinduzi kutasaidia sana katika ufanisi na kuhakikisha kuwa elimu itolewayo katika shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu inalenga katika kutoa elimu bora kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mwaliko wenu katika uzinduzi huu umetokana na Serikali kutambua nafasi zenu katika kufanikisha Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa. Mimi, kama Waziri wenu, nina imani nanyi sana. Naamini katika uwezo wenu, na naamini katika mchango wenu mkubwa katika Sekta ya Elimu na katika kazi iliyo mbele yetu. Naomba nanyi muamini hivyo. Mjue kuwa uteuzi wa nafasi mlizonazo haukufanyika kiholela tu, bali ulizingatia uwezo, uwajibikaji, uzoefu mlionao katika masuala ya Elimu nchini, upeo wa kuona mbali, kuthubutu na kutathmini mipango ya maendeleo ya kazi zenu. Kwangu mimi, ninyi ni wadau wangu wakubwa. Kwa hivyo tuingie kazini.

Vilevile, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa kuona umuhimu wa shughuli hii na kuweza kutumia muda wenu muhimu ambao ungetumika kufanya shughuli zingine ambazo pia ni muhimu. Katika siku mtakazokuwa hapa mtajifunza dhana ya “Matokeo Makubwa Sasa/ Big Results Now” katika Sekta ya Elimu.

2.0 HALI YA ELIMU NCHINI

Ndugu Washiriki,

Wote katika nafasi zetu mnaelewa kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inayo mipango endelevu ya kuinua, kuimarisha na kuendeleza sekta ya Elimu. Mifano ni mingi, na kumekuwepo na mafanikio makubwa ndani ya Mipango ya Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM), na Mipango ya Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) na mipango na Mikakati mingine. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na yafuatayo:

2.1 Mafanikio

2.1.1    Mafanikio katika Elimu ya Msingi

i)       kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi katika shule za Msingi kutoka 7,541,208 mwaka 2005 hadi 8,363,386 mwaka 2011. Ambapo watoto wa jinsia zote wamepata fursa ya kuandikishwa katika elimu ya msingi;
ii)    Kuongezeka kwa idadi ya shule za Msingi kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,001 mwaka 2011;
iii)  Kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kutoka 493,636 mwaka 2005 hadi 983,545 mwaka 2011.
iv) Idadi ya walimu wa shule za msingi imeongezeka kutoka 135,013 mwaka 2005 hadi 175,449 mwaka 2011; na
v) Uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi umeimarika kutoka uwiano wa 1:56 mwaka 2005 hadi uwiano wa 1:48 mwaka 2011.

2.1.2    Mafanikio katika Elimu ya Sekondari
i)   Kuongezeka kwa udahili katika shule kutoka wanafunzi 524,325 mwaka 2005 hadi wanafunzi 1,789,547 Mwaka 2011.
ii) Kuongezeka kwa idadi ya wahitimu wa elimu ya sekondari kutoka wahitimu 85,292 mwaka 2005 hadi wahitimu 339,330 Mwaka 2011.

2.1.3 Mafanikio katika Elimu ya Ualimu
i) Kuongezeka kwa udahili wa wanachuo kutoka 16,640 mwaka 2005 hadi 37,698 mwaka 2011;
ii) Kuwepo kwa utoaji wa mafunzo ya Walimu Kazini kuanzia mwaka 2010 (MWAKEM).
iii)        Kuongezeka kwa vyuo vya ualimu visivyo vya Serikali hadi kufikia vyuo 86, mwaka 2012

Ninawashukuru Maafisa Elimu wa Mikoa, Wilaya, Wakaguzi wa Shule na Wakuu wa Vyuo vya Ualimu kutokana na juhudi za uhamasishaji, usimamizi, ushauri na ufuatiliaji katika kufikia mafanikio hayo.

Kwa upande wa Elimu ya Watu wazima, yafuatayo ni baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika utoaji wa elimu;

i)       Idadi ya washiriki walioandikishwa katika madarasa ya Elimu ya Watu Wazima kupitia MUKEJA imeongezeka kutoka 260,502 (wanaume 158,706 na wananawake 101,796) mwaka 2005 hadi washiriki 1,050,517 (Wanaume 499,898 na wanawake 550,619) mwaka 2011;
ii)    Wanafunzi zaidi ya 500,000 waliokuwa MEMKWA wameweza kujiunga katika mfumo rasmi wa shule katika kipindi cha mwaka 2005-2011; na
iii)  Idadi ya wanafunzi wanaosoma elimu ya sekondari kupitia Elimu Masafa na Ana kwa Ana imeongezeka kutoka 10,000 Mwaka 2005 hadi 50,036 mwaka 2011;

2.2 Changamoto

Ndugu Washirki,

Pamoja na mafanikio ambayi tumeyapata katika Elimu, utoaji wa Elimu katika ngazi zilizotajwa umekumbana na changamoto nyingi na za aina mbalimbali. Ninyi mnazifahamu sana. Baadhi ya changamoto hizo ni kama ifuatavyo;

i)  Uandikishaji mdogo wa wanafunzi katika madarasa ya awali;
ii) Msongamano wa wanafunzi darasani katika baadhi ya shule, pamoja na shule za mijini;
iii)  Upungufu wa walimu kwa ujumla na zaidi walimu wa masomo ya Sayansi na hisabati;
iv)  Upungufu wa nyumba za walimu,
v)    Uhaba wa madawati ya wanafunzi;
vi)  Upungufu wa matundu ya vyoo;
vii)  Uchakavu wa miundombinu ya shule;
viii)   Upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia;
ix)  Ufaulu duni wa wanafunzi wanaohitimu mafunzo.
x)    Ongezeko la watu wasiojua kusoma na kuandika waliofikia 31% mwaka 2010

Kumekuwepo kwa watoto 2,500,000 ambao hawana fursa ya kupata elimu ya msingi.

Ndugu Washirki,

Sisi sote tunatambua kuwa zipo changamoto nyingi sana katika Sekta ya Elimu na zilizotajwa ni baadhi tu. Baadhi ya changamoto zinatokana na uhaba wa rasilimali fedha, zingine uhaba na ubora wa rasilimali watu, utendaji wa watumishi na mambo mengine. Leo ningependa nichukue fursa hii kufafanua baadhi ya changamoto ambazo zinagusa utendaji wetu wa kila siku na jinsi ambavyo tungewajibika ipasavyo zingepungua sana au kuzitokomeza kabisa.

Kwa mfano:
2.2.1    Uandikishaji mdogo wa wanafunzi katika madarasa ya awali.
Maafisa Elimu wa Mkoa na Wilaya, changamoto hii mngeweza kuipunguza ama kuiondoa kabisa iwapo mngetekeleza jukumu lenu la kuhakikisha kuwa vipaumbele na malengo yaliyowekwa yanatimizwa kikamilifu katika mikoa yenu.

Kwa mfano mmeelekezwa katika Sera ya Elimu ya mwaka 1995 kuwa kila shule ya msingi inatakiwa kuwa na darasa la Elimu ya Awali. Lakini nani ambaye shule zake zote katika Mkoa/Wilaya zina madarasa ya Elimu ya Awali? Na kama hazipo, je umechukua hatua gani? Au Mkoa wako una mkakati gani kuhusu madarasa ya Elimu ya Awali? Wakaguzi wa shule katika Kanda zenu ama katika Wilaya zenu, je katika ukaguzi wenu mnaonesha shule zisizo na madarasa ya awali? Je ni kwa namna gani mnafanya ufuatiliaji kuona shule inatekeleza maagizo yenu ya utekelezaji wa kuwa na madarasa ya Elimu ya Awali?

Je wakuu wa vyuo ni kwa namna gani mnahamasisha wanachuo wenu kusoma Elimu ya Awali? Kila mtu anahitaji kutafakari kwa nafasi yake na kuchukua hatua.

2.2.2  Mfano mwingine: Msongamano wa wanafunzi darasani katika baadhi ya shule za mijini

Maafisa Elimu wa Wilaya kushindwa kusimamia na kufuatilia mgawanyo wa wanafunzi katika shule ndani ya mji mmoja. Hii ni dalili ya kushindwa kuwahusisha wadau wa elimu katika kupata mafanikio makubwa katika utoaji wa elimu bora.

Shule za mijini zina fikika kwa urahisi naWakaguzi wa shule, je mnazipitia mara ngapi na kushauri kuhusu msongamano unavyoathiri utoaji wa elimu darasani? Kuna malalamiko kuwa hata shule zilizopo jirani na ofisi zenu hazikaguliwi kwa kisingizio cha kukosa pesa. Je tunatimiza wajibu wetu ipasavyo?

2.2.3    Upungufu wa walimu hususani walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati.

Maafisa Elimu kushindwa kutumia fursa za wazi za kuelimisha wanafunzi, walimu na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa kuwepo na uwiano sawiya wa kujifunza masomo ya Sayansi na Sayansi Jamii; na hivyo kuwa na idadi ndogo sana ya wanafunzi wanaosoma masomo ya michepuo ya Sayansi katika Shule za Sekondari. Hii inapelekea kupata idadi ndogo ya walimu wa Sayansi na Hisabati shuleni. Hivi ni kweli miongoni mwenu Maafisa Elimu Mkoa na Wilaya hakuna maafisa wenye uwezo wa kubuni na mikakati ya kupunguza changamoto hizi katika Mikoa na Wilaya zenu?

2.2.4    Mfano mwingine ni Upungufu wa nyumba za walimu, madawati na matundu ya vyoo.

Baadhi ya Maafisa Elimu kushindwa kuwashawishi wadau mbalimbali katika kuwezesha mazingira mazuri na salama ya kufundishia na kujifunzia. Kwa mfano, zipo baadhi ya shule zisizo na idadi ya matundu ya vyoo kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo. Je Maafisa Elimu Mkoa/Wilaya na Wakaguzi wa Shule Kanda/Wilaya, mnatumiaje nafasi zenu na ushawishi wenu kulikabili tatizo hili kwa kutumia fursa za wadau waliopo na rasilimali zilizopo katika maeneo yenu? Nani mnataka awakumbushe kwa hili? Je, zile sifa zilizotumika kukutea zimepotelea wapi? Wapi unatoa kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu yako?

2.2.5    Mfano mwingine ni Ufaulu duni wa wanafunzi wanaohitimu mafunzo

Kumekuwepo na ufaulu duni katika Mitihani ya Taifa, hii inaashiria kwamba kunatatizo katika utendaji wetu hata kama kunasababu nyinginezo, kama vile namna ya kuwatambua watoto wenye mahitaji maalumu ya kujifunza. Napenda tujiulize maswali machache ambayo yatatupelekea kutafakari uwajibikaji wetu:- Je, walimu wakuu na wakuu wa shule tunaowateua wanasifa stahiki? Je walimu wetu wanapofika kwenye ofisi zenu mnawasikiliza ipasavyo? Je, ni lugha gani tunatumia katika kuwasiliana nao? Je tunazungukia shule zetu au tunasubiri mpaka wakati wa kusambaza Mitihani? Je , Wakaguzi wa Shule na Maafisa Elimu ni kwa namna gani mnashirikiana katika kufuatilia utekelezaji wa Mitaala Shuleni na Vyuoni? Je, mnautaratibu wa kufanya tathimini ya pamoja kuhusu matokeo ya mitihani ya Wilaya, Mikoa na Taifa? Nadhani tumekosa utamaduni wa tafakuri ya pamoja ya kuwezesha kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika shule na vyuo vyetu. Ninachotaka kusisitiza hapa ni kuwa Tuwajibike na tubadilike katika utendaji wetu.

2.2.6   Mfano mwingine ni Ongezeko la watu wasiojua kusoma na kuandika

Inashangaza sana kuwepo na wanafunzi wanaofika mpaka darasa la saba pasipo kujua kusoma na kuandika. Halafu Afisa Elimu unawateua wanafunzi wa aina hiyo kwenda Sekondari. Tatizo liko wapi? Uteuzi wenu unazingatia vigezo vipi? Je hakuna namna ya kuthibitisha wale waliochaguliwa wanajua kusoma na kuandika? Maafisa Elimu mnashirikiana vipi na Walimu Wakuu katika hili?Ndugu Watendaji,

Inabidi changamoto zilizopo zitafutiwe njia za kuzipunguza na hatimaye kuzimaliza kabisa. Lazima tuziondoshe Changamoto zinazotukabili katika Sekta ya Elimu. Inafahamika kuwa kila mmoja wenu anafahamu majukumu na wajibu wake katika eneo lake la kazi.

Serikali imeona kuwa haiwezekani hali hii iendelee kama ilivyo na wakati huo huo, itegemee maendeleo yanayotarajiwa na Watanzania. Njia Njia tuliyoichagua mpango wa utendaji kazi utakaoweza kuleta matokeo makubwa na yanayotarajiwa na wananchi. Mpango huu unaitwa, “Matokeo Makubwa Sasa/ Big Results Now”.

3.0 MATOKEO MAKUBWA SASA

Serikali imeamua kuutumia mpango huu katika utendaji kazi wetu ambapo unaelekeza kila mtendaji awajibike kwa kiwango cha juu katika nafasi yake aliyonayo na hivyo kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Katika siku mtakazokuwepo hapa mtaelekezwa mchakato wa utendaji kazi kwa kutumia mpango huu wenye vipaumbele tisa vifuatavyo:

3.1 Upangaji wa shule kwa ubora wa matokeo ya Mtihani Kitaifa kuanzia shule iliyoongoza hadi ya mwisho

Upangaji wa shule kwa ubora wa matokeo ya Mtihani Kitaifa unafanywa na Baraza la mitihani. Katika ngazi ya Mkoa na Wilaya kazi hii itafanywa na maafisaelimu husika. Lengo la upangaji huu ni kuwezesha kila mkoa/wilaya kujitathmini na kupanga mikakati ya kuongeza ubora wa elimu katika mkoa husika. Maafisaelimu na wakaguzi wa shule mnapaswa kufuatilia, kusimamia na kutoa ushauri wa kuwezesha kila shule kutekeleza mtaala kwa ufanisi. Aidha, mosi, utatumia upangaji wa shule kwa ubora wa matokeo ya Mtihani kama kigezo cha uteuzi na kuwabakisha Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kwenye nafasi zao; na pili, kiwe ni kigezo cha kuainisha shule ambazo zitafuatiliwa zaidi ili kuboresha uwajibikaji, kupanda daraja na kuongeza kiwango cha ufaulu.

3.2 Uratibu wa utoaji wa tuzo kwa shule zilizofanya vizuri

Maafisaelimu mnapaswa kuandaa tuzo kwa shule, walimu na wanafunzi ambao watakuwa wamefanya vizuri katika Mitihani yao Taifa. Kadhalika, kwa shule ambazo zitafanya vibaya wahusika wawajibishwe kwa kufuata taratibu za kiutumishi. Aidha, Maafisaelimu mnatakiwa kutumia utaratibu wa utoaji tuzo hata kwa mitihani ya ndani, mfano mitihani ya Mock ya mikoa na wilaya.

3.3Kuwa na Kiongozi cha usimamizi wa shule


Maafisaelimu mnahitajika kuhakikisha kwamba kila shule inakuwa na Kiongozi cha Usimamizi wa Shule. Vilevile, mtahitajika kuweka utaratibu wa ufuatiliaji wa kuhakikisha matumizi ya Kiongozi cha Usimamizi wa Shule kwa kila shule. Aidha, Maafisaelimu ambao mtashindwa kuwezesha shule kutumia kiongozi hicho mtawajibishwa.

3.4 Upimaji wa Kitaifa wa Stadi za Kusoma, Kuandika, na Kuhesabu

Maafisaelimu Mkoa/Wilaya na wakaguzi wa shule mnapaswa kufuatilia, kusimamia na kutoa ushauri kwa mwalimu mkuu katika kuwezesha kila mtoto kuwa na stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu amalizapo darasa la pili. Maafisaelimu Mkoa/Wilaya mtawajibika kwa kushindwa kuwawezesha watoto wote kuwa na stadi za KKK wanapomaliza Darasa la Pili.

3.5 Mafunzo kwa walimu kwa Stadi za Kusoma, Kuandika, Kuhesabu

Wakuu wa vyuo wanatakiwa kuhakikisha kuwa wahitimu wa Mafunzo ya Ualimu Elimu ya Awali wanakuwa na ujuzi wa kufundisha Stadi KKK. Mkuu wa Chuo atawajibishwa kwa kumpitisha mwanachuo kuhitimu Mafunzo ya Ualimu Elimu ya Awali bila kuwa na ujuzi wa kufundisha KKK.

3.6 Kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi katika ufundishaji na Kujifunza

Maafisaelimu Mkoa/Wilaya na wakaguzi wa shule mnapaswa kufuatilia, kusimamia na kutoa ushauri wa kitaalamu na kitaaluma kwa mwalimu mkuu na Mkuu wa shule katika kusimamia utekelezaji wa ufundishaji wa mada mbalimbali zilizomo katika mihtasari ya masomo. Maafisaelimu Mkoa/Wilaya na wakaguzi mtawajibishwa kwa kushindwa kusimamia shule zinazojitokeza kushindwa kukamilisha mada zilizomo kwenye mhtasri wa masomo husika. Hii itajionesha kwa wanafunzi wengi toka wilaya moja au shule moja kushindwa kabisa kujibu maswali ya Mtihani.

3.7 Ujenzi wa miundombinu muhimu ya shule

Maafisaelimu Wilaya mnatakiwa kuhakikisha kwamba ujenzi wa miundombinu inafuata viwango vilivyotolewa na Serikali. Miundombinu inayotosheleza mahitaji ya shule kulingana na idadi ya wanafunzi watakaotumia miundombinu hiyo. Wakaguzi wa shule mnatakiwa kukagua miundombinu ya shule hizo zitakazokarabatiwa na kujengwa.

3.8 Utoaji wa ruzuku ya uendeshaji wa shule.

Maafisaelimu mnatakiwa kuhakikisha kuwa ruzuku ya uendeshaji inafika kwa wakati kwa kiwango kilichoelekezwa na kinatumika kama ilivyoelekezwa. Maafisaelimu ambao watashindwa kusimamia upelekaji na matumizi ya ruzuku tutawawajibisha.

3.9 Motisha kwa walimu.

Maafisaelimu wahakikishe wanajenga mazingira ya kuwa karibu na walimu kwa kuwasikiliza shida zao na kuweza kuzitatua pale inapobidi. Vilevile mnatakiwa kufuatilia madai ya walimu kwa wakati na kuepuka kulimbikiza madeni yasiyo yalazima, mfano, kutoa uhamisho wakati huna tengeo la fedha kwa shughuli hiyo.

4.0    MAAZIMIO

Ndugu watendaji;

Katika kutekeleza vipaumbele hivyo, kila mmoja wenu atakuwa na eneo la kutekeleza na atapimwa kutokana na utekelezaji katika eneo lake. Hii ni katika kuhakikisha kuwa kuanzia mwaka huu wa 2013:

i)   Ufaulu katika elimu ya msingi unaongezeka kutoka 31% hadi kufikia 60%;

ii)  Ufaulu katika shule za sekondari unaongezeka kutoka 43% hadi kufikia 60%; na

iii)   Mwanafunzi wa Darasa la Pili ataingia Darasa la Tatu akiwa anafahamu Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

Ili kufikia azma hiyo inabidi kila mmoja wetu ajipange katika kuangalia upya majukumu yake. Baadhi ya majukumu yatakuwa kama ifuatavyo:

4.1     Majukumu ya Maafisaelimu Mkoa

i)       Kuhakikisha kuwa unafahamu raslimali zilizopo na zinazotakiwa katika utoaji wa elimu kwenye Mkoa wako na zinatumiwa kulingana na matarajio ya utoaji wa elimu bora

ii)    Kuhakikisha kuwa maafisa elimu wanawajibika katika kuhakikisha kuwa vipaumbele na malengo yaliyowekwa yanatimizwa kikamilifu katika mkoa wako; na

iii)  Kuwahusisha wadau wa elimu katika kupata mafanikio makubwa katika utoaji wa elimu bora.

4.2     Majukumu ya Maafisaelimu Wilaya

i)   Kuhakikisha kuwa raslimali zilizopo za utoaji wa elimu bora katika Halmashauri zinatumika vizuri katika kuinua ufaulu ili kufikia malengo yaliyowekwa

ii)   Kuhakikisha kuwa walimu wanafanya kazi ipasavyo

iii)   Kuhakikisha kuwa walimu wanapangiwa kufundisha masomo walio na uwezo wa kuyafundisha

iv)   Kuratibu na kuyashughulikia kwa wakati matatizo ya walimu yakiwemo upungufu wa nyumba, madeni, madaraja na madai mengine ya kiutumishi

v)  Kufuatilia shule zinazofanya vibaya katika mitihani ya kitaifa na kuwahusisha wadau wa elimu katika kutatua matatizo hayo

vi)   Kuwabaini walimu wenye uwezo mdogo wa kufundisha katika baadhi ya mada na kuwajengea uwezo kwa kuwatumia wakaguzi wa shule na wadau wengine

vii) Kuwasiliana na wenye shule katika kuhakikisha kuwa mazingira ya utoaji wa elimu ni rafiki kwa wanafunzi wote ikiwa ni pamoja na utoshelevu wa vitabu vya kiada na rejea, madawati, matundu, nk.

viii) Kushughulikia matatizo ya kinidhamu ya walimu kwa wakati  

4.3  Majukumu ya Wakaguzi wa Shule

i)   Kuhakikisha kuwa shule zinakaguliwa kwa wakati hususani zile ambazo zipo karibu na ofisi za ukaguzi wa shule

ii)   Kukagua shule, kuandika taarifa na kufuatilia kikamilifu utekelezaji kulingana na ukaguzi uliyopita na kupima utekelezaji kulingana na ushauri uliotolewa

iii)   Kubaini shule zinazofanya vibaya katika mitihani ya kitaifa na kushauri ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuwaarifu wenye shule na wadau wa elimu hali ilivyo na ushauri uliyotolewa

iv)   Kubaini shule zinazofanya vizuri na kuwashuri wenye shule na wadau wengine wa elimu ipasavyo ili shule iendelee kufanya vizuri.

4.4  Majukumu ya Mkuu wa Chuo cha Ualimu

i)   Kuhakikisha kuwa raslimali zilizopo katika chuo zinatumika kwa uangalifu zaidi na zinalenga katika kuwawezesha wanachuo kuwa walimu bora.

ii)  Kusimamia utekelezaji wa mtaala wa Elimu ya Ualimu kwa ufanisi,

iii)  Kuhakikisha uwepo wa Miundombinu toshelevu kwa mahitaji ya chuo na shule za mazoezi;

iv)  Kutathmini ubora
wa mazoezi na mitihani inayotolewa chuoni;

v)    Kuhamasisha na kusimamia tafiti ndogo za kielimu zinazolenga kuboresha ufundishaji na ujifunzaji;

vi)  Kubadilishana uzoefu na ushauri na taasisi zingine zinazoshughulika na taaluma ya ualimu ili kukuza kiwango cha taaluma;

vii)   Kufuatilia kila mwalimu mwenye uwezo anafundisha masomo yake kikamilifu na wale wasio na uwezo wanapatiwa mafunzo kazini

viii) Kuratibu kwa wakati matatizo ya wakufunzi yakiwepo ya madeni, madaraja na madai mengine ya kiutumishi na kuyawasilisha kunakotakiwa.

5.0     HITIMISHO

Ndugu watendaji,

Mpango huu unatutaka tufanye kazi kwa ubunifu zaidi kwa kutumia raslimali zilizopo katika maeneo yetu ya kazi. Kwa kufanya hivyo tutapata matunda yanayotarajiwa na Watanzania.

INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO!
Asanteni kwa Kunisikiliza
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top