Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Nchini (Necta), Dk Joyce
Ndalichako
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Nchini (Necta), Dk Joyce
Ndalichako amesema karatasi za majibu ambazo wamekuwa wakizipata kutoka
kwa wanafunzi zinaonyesha kuwa, watoto wengi wanahudhuria shuleni lakini
hakuna wanachojifunza.
Dk Ndalichako aliyasema hayo jana jijini hapa
alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa mabaraza ya mitihani ya Afrika,
ambao umejikita kujadili suala la tathimini ya elimu kwa nchi za Afrika.
Hii ni mara ya kwanza kwa Dk Ndalichako kuzungumza
tangu Serikali itangaze kufuta matokeo ya kidato cha nne mwaka 2012 na
kutaka yapangwe upya, suala ambalo lilipingwa na wadau wengi wa elimu.
Alisema kuwa wakati nchi nyingi za bara hili
zikiwa zimejitahidi kuongeza upatikanaji wa elimu kwa watu, ubora wa
elimu unaendelea kuwa tishio kwa watu wa bara hili kwa vizazi vijavyo.
“Kama mabaraza ya mitihani, tumekuwa tukiona
karatasi za majibu kutoka kwa wanafunzi ambazo zinaonyesha kwa uwazi
kabisa kuwa watoto wanahudhuria shuleni lakini hakuna wanachojifunza,”
alisema Dk Ndalichako.
Kwa upande wake Profesa Justinian Galabawa,
alisema ili kuendeleza elimu, lazima uamuzi wa kitaalamu usiingiliwe na
siasa kwa namna yoyote ile.
Alitolea mfano kitendo cha Serikali kufuta matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka 2012 akisema hakikuwa sahihi hata kidogo.
Alisema lazima vyombo vilivyopewa mamlaka kisheria
kama Necta viachwe vifanye kazi bila kuingiliwa kwani kufanya hivyo
kutaporomosha elimu.
Alisema pia lazima kuwa na sera ya nchi ya kufanya
tathmini ambayo ili ifanye kazi lazima ishirikishe wadau wote na kila
anayehusika kuitekeleza awe nayo.
“Jambo la kwanza ni lazima tuheshimu wataalamu na
wasiingiliwe na wanasiasa, taasisi zilizoundwa kisheria na kupewa
mamlaka ya kupima na kutambua watu ni lazima ziheshimiwe. Kama mtoto
amepata daraja la nne huwezi kumpa la kwanza,” alisema Profesa Galabawa.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar, Seif Ali Iddi alisema mkutano huo ni sehemu nzuri ya Tanzania
kujifunza kutoka kwenye nchi nyingine kujua ni nini watu wengine
wanafanya.
Alisema uzoefu utakaopatikana kutokana na mkutano huu utasaidia katika kujipima na kuendeleza elimu nchini.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo, Philipo Mulugo alisema kwa
siku ya kwanza tu wamebaini kuwa zaidi ya asilimia 80 ya nchi za Afrika
tayari wanatumia mfumo wa usahihishaji kwa kutumia mashine maalumu (OMR)
ambao bado baadhi ya watu nchini wanaulalamikia.
Alisema baadhi ya nchi sasa wameanza kusahihisha
kwa kutumia kompyuta hata maswali ya kujieleza, hivyo akawataka
Watanzania waache kujirudisha nyuma.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment