MKOA wa Kilimanjaro umetajwa kuongoza
kwa wizi wa miundombinu ya umeme katika kanda ya Kaskazini, ambapo katika
kipindi cha mwezi Julai mwaka huu, nyaya za umeme zenye urefu wa mita zaidi ya
3,750, zimeibiwa katika kata ya Kia wilaya ya Hai mkoani humo, na kusababisha
hasara ya zaidi ya shilingi milion 50.
Katika kipindi
cha Januari hadi Julai mwaka huu, shirika la umeme nchini Tanesco, Mkoa wa
Kilimanjaro limepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 100 kutokana na wizi
wa nyaya za umeme, hasara ambayo ni kubwa ikilinganishwa na mwaka jana ambapo
katika kipindi cha Januari hadi Disemba zilipotea milioni 80 kutokana na wizi
wa nyaya.
Hayo
yalibainishwa jana na Meneja Mwandamizi wa Tanesco Kanda ya Kaskazini, Mhandisi
Makoye Ng'erere wakati akitoa taarifa ya matukio ya wizi wa miundombinu ya
umeme kwa waandishi wa habari mkoani hapa ambapo alisema katika kanda ya
Kaskazini inayojumuisha Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga, mkoa wa
Kilimanjaro unaongoza kwa matukio hayo ukifuatiwa na mkoa wa Arusha.
Mhandisi
Ng'erere alisema katika kipindi cha Julai mwaka huu wizi wa miundombinu ya
umeme katika Mkoa wa Kilimanjaro, umefanyika mara tatu mfululizo ambapo tukio
la kwanza lilitokea Julai 13 na nyaya zenye urefu wa mita 750 ziliibwa, Julai
17 nyaya zenye urefu wa mita 1,000 na Julai 21nyaya zenye urefu wa mita 2,000
na kwamba matukio hayo yote yalitokea katika Kata ya Kia wilayani Hai.
"Matukio haya yanasababisha hasara
kubwa kwa shirika hili, na hasara inayotokea si ya fedha tu ni pamoja na
wananchi wanaohudumiwa na shirika hili katika maeneo ambayo yameibiwa nyaya
kukosa umeme na kurusha lawama kwa Tanesko huku tatizo likiwa si letu,
kukosekana kwa usalama kutokana na watu kutumia fursa ya kukosekana kwa umeme
kufanya matukio ya uhalifu na shirika kupoteza heshima kwa wananchi kutokana na
kukatika kwa umeme bila ya taarifa," alisema.
Mhandisi huyo alisema zipo jitihada
mbalimbali ambazo tayari zimeshachukuliwa na Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro
ili kudhibiti matukio hayo ya wizi wa miundombinu ya umeme, ikiwa ni pamoja na
kuundwa kwa kamati ya kupambana na wahalifu hao.
Alisema kamati hiyo ambayo iliundwa
baada ya kikao cha kamati ya ulinzi na usalama mkoani humo kukaa Julai 24 mwaka
huu tayari imefanikisha kukamatwa kwa watu wanne wakiwa na nyaya za umeme
ambazo hazikuweza kufahamika mara moja urefu wake, kutokana na kukatwa vipande
vipande na kuwekwa kwenye mifuko ya 'Salfet' tayari kwa kusafirishwa.
Alisema watu hao ambao w a l i k a m a
t w a n a n y a y a zinazosadikiwa kuibwa katika kata ya Kia wilaya ya Hai,
walikamatwa Julai 26, mwaka huu katika eneo la Kiboroloni Manispaa ya Moshi na
kwamba haijafahamika nyaya hizo walikuwa wakizisafirisha kwenda wapi.
Kufuatia kuendelea kushamiri kwa
matukio ya wizi wa miundombinu ya umeme, shirika hilo kanda ya Kaskazini
limetangaza zawadi ya shilingi 50,000 hadi milioni tano kwa mwananchi
atakayetoa taarifa zitakazowezesha kukamatwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo
vya wizi na kuhujumu miundombinu ya umeme.
Akizungumza Kamanda wa Polisi mkoani
Kilimanjaro, Robert Boaz, alikiri kukamatwa kwa watu wanne kwa tuhuma za
kujihusisha na wizi wa nyaya za umeme.
Chanzo: Majira
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment