Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, amewavua
madaraka maofisa wanne wa Jeshi la Polisi na kumsimamisha kazi mmoja
ambaye atafunguliwa mashtaka ya kijeshi kutokana na kukiuka maadili na
taratibu za jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri
Nchimbi alisema hatua hiyo ni katika kuendeleza vita ya kuhakikisha
jeshi hilo linakuwa na nidhamu, kutekeleza wajibu wake wa kutenda haki
na kuwalinda raia na mali zao.
Alisema kuwa amewachukulia hatua maofisa hao baada ya kuridhia maoni
ya kamati aliyoiunda kufanya uchunguzi wa matukio yaliyolalamikiwa dhidi
ya askari polisi katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na
Kigoma kati ya Desemba 2012 na Mei, 2013.
Waziri Nchimbi alisema kuwa askari wawili, F. 1734 CPL Edward wa FFU
Arusha na G 2434 PC George walifukuzwa kazi tangu Mei 20, mwaka huu, kwa
kosa la kusafirisha bangi kwa kutumia gari la polisi Mei 18, 2013,
maeneo ya Kilema pouf, barabara ya Himo - Moshi mkoani Kilimanjaro.
Aliongeza kuwa Mkuu wa kikosi cha kutuliza ghasia, Ramadhani Giro,
amevuliwa cheo chake kwa kukosa umakini wa kusimamia magari ya polisi
hadi gari namba PT 2025 likatumiwa kwa kusafirisha bangi.
Katika sakata hilo, Inspekta Isaac Manoni, aliyetuhumiwa kumtorosha
mtuhumiwa huyo hatari, kitendo hicho kimetafsiriwa kuwa ni cha
kulifedhehesha Jeshi la Polisi, hivyo amesimamishwa kazi na atashtakiwa
kijeshi.
Inspekta Salum Kingu wa FFU Mkoa wa Kilimanjaro alipewa onyo na
kutakiwa kuwa makini na kazi yake, kwani alibaki kwenye gari umbali wa
mita 80 kutoka nyumba ya mtuhumiwa, hivyo kurahisisha kutoroka.
Hata hivyo Waziri Nchimbi alisema kuwa askari ASP Francis Duma,
aliyekuwa kiongozi katika tukio la kukamata gari la jeshi lililokuwa
limebeba bangi hiyo, amepandishwa cheo tangu juzi huku askari wengine
14 waliokuwa chini yake wakisubiri kupandishwa vyeo au zawadi nyingine
kadiri atakavyoona Inspekta Jenerali wa Polisi.
Katika hatua nyingine, Nchimbi alisema askari E. 4344 D/Sgt Mohamed,
E. 3861 Cpl Nuran wa Kituo cha Polisi Dumila na D. 4807 D/Ssgt Sadiki
Madodo wa Dakawa waliombambikizia fuvu la kichwa cha binadamu
mfanyabiashara Samson Mita, wamefukuzwa kazi na wameshtakiwa kwa uhalifu
waliotenda.
Katika tukio hilo la kubambikiza fuvu, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya
Mvomero, Inspekta Jamal Ramadhani na Mkuu wa Kituo cha Polisi Juma
Mpamba wamevuliwa madaraka waliyonayo kwa kutosimamia vema askari hao
hadi wakaanza kujipangia kazi kinyume cha taratibu.
Vilevije jeshi hilo limewafukuza kazi D. 8622 Cpl Peter na G. 1236 PC
Sunday wa Kituo Kidogo cha Heru Ushingo, kilichopo Kasulu mkoani Kigoma,
ambao walimpiga Gasper Musa na kumweka katika mahabusu hadi alipopoteza
maisha Desemba 26, 2012 kutokana na kupasuka bandama.
“Kwa sasa kuna makanjanja hadi mawaziri, watu wanaojiita mawaziri
kutapeli wafanyabiashara au wafanyakazi wa wizara. Naitaka jamii kuwa
makini na kushirikiana vema katika kuwafichua wahalifu hao wanaotishia
amani nchini,” alisema Nchimbi.
Aidha, kuhusu suala la Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Renatus Chalamila,
Waziri Nchimbi alisema kuwa hatima yake itajulikana hivi karibuni,
kwani kutakuwa na kikao kuangalia hatua gani zilizofikiwa.
0 comments:
Post a Comment