Rais jakaya Mrisho kikwete
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameyapatia ufumbuzi matatizo makubwa na ya
muda mrefu ambayo yamekuwa yanawakabili wahadhiri na wanataaluma wa Vyuo Vikuu
na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini.
Katika
kikao kilichofanyika Ikulu, Dar Es Salaam jana, Jumatano, Agosti 21, 2013 kwa
muda wa saa sita kati ya Rais na Viongozi wa Muungano wa Wanataaluma wa Vyuo
Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini wakiongozwa na Mwenyekiti wao
Prof. Remmy Assey kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine, na kuhudhuriwa pia na Makamu
wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohamed
Gharib Bilal na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Y. Sefue, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aliamua na kuelekeza
ifuatavyo:
(1)
Serikali, kupitia Wizara ya Fedha, ihakikishe
kuwa Bajeti ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma ambayo imekuwa
inapungua mwaka hadi mwaka inarejeshwa kwenye viwango vya zamani mapema
iwezekanavyo, na kwamba bajeti hiyo isiwe inapungua mwaka hadi mwaka kama ilivyo sasa.
(2)
Nyongeza ya fedha hizo itumike kuboresha
mazingira na miundombinu ya kufundishia katika
Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma.
Shughuli hiyo ianze kwa kufanyika tathmini ya kujua vipaumbele, na
kuandaa mpango mahsusi wa utekelezaji.
(3)
Madai ya wanataaluma yatokanayo na stahili
zao, na ambayo yamehakikiwa yalipwe kwa awamu na kazi ya uhakiki wa madeni
mengine iendelee.
(4)
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti
ya Utumishi wa Umma, ishirikiane na Viongozi wa Vyuo hivyo kupitia upya Muundo
wa Utumishi (Scheme of Service) kwa ajili ya wanataaluma kwa lengo la
kuuboresha kwa kuzingatia mahitaji maalum ya wanataaluma.
(5)
Vyuo Vikuu vya Umma virejeshewe uhuru wa
kuajiri wanataaluma moja kwa moja bila ya shughuli hiyo kufanywa na
Sekretarieti ya Ajira Serikalini.
(6)
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma ikutane na Viongozi wa Muungano wa Wanataaluma haraka iwezekanavyo ili
kupata ufumbuzi wa matatizo ya upandishaji vyeo wanataaluma na nyongeza za
mishahara za kila mwaka.
(7)
Utaratibu wa Mikopo ya Ujenzi wa Nyumba kwa
ajili ya Watumishi wa Serikali ulioanzishwa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
uhusishe pia Wanataaluma wa Vyuo Vikuu. Aidha, Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu
Vishiriki vyenye ardhi ya kujenga nyumba za kuishi wanataaluma vijadiliane na
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yenye wanachama kwenye vyuo hivyo ili kuona
uwezekano wa Mifuko hiyo kujenga nyumba za kuishi za wanataaluma kwenye maeneo
hayo.
(8)
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mdhibiti wa
Mifuko hiyo washirikiane haraka na Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma pamoja
na Serikali ili kulipatia ufumbuzi tatizo la uwasilishaji wa michango ya
pensheni ya wanataaluma.
Rais na viongozi wa
wanataaluma hao wamekubaliana kukutana tena baada ya miezi mitatu kupokea taaarifa
ya utekelezaji na kufanya maamuzi kuhusu maeneo mengine yanayoendelea
kuchambuliwa kwa kushirikiana kati ya Serikali, Uongozi wa Vyuo na Uongozi wa Muungano
wa Wanataaluma.
Viongozi wa
Muungano wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vya Umma nchini walimshukuru
Rais kwa hatua hizi na maamuzi yake katika kushughulikia matatizo yao ya siku
nyingi na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuyapatia ufumbuzi
matatizo yaliyobaki.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
22 Agosti,
2013
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment