Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete
Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera kimewafukuza uanachama wa chama hicho, madiwani wake wanane kutokana na kile kilichoelezwa kuwa
ni kukaidi maelekezo mbalimbali ya chama hicho, pia kushirikiana na
upinzani kukihujumu.
Madiwani waliotimuliwa ni wale Manispaa ya Bukoba
ambao wamekuwa wakitajwa kumuunga mkono Mbunge wa Bukoba Mjini ambaye
pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki ambaye
amekuwa akivutana vikali na Meya wa Manispaa hiyo, Anatory Amani.
Miongoni mwa waliotimuliwa ni Mwenyekiti wa CCM
Wilaya ya Bukoba na Diwani wa Kashai, Yusuph Ngaiza, aliyepata kuwa
mbunge wa muda mrefu wa Bukoba Mjini na baadaye Meya wa Manispaa hiyo,
Samuel Ruhangisa ambaye ni Diwani wa Kitendagulo na Diwani wa Buhembe,
Alexander Ngalinda ambaye pia alikuwa Naibu Meya.
Katibu wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Averin Mushi
alisema uamuzi wa kuwatimua madiwani hao umefikiwa jana na halmashauri
ya CCM ya Mkoa kwa kile alichosema ni kwa ajili ya “kulinda masilahi ya
chama na wananchi wa Bukoba”.
Ibara ya 93 (15) ya Katiba ya CCM inataja moja ya
kazi za halmashauri ya chama hicho ngazi ya mkoa kuwa ni: “Kumwachisha
au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho
unafanywa na Halmashauri ya CCM ya Mkoa”.
Hata hivyo kipengele cha 14 cha ibara hiyo ya 93
kinasema hatua ya kumwachisha au kumfukuza mtu uanachama itachukuliwa
endapo halmashauri itaridhika kwamba tabia na mwenendo wake
vinamwondolea sifa za uanachama.
Hatua ya kuwafukuza uanachama madiwani hao ambao
pia watakuwa wamepoteza nafasi zao za udiwani, imekuja siku chache tangu
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alipozitaka pande zinazohusika
katika mgogoro huo kumaliza kwa njia ya mazungumzo.
“Madiwani wote wa CCM walioendelea na mgomo hata
baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kusaini barua ya kutaka
Mkurugenzi aitishe kikao cha kumwondoa Meya tumefikia uamuzi mgumu wa
kuwafukuza uanachama kwa masilahi ya chama na wananchi wa Bukoba,’’
alisema Mushi.
Mushi aliwataja madiwani wengine waliofukuzwa ni
Robert Katunzi (Hamugembe), Deus Mutakyahwa (Nyanga), Richard Gasper
(Miembeni), Mulungi Kichwabuta (Viti Maalumu) na Dauda Kalumuna
aliyekuwa Diwani wa Ijuganyondo.
Katibu huyo alisema Balozi Kagasheki na Meya Amani
ambao mamlaka yao ya uteuzi ni ya kitaifa na wanatakiwa kumaliza
tofauti zao kama walivyoelekezwa na Rais.
Mgogoro uliosababisha madiwani hao kutimuliwa
uliibuka baada ya Kagasheki kumtuhumu Meya Amani kwamba ameingiza
Manispaa katika miradi ya ufisadi hali ilioibua makundi na kukwamisha
kufanyika hata vikao vya Baraza la Madiwani.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment