Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
UAMUZI wa Kituo cha Haki za Binadamu wa kumshitaki mahakamani
Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kauli yake ya kuagiza wananchi wapigwe,
imelitikisa taifa kiasi cha kuisukuma ofisi ya Bunge kumkingia kifua.
Huku idadi kubwa ya taasisi na wanasheria mashuhuri wakiungana na
kituo hicho katika kumfungulia Waziri Mkuu Pinda mashitaka
yanayotarajiwa kufunguliwa kesho jijini Dar es Salaam, Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai amesema jana kuwa hawezi kushitakiwa popote kutokana
na kuwa na kinga ya kibunge inayomlinda.
Katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima Jumatano, Ndugai alisema
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa uhuru wa mawazo,
majadiliano na utaratibu katika Bunge, na uhuru huo hautavunjwa wala
kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika
mahakama, au mahali pengine nje ya Bunge.
“Ninashangaa sana wanasheria hawa, tena ni Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu, wameacha kabisa kufuata sheria, sasa naona wanafanya
siasa, wanatafuta umaarufu tu na mahakama haitaweza kusikiliza kesi
hiyo,” alisema Ndugai.
Hata hivyo, utetezi huo wa Ndugai, umepingwa na wanasheria wengi
waliohojiwa wakisema kuwa tamko la Pinda linavuka mipaka ya kinga za
kibunge, na hivyo anaweza kufikishwa mahakamani kwa tuhuma
zinazomkabili.
Mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya kufuatilia mwenendo wa Bunge, Marcus
Albany pamoja na kukipongeza Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa
hatua hiyo, alisema tamko la Waziri Mkuu Pinda ni la hatari na lenye
madhara makubwa kwa usalama wa nchi.
Albany alisema waziri mkuu anapaswa kuongezewa mashitaka kwa sababu
kauli yake inagusa kosa jingine kwa kulitangazia taifa kuwa serikali
iliyoko madarakani imechoka.
“Waziri Mkuu hakusema piga tu peke yake, bali alisema pia serikali
imechoka, hili nalo ni kosa jingine kwa Waziri Mkuu kulitangazia Bunge
kuwa serikali imechoka halafu hataki kujiuzulu, hivyo ashitakiwe tu,”
alisema.
Mkurugenzi huyo alisema wataungana nao kituo hicho katika mashitaka
hayo kwa sababu yana uzito mkubwa na athari kwa taifa ikiwa
hakutachukuliwa hatua dhidi ya kiongozi huyo kwa sababu yanaweza kuleta
maafa makubwa.
Mwanasheria wa kituo hicho, Harold Sungusia alisema utetezi wa Ndugai
umejaa siasa zaidi na ametafsiri kimakosa kifungu hicho cha katiba
kinachompa kinga mbunge.
“Pinda hataepuka kikombe hiki, ni lazima wafike mahakamani ili mahakama ndiyo iseme kama Pinda alikosea au la.
“Sisi tulijua kuwa watajiegemeza katika kipengele hicho cha kinga ya
Bunge, lakini tunaenda mahakamani kuiomba mahakama ituambie kama kinga
dhidi ya Bunge inamlinda mtu anayevunja katiba, tunataka mahakama
ituambie kama mtu anayesema watu wapigwe ni sahihi au la,” alisema
Sungusia.
Alisema katiba ndiyo sheria mama ambayo Waziri Mkuu Pinda aliivunja
kwa tamko lake la hatari na linaloweza kusababisha vurugu na umwagaji
wa damu. Hivyo hawatarudi nyuma kumfikisha mahakamani.
Aliongeza kwamba kipengele cha katiba alichoshikilia Ndugai bado
kinasisitiza kuwa bila kuathiri katiba, na Waziri Mkuu Pinda hakuvunja
kanuni za Bunge tu, alivunja katiba aliyoapa kuilinda, na hivyo
kipengele ambacho Bunge kinang’ang’ania kipo kinyume cha katiba, na
katiba inasisitiza bila kuathiri.
“Chukulia kuwa ikatokea siku moja mbunge ama kiongozi mkubwa kabisa
akasema wanawake wote wabakwe, asichukuliwe hatua kwa kuwa alisemea
bungeni?
“Ikitokea waziri akaamuru watu wauawe asishitakiwe kwa kigezo kuwa
alisemea bungeni? Tunataka mahakama ndio itoe tafsiri ya kifungu
hicho,” alisema.
Mwanasheria mwingine maarufu ambaye jina lake linahifadhiwa kutokana
na dhamana aliyonayo serikalini, alisema kuwa sheria ya haki na wajibu
inayotekelezwa na mahakama ya mwaka 1994, inatoa mwanya kwa Waziri Mkuu
kushitakiwa hata kwa alichokisema bungeni.
“Hii ni kwa kutumia madaraka ya Mahakama Kuu ya kutengua uamuzi
unaolalamikiwa, ili mamlaka husika itoe amri nini kifanyike au mahakama
ilazimishe jambo fulani lisifanyike (Prerogative of certiorari,
mandamus et Prohibimus),” alisema mwanasheria huyo.
Alisema Pinda alikiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ibara ya 13(2) inayosema: “Ni marufuku kwa sheria yoyote iliyotungwa na
mamlaka yoyote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweka sharti
lolote ambalo ni la kibaguzi ama wa dhahiri au taathira yake.
“Kifungu cha nne cha ibara hiyo hiyo kinasema ‘ni marufuku kwa mtu
yeyote kubaguliwa na mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake
chini ya sheria yoyote au katika utekelezaji wa shughuli yoyote ya
mamlaka ya nchi’. Pinda alitoa kauli hiyo akiwa anatekeleza kazi yake
kama kiongozi wa serikali bungeni.
“Katiba Ibara ya 13 (6) (e) inaonya kuwa ‘ni marufuku kwa mtu
kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au
kumdhalilisha’. Pia Ibara ya 16 ya Katiba inasema ‘kila mtu anastahili
kuheshimiwa na kupata hifadhi ya nafsi yake, maisha yake binafsi na
familia yake na pia heshima na hifadhi ya maskani na mawasiliano yake
binafsi’,” alisema.
Akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini,
Murtaza Mangungu (CCM) katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa
Waziri Mkuu, bungeni Dodoma aliyetaka kujua serikali
inavyoshughulikia tuhuma za vyombo vya dola kutuhumiwa kuwapiga
wananchi kama ilivyotokea Mtwara na kwingineko, Pinda alijibu:
“Ni lile lile nililosema... mwishowe unaona anasema vyombo vya dola
vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi,
utapigwa tu. Hakuna namna nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi
hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi, wewe
ndiye jeuri zaidi, watakupiga tu. Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu
hakuna namna nyingine, maana tumechoka.”
Tamko hilo lililoshangiliwa na wabunge karibu wote wa CCM huku wale
wa upinzani, wakitikisa vichwa vyao kwa masikitiko lilizua malalamiko
mengi kutoka kwa Watanzania wa kada mbalimbali, na wengine kwenda mbali
zaidi wakimtaka kiongozi huyo kujiuzulu.
Ikiwa atafikishwa mahakamani, itakuwa tukio la kwanza katika historia
ya Tanzania kwa Waziri Mkuu kushitakiwa kutokana na matamshi yake
bungeni, ama akiwa nje ya Bunge.
0 comments:
Post a Comment